Viwanda, hoteli zaidi nchini kufungwa-Waziri.
KWA UFUPI:
Hatua hiyo imekuja baada ya siku chache zilizopita kuzifungia hoteli mbili kutokana na kukiuka taratibu za utunzaji wa mazingira, ambazo ni Girafee Ocen View, Double Tree.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Terezya Huvisa (wa
kwanza kulia) akikagua mfumo wa maji taka katika Hotel ya Double Tree
jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Waziri ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Rais, Charles Kitwana na Dkt. Robert Ntakamulenga kutoka Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Dkt. Terezya Huvisa.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk Terezya
Huvisa amesema serikali itaendelea na mkakati wa kuzifungia hoteli na
viwanda vitakavyokaidi sheria za uhifadhi wa mazingira.
Pia amesema, anaandaa ripoti atakayoipeleka kwa Makamu wa Rais Dk Mohammed Galib Bilal inayohusu utendaji kazi mbovu wa viongozi wa Jiji la Dar es Salaam unaosababisha kuendelea kukithiri kwa uchafu katika jiji hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya siku chache zilizopita kuzifungia hoteli mbili kutokana na kukiuka taratibu za utunzaji wa mazingira, ambazo ni Girafee Ocen View, Double Tree na Jangwani Resort iliyokaidi agizo la kusimamisha ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dk Huvisa alisema zoezi la kuzifungia hoteli na viwanda ni endelevu ambalo linahusisha nchi nzima.
“Tutapita katika hoteli zote zilizo kandokando ya fukwe na zilizopo katikati ya jiji na miji, ambazo zitabainika kukiuka sheria za uhifadhi wa mazingira sambamba na kuzifungia, zitatozwa faini” alisema Dk Huvisa.
“Tumemkamata aliyekuwa anasimamia ujenzi wa hoteli ya Jangwani na mpaka sasa yuko kituo cha polisi Kawe sambamba, huyo pamoja na mambo mengine atatozwa faini ya Sh35 milioni kwa kudharau amri ya Serikali iliyotaka kusimamishwa ujenzi huo” alisema.
Dk Huvisa alisema kutokana na kuendelea kukithiri kwa uchafu jijini Dar es Salaam huku kukiwa na watendaji wanaotakiwa kuwajibika kukomesha hali hiyo, atapeleka taarifa kwa makamu wa rais kwa ajiri ya utekelezaji zaidi.
“Unajua ningekuwa na uwezo ningeshawafukuza watu kazi lakini kwa kuwa kila kiongozi ameajiriwa na wizara nyingine lakini zote ziko chini ya makamu wa rais basi yeye atakuwa na jukumu la kuchukua hatua zinazostahili” alisema Dk Huvisa ambaye pia ni Rais wa Mazingira barani Afrika.
0 comments:
Post a Comment