KWA UFUPI
Hatahivyo, alisisitiza kwamba watu wa kipato cha chini wamekuwa wakitibiwa katika hospitali za hapa nchini kutokana na kukosa kipato cha kutibiwa nje ya nchi na kutaka hali hiyo itumike pia kwa watumishi wengine wa umma.
RAIS JAKAYA KIKWETE.
MKAZI wa Mwandet wilayani Arumeru mkoani Arusha, Emmanuel Masakoi (67) ameshauri itungwe sheria ya kumbana Rais, wabunge na mawaziri ili waweze kutibiwa hapa nchini badala ya nje ya nchi ili taifa liweze kuboresha sekta ya afya.
Akitoa maoni yake juzi mbele ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, mkazi huyo alisema kwamba baadhi ya wabunge na mawaziri wamekuwa wakitibiwa nje ya nchi ilhali wale wasio na uwezo wakitibiwa kwenye hospitali za hapa nchini.
Alisema kitendo hicho kimekuwa kikiwagawa Watanzania katika makundi ya walionacho na wasiyonacho na kutaka Katiba Mpya iwabane watumishi hao ili wasiweze kwenda nje kutibiwa.
Hatahivyo, alisisitiza kwamba watu wa kipato cha chini wamekuwa wakitibiwa katika hospitali za hapa nchini kutokana na kukosa kipato cha kutibiwa nje ya nchi na kutaka hali hiyo itumike pia kwa watumishi wengine wa umma.
Alisisitiza kwamba hospitali za hapa nchini zimekuwa zikitoa huduma kwa hali ya chini kutokana na kukosa huduma bora kama madawa na vifaa kwa kuwa baadhi ya vigogo serikalini wamekuwa hawapati matibabu katika hospitali hizo.
“Mimi napendekeza Katiba Mpya iwabane Rais, wabunge na mawaziri wasitibiwe nje ya nchi, watibiwe hapa hapa kama sisi na nyie mtaona huduma zinaboreshwa, sasa hivi hawana uchungu kwa kuwa wanatibiwa nje,” alisema Masakoi.
Naye, mkazi mwingine wa eneo hilo, Dunstan Kitangiro (60) alisema kwamba Rais apunguziwe madaraka kwa kuwa amekuwa akitumikia nafasi nyingi kama mwenyekiti wa chama chake na amri jeshi mkuu na kupendekeza kwamba aachie baadhi ya nafasi.
0 comments:
Post a Comment