Kiwango cha kufaulu chaongezeka, 203 wafutiwa matokeo, Waziri Kawambwa asisitiza mitihani ya majaribio.Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
WANAFUNZI WA DARASA LA SABA SHULE YA MSINGI MWERE MANISPAA YA MOROGORO WAKIFANYA MTIHANI WA TAIFA WA SOMO LA HISABATI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI MWAKA HUU.
HATIMAYE matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2012 yametangazwa, huku wasichana wakifanya vizuri zaidi kuliko wavulana. Mbali ya wasichana kuongoza, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 58.28 mwaka jana, hadi asilimia 64.78 mwaka huu.
Akitangaza matokeo hayo mjini Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema jumla ya wanafunzi 560,706 kati ya 865,534 waliofanya mtihani, wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari za Serikali.
“Idadi hii, ni sawa na asilimia 64.78 ya wanafunzi waliofanya mtihani, aidha kati ya wanafunzi hao waliochaguliwa, wasichana ni 281,460 sawa na asilimia 50.20 na wavulana ni 279,246 sawa na asilimia 49.80.
“Takwimu hizi, zinaonesha idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kwa asilimia 8.8, ikilinganishwa na wanafunzi 515,187 waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka 2011,” alisema.
Alisema katika mtihani huo ambao ulifanyika kuanzia Septemba 19 hadi 20 mwaka huu, jumla ya wanafunzi 894,839 wa shule za msingi walijisajili kufanya mtihani huo, wakiwamo wasichana 468,583 sawa na asilimia 52.37 na wavulana 426,256 sawa na asilimia 47.63.
“Watahiniwa 865,827 sawa na asilimia 96.76 ya waliosajiliwa walifanya mtihani, kati yao wasichana walikuwa 456,082 sawa na asilimia 52.68 na wavulana walikuwa 409,745 sawa na asilimia 47.32.
“Watahiniwa 29,012 sawa na asilimia 3.24 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo utoro, vifo na ugonjwa. Kati yao wasichana ni 12,501 sawa na asilimia 2.67 na wavulana ni 16,511 sawa na asilimia 3.87,” alisema.
Alisema katika matokeo hayo, yanaonesha kuwa, alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.
“Matokeo haya, yanaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 3,087 walipata alama za daraja la A, wakati wanafunzi 40,683 walipata daraja la B.
“Jumla ya wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja la C na 526,397 walipata alama za daraja la D na watahiniwa waliobaki 73,264 walipata alama E,” alisema.
Alisema katika matokeo hayo, yanaonyesha idadi za shule za Serikali ndizo zilizofaulisha wanafunzi wengi zaidi ya shule binafsi.
203 wafutiwa matokeo kwa udanganyifu
Pia Dk. Kawambwa, alisema takwimu zinaonyesha idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo, vimepungua.
“Kwa sababu waliofutiwa matokeo mwaka 2012, ni watahiniwa 293 tu ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliofutiwa matokeo kwa udanganyifu mwaka 2011.
“Kutokana na udanganyifu huu, Serikali itawabaini wale wote waliohusika katika udanganyifu huo na kuwachukuliwa hatua stahiki,” alisema.
0 comments:
Post a Comment