kocha wa Kilimanjaro stars kim poulsen
KILIMANJARO Stars na Zanzibar Heroes, leo zinaweza kuandika historia ya kupeperusha bendera moja ya Tanzania kwa kucheza fainali ya Kombe la Chalenji, lakini hilo linawezekana iwapo tu zitashinda mechi zao za nusu fainali leo hii kwenye Uwanja wa Namboole.
Stars itaikabili Uganda, wenyeji wa michuano hiyo katika nusu fainali ya pili, huku Heroes ikipepetana na Kenya katika mchezo mwingine wa hatua kama hiyo utakaoanza mapema.
Stars na Heroes mara ya mwisho zilikutana hatua ya makundi nchini Malawi, na Bara kulala kwa bao 1-0 na hivyo kukosa nafasi ya kusonga mbele wakati Zanzibar haikuwa na la kupoteza kwenye mchezo huo.
Timu hizo pia zinaweza kukutana zenyewe katika hatua ya kuwania nafasi ya tatu, iwapo zote zitapoteza mechi zao mbele ya Kenya na Uganda inayopewa matumaini makubwa ya kutetea taji.
Hata hivyo, dhamira ya kila upande ni kushinda mechi hizo na kucheza hatua ya fainali ili kutwaa taji pamoja na kitita cha pesa kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo, kampuni ya kutengeneza bia aina ya Tusker.
Mtazamo wa kiupinzani unatarajia kuonekana kwenye mechi zote zinazozikutanisha timu kutoka nchi waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku mchezo kati ya Uganda na Tanzania ukionekana kuwa kiini cha ushindani.
Stars yenye kujiamini na kujivunia kiwango kizuri kuwahi kushuhudiwa usoni mwa mwashabiki wa soka miaka ya karibuni, itakuwa na kazi ya kulipa kisasi cha mabao 3-1 walichopata kutoka Uganda kwenye michuano iliyotangulia jijini Dar es Salaam.
Kocha wa Stars Kim Poulsen anatarajiwa kuwapanga viungo wake mahiri Mwinyi Kazimoto na Salum Abubakar ili kuzima mipango ya The Cranes, ambayo hakuna shaka itaratibiwa na Geofrey Kizito na Hassani Waswa.
Ili kuwadhibiti washambuliaji matata wa Uganda chini ya Brian Umony, Kim atampanga Kelvin Yondan kucheza beki ya kati akisaidiana na Shomari Kapombe na pembeni watakuwa Amir Maftah na Erasto Nyoni.
Katika ushambuliaji, Kim ataendelea kuwatumia John Bocco na Mrisho Ngassa wanaoongoza kwa pamoja orodha ya wapachikaji mabao ili kuhakikisha nyavu za The Cranes zinakuwa hatarini ingawa watasaidiwa kwa karibu na Amri Kihemba pamoja na Frank Domayo.
Akizungumzia mchezo huo, Kim alisema kuwa kikosi chake kipo katika hali nzuri kimwili na kiakili kuweza kuikabili The Cranes na kupata matokeo mazuri.
Kwa upande mwingi, Kocha wa Heroes alisema kuwa kikosi chake kina morali ya hali ya juu kushinda mchezo dhidi ya Kenya.
0 comments:
Post a Comment