UMOJA wa Ulaya umepokea tuzo ya amani ya Nobel leo mjini Oslo,
ukitambuliwa na kamati ya tuzo hiyo, ambayo imetambua mchango wake wa
kuendeleza utulivu na demokrasia.
Umoja huo umewatuma marais wake watatu katika sherehe hiyo ya mjini Oslo
kupokea tuzo hiyo ya mwaka 2012, ambayo wakosoaji akiwemo mshindi wa
zamani Desmond Tutu wanasema haukustahili.
Lakini mwenyekiti wa kamati
wa kamati ya Nobel, Thorbjorn Jagland amesema kamati yake haikukosea
kuupa Umoja huo tuzo hiyo.
Mwenyekti wa kamati ya Nobel, Thorbjörrn Jagland.
"Umoja wa Ulaya umekuwa nguzo muhimu katika michakato hii ya maridhiano.
Umoja wa Ulaya umesaidia kuleta udugu kati ya mataifa na kuendeleza
mikutano ya amani ambayo Alfred Nobel aliiandika katika wosia wake.
Kwa
hiyo tuzo hii ya amani inastahili na ni muhimu, na sote tunatoa pongezi
zetu," alisema Thorbjorn.
Wajigamba kuwa kinara wa kulinda amani
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy amesema tuzo hiyo ni
ushahidi kwamba umoja huo ni chombo cha kulinda amani cha daraja la
kwanza.
Van Rompuy pamoja na rais wa halmashauri ya umoja huo Jose
Manuel Barroso na rais wa bunge la umoja huo Martin Schulz wamekabidhiwa
tuzo hiyo kwa pamoja.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande
ambao ni viongozi wenye ushawishi mkubwa katika kanda inayotumia sarafu
ya euro, walikaa karibu wakati wa sherehe hiyo na walikuwa wakitabasamu
na kunong'onezana mara kwa mara.
Umoja wa Ulaya unakabiliwa na hali
ngumu ya kiuchumi, kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na mataifa kadhaa
wanachama wa umoja huo hayawezi tena kulipa madeni yake.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy.
Maumivu hayo ya kiuchumi yamesababisha vurugu katika mataifa kadhaa,
hususani Ugiriki ambayo inakabiliwa na kitisho cha kufilisika.
Lakini
kamati ya Nobel ilizingatia nafasi ya umoja wa Ulaya katika kuyaleta
pamoja mataifa yaliyokuwa yanahasimiana katika bara hilo, muhimu zaidi
ikiwa kuzibadilisha Ujerumani na Ufaransa kutoka maadui wakubwa na kuwa
washirika wa karibu.
Kutoka mataifa 6 hadi 27
Kutoka mataifa sita tu yaliyokubali kuzalisha kwa pamoja nishati ya
makaa ya mawe na chuma katika miaka ya 1950 na kufikia 27 leo hii, na 28
pindi Croatia itakapojiunga mwakani, Umoja wa Ulaya sasa unaanzia Ureno
hadi Romania, na Finnland hadi Malta, na unatunga sheria na kanuni
zinazoathiri zaidi ya watu milioni 500.
Kamati ya Nobel ilisema
mgawanyiko kati ya Ulaya mashariki na magharibi umepunguzwa kwa kiasi
kikubwa, demokrasia imeimarishwa na migogoro mingi imesuluhishwa.
Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, amesema tuzo hiyo ni
utambuzi wa mafanikio ya umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka 60, na
pia kuuhamasisha umoja huo kwa ajili ya wakati ujao.
Vijana wanne kutoka
Ulaya akiwemo msichana mwenye umri wa miaka 12 kutoka Uhispania na
mwanamke mwenye miaka 21 kutoka Poland nao walihudhuria sherehe hiyo
baada ya kushinda mashindano. Viongozi 20 wa nchi na serikali za umoja
huo pia walihudhuria.
Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.
Kiasi cha euro 930,000, sawa na dola za Marekani milioni 1.25
zinazotolewa sambamba na tuzo hiyo zitagawiwa kwa miradi inayosaidia
watoto walioko katika maeneo yenye vita, ambapo wapokeaji watatangazwa
mwakani.
Umoja wa Ulaya umesema utajaliza fedha hizo za zawadi na
kufanya jumla ya fedha zitakazotolewa kwa miradi itakayochaguliwa kuwa
euro milioni mbili.
Uamuzi huo umewanyamanzisha wakosoaji katika mtandao wa Twitter na
mitandao mingine ya kijamii ambao hapo awali walikuwa wakitania kwamba
kama tuzo hiyo ni ya raia wote wa Ulaya, basi wote wanapaswa kugawana
fedha za zawadi ambapo kila moja angepata euro 0.2.
Sauti zaidi zapinga Umoja wa Ulaya kupewa tuzo hiyo
Kansela Angela Merkel (wa tatu kushoto) akishikana mikono na rais
Francois Hollande wa Ufaransa (wa tatu kulia) wakati wa sherehe ya
kukabidhi tuzo hiyo.
Si watumiaji wa mtandao pekee wanaokosoa tuzo hiyo kutolewa kwa umoja
huo, Desmond Tutu kiongozi wa Kanisa ambaye alipambana dhidi ya ubaguzi
wa rangi katika nchi yake ya Afrika Kusini, alisema wiki iliyopita kuwa
umoja huo haukustahili kupata tuzo hiyo.
Siku ya Jumapili, karibu watu
1,000 wanachama wa vyama vya mrengo wa kushoto na makundi ya haki za
binaadamu walianadamana katika mitaa ya jiji la Oslo wakisema Umoja wa
Ulaya siyo mpokeaji anayestahili wa tuzo hiyo chini ya masharti ya
Alfred Nobel aliyoyabainisha katika wosia wake mwaka 1895.
"Alfred Nobel alisema tuzo hiyo laazima itolewe kwa wale wanaofanya kazi
kwa ajili ya kuondoa matumizi ya silaha," alisema Elsa-Britt Enger,
mwenye umri wa miaka 70 ambaye anawakilisha shirika la 'Grandmothers for
Peace' na kuongeza kuwa Umoja wa Ulaya haufanyi hivyo.
Alisema umoja
huo ndiyo moja ya watengenaji wakubwa wa silaha duniani.
0 comments:
Post a Comment