Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene Dec 16 aliitaka Tanesco kuacha kununua nguzo za umeme nje ya nchi na badala yake kununua nguzo zinazopatikana hapa nchini, shirika hilo limeibuka na kusema litatekeleza agizo la waziri huyo bila kusita.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, Felchesmi Mramba alisema juzi jijini Dar es salaam kuwa, agizo hilo litaiwezesha Tanesco kutumia nguzo za ndani kusambaza umeme kwa wadau.
Alisema uamuzi huo utapunguza gharama za ununuzi wa nguzo na kuinua biashara ya kampuni zinazozalisha bidhaa hizo hapa nchini.
Kama tulivyosema hapo juu, hii ni hali ambayo siyo ya kawaida. Kitendo cha viongozi wa Tanesco kufurahia agizo hilo la waziri pasipo hata kuhoji jambo lolote katika utekelezaji wake ni ishara kwamba viongozi hao huko nyuma walikuwa wakilihujumu shirika hilo kwa makusudi kwa kununua nguzo za umeme kutoka nje badala ya nguzo zinazozalishwa hapa nchini.
Kama kweli zilikuwapo sababu za msingi kibiashara kununua nguzo kutoka nje na kuziacha za ndani, viongozi wa shirika hilo wasingesita kutoa hoja za kupinga msimamo wa Serikali na baadaye kulazimika kuukubali shingoupande.
Jambo la ajabu ni kwamba viongozi wa Tanesco sasa wamefanya usanii wa kuikumbatia hoja ya Serikali na kuifanya iwe yao na ndiyo maana mkurugenzi wake mkuu anasema shirika lake limeamua kufanya mabadiliko ndani ya shirika kwa kutumia nguzo za hapa nchini badala ya kununua za nje.
Baada ya agizo hilo la Serikali, sasa ndipo shirika hilo linajifanya kutambua kuwa, hatua hiyo ya kutumia nguzo za ndani italipunguzia gharama na kuboresha masoko ya ndani pamoja na kuleta ushirikiano mzuri kati ya shirika hilo na wazalishaji wa nguzo.
Hivi sasa shirika linajiandaa kutangaza zabuni za ununuzi wa nguzo za hapa nchini kama zilivyo taratibu, ikiwa ni pamoja na kushindanisha kampuni zitakazojitokeza.
Tunaipongeza Wizara kwa kusimama kidete kukata mizizi ya kifisadi katika wizara hiyo.
Tangu uongozi wa wizara hiyo ulipoteuliwa miezi michache iliyopita, tumeona kasi, nguvu na ujasiri wa ajabu wa viongozi hao katika kupambana na vitendo vya wizi, hujuma, rushwa na ubadhirifu katika wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwamo Tanesco.
Itakumbukwa kwamba Tanesco ilifika mahali ikajiweka juu ya sheria na Serikali na kufanya vitendo vya kifisadi pasipo kukemewa na mamlaka yoyote, ikiwamo Ewura.
Kwa shinikizo la Tanesco, Serikali ilitunga sheria ya kuliruhusu kupandisha bei ya umeme kila mwaka, tena kwa viwango vikubwa ajabu.
Serikali bado ina kazi ngumu kuirudisha Tanesco katika mstari ulionyooka wa maadili mema.
Bado hujuma ni nyingi. Kwa mfano, ‘Operesheni Wezi wa Umeme’, ambayo ilipata mafanikio makubwa sasa imekwama kwa sababu wakubwa hawana faida nayo, kama ambavyo imekuwa kwa shirika hilo kushindwa kukusanya madeni ya Sh300 bilioni.
Hata hivyo, kwa nini shirika hilo likusanye madeni au liwatoze faini wezi wa umeme ikiwa limeruhusiwa kisheria kupandisha bei ya umeme kila mwaka ?.
Ni matumaini yetu kwamba hatua hiyo ya Serikali ya kuitaka Tanesco itumie nguzo za ndani litashusha gharama za usambazaji wa umeme kwa wateja.
Ni matumaini yetu pia kwamba Serikali itahakikisha bei ya umeme inashuka kutokana na kupatikana kwa kiwango kikubwa cha gesi.
Sasa ndiyo tumejua kwamba kumbe Tanesco ilikuwa ikijihujumu yenyewe.
0 comments:
Post a Comment