KWA UFUPI
adra alisema gharama za kuunganisha umeme vijijini katika umbali usiozidi mita 30 bila nguzo sasa itakuwa Sh177,000 na wateja wa mijini watatakiwa kulipia Sh320,000 badala ya Sh455,108 za sasa akisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja wa mijini.
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limetangaza rasmi kupunguza viwango vya kuunganisha umeme kuanzia Januari Mosi, 2013 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyoitoa katika Bunge la Bajeti lililopita.
Ahadi hiyo ya Waziri Muhongo, ilitokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa alipozungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, Machi 2011 ya kulitaka shirika kupunguza gharama za kuunganisha umeme ili kupata wateja wengi zaidi.
Rais Kikwete alilitaka shirika hilo kupunguza gharama hizo ili kuongeza asilimia 30 ya wateja ifikapo mwaka 2015.
Katika tangazo lake lililochapishwa katika gazeti hili leo, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud amesema kupunguzwa kwa viwango hivyo kutasaidia wananchi wengi kuunganisha umeme katika nyumba zao.
Badra alisema gharama za kuunganisha umeme vijijini katika umbali usiozidi mita 30 bila nguzo sasa itakuwa Sh177,000 na wateja wa mijini watatakiwa kulipia Sh320,000 badala ya Sh455,108 za sasa akisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja wa mijini.
Alisema kwa wateja wanaoishi vijijini wanaohitaji umeme wa njia moja na nguzo moja watatakiwa kulipia Sh337,740 wakati wale wa mijini watalipia Sh515,618 badala ya Sh1,351,884 zinazolipwa na wateja hivi sasa.
“Punguzo hilo ni sawa na asilimia 75.02 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio mijini.”
Alisema wateja wa vijijini watakaojengewa njia moja na nguzo mbili watatakiwa kulipia Sh454,654 na wa mijini watalipia Sh696,670, badala ya Sh2,001,422 ambazo zinalipiwa hivi sasa.Alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja wa mijini.
Alisema vifaa mbalimbali vya kuwaunganishia umeme wateja wapya vimekwishawasili katika mikoa na wilaya mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo.
“Tumejiandaa kikamilifu kuwaunganishia wateja wapya, tunafahamu punguzo hilo litawavutia wananchi wengi kuunganisha umeme katika nyumba zao.”
0 comments:
Post a Comment