BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PADRI MKENDA AENDELEA VIZURI, ATOLEWA CHUMBA CHA WAGONJWA MAHUTUTI (ICU) NA KUHAMISHIWA WODI YA KAWAIDA.


HALI ya Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye, Zanzibar, Padri Ambrose Mkenda, ambaye alipigwa risasi juzi na watu wasiojulikana, inaendelea vizuri. 
Kutokana na kuimarika jana, alihamishwa kutoka Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na kuhamishiwa katika wodi za kawaida.

Paroko huyo amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI), kabla ya kutolewa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar alikokuwa amelazwa baada ya tukio hilo.

Akizungumza kwa shida na waandishi wa habari waliopata fursa ya kumuona jana, alisema hali yake inaendelea vizuri.

“Hali yangu, inaendelea vizuri kwani sasa namshukuru Mungu ninajitambua” alisema.

Msemaji wa taasisi hiyo iliyopo ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Almas Jumaa, alisema kiujumla hali ya paroko huyo inaendelea vizuri.

“Anaendelea vizuri, kwa sababu sasa anajitambua na ametolewa kule ICU na kurudishwa katika wodi ya kawaida, lakini hatuwezi kumruhusu aendelee kuzungumza zaidi mpaka tupokee ruhusa ya daktari wake,” alisema.

Serikali yatangaza kuzidisha uchunguzi wa tukio hilo

Siku moja baada ya tukio hilo, Serikali ya Zanzibar imetangaza kuchukua hatua zaidi kwa kuchunguza tukio hilo ambalo ni la pili kwa kiongozi wa dini kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kumtembelea paroko huyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Abood, alisema Serikali imeandaa mkakati kwa kupitia jeshi la Polisi ili kujua iwapo matukio ya aina hiyo, kuwa ni hujuma au laa.

“Nimekuja kumjulia hali Padri, aliyepigwa risasi kujua hali yake ya matibabu na kiafya kama anaendeleaje.

“Kwa kuwa hili ni tukio la pili lenye utata, tunaendelea kuzidisha jitihada kuwabaini wahalifu, hivyo jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha matukio haya.

“Hivi karibuni Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, alimwagiwa tindikali na wahalifu waliofanya tukio hili bado hawajapatikana, hivyo tunataka kujua ni hujuma, wezi au ni watu wanaodhamiria kuvuruga amani ya nchi yetu.

“Iwapo watuhumiwa hao watakamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, pia nataka niwatoe hofu wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, kuwa Jeshi na vikosi vyake limejipanga kuhakikisha wahalifu hawa wanakamatwa haraka iwezekanavyo,” alisema.

Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari inadaiwa kuwa, Padri Mkenda alipigwa risasi juzi majira ya saa 1:30 jioni nyumbani kwake na watu wawili wasiojukana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa.

Katika tukio hilo inadaiwa kuwa, Padri huyo alipigwa risasi kwa kupitia kioo cha mbele ya gari yake aina ya Toyota Rav4, lenye namba za usajili Z 586 AW wakati akirudi nyumbani kwake baada ya kutoka kanisani kuhudhuria misa.

Tukio la kupigwa risasi kwa Padri Mkenda limekuja miezi mitatu tangu Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, amwagiwe tindikali na watu wasiojulikana na kupelekwa kwenye matibabu nchini India.

Matukio ya viongozi wa dini kuhujumiwa yametanguliwa na matukio ya kuchomwa moto baa 12 na makanisa 25 katika maeneo tofauti visiwani Zanzibar.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: