MCHEZAJI WA SIMBA, MRISHO NGASSA KULIA AKIWATOKA WACHEZAJI WA PRINSON YA MBEYA WAKATI WA MICHEZO YA LIGI KUU TANZANIA BARA MZUNGUKO WA KWANZA UWANJA WA TAIFA JIJINI DAR ES SALAAM.
AZAM FC imesema ipo tayari kusitisha mkataba na El Merreikh ya Sudan na kuwauzia Yanga, straika Mrisho Ngassa kwa Dola 80,000 (Sh.126 milioni). Ngassa amekubali kujiunga na El Merreikh baada ya kufikia makubaliano ya mshahara na dau la usajili na Azam nao tayari walishakubali na kusaini mkataba wa Dola 75,000 (Sh. 118 milioni). "Yanga au timu nyingine yeyote wakija na dau kubwa zaidi ya El Merreikh tutakuwa tayari kuwapa Ngassa," alisema Meneja wa Azam, Patrick Kahemele akiwa nje ya nchi jana Jumatatu. Mchezaji huyo alitakiwa kwenda Sudan wiki hii kupima afya, lakini Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF, likaamuru asiende baada ya kupata barua ya malalamiko kutoka kwa Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo. Kahemele aliiambia Mwanaspoti kwamba kama Yanga wakifika dau la Dola 80,000 (Sh126.3 milioni) wapo tayari kuwapa Ngassa, lakini viongozi wa Yanga jana Jumatatu hawakupenda kuzungumzia kabisa suala la Ngassa. Hata hivyo, habari za ndani zinasema kwamba Merreikh walitazamiwa kutua Dar es Salaam kwa mara nyingine jana Jumatatu jioni na kuna uwezekano wakaongeza dau kwa Azam kufikia Dola 100,000 (Sh157.9 milioni) ili mchezaji huyo aondoke haraka. Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema: "Sisi hatuna tatizo na Azam wala Ngassa. Hizo pande mbili zije tukae mezani tuelewane hata kama wataturudishia kile kiwango tulichowapa lakini itabidi waongeze kidogo kama fidia kwavile sisi tutaathirika, ingawa mchezaji alitoka kwao." |
0 comments:
Post a Comment