ADAI HAWATAFUTI UMAARUFU BALI WANAPINGA
DHULUMA.
DK SLAA.
KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
amesema suala la gesi asili linaleta mvutano kwa sababu ya maslahi ya watu
wachache.
Watu wanaoendekeza mgogoro katika sakata hilo ni wale
waliofilisika kifikra, hawajui Katiba na hawajui kuwa wananchi ndio walinzi wa
kwanza wa rasilimali zao.
Alisema kuwa wanaokuja na hoja ya kusema ni siasa, wanakurupuka
kwani wao kama wanasiasa ni lazima kupiga kelele kupinga dhuluma inayotaka
kufanywa na serikali dhidi ya wananchi hao.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Dk. Slaa, alisema Katiba ya
nchi pamoja na udhaifu iliyonao, imeainisha vema misingi ya kusimamia
rasilimali za taifa kwa usawa bila ubaguzi wala dhuluma.
Alisema kuwa katika suala hilo hawatafuti umaarufu wowote wa kisiasa, na
hivyo kuhoji ni nani anaweza kutafuta umaarufu katika shida za watu ?.
Dk. Slaa aliongeza kuwa Mtwara ni sehemu tu ya Tanzania, hivyo wananchi
wa huko na Lindi wana haki ya kunufaika na rasilimali iliyopatikana kwao.
“Serikali inasisitiza kujenga mitambo Kinyerezi kwa kuwa wanataka kuleta
gesi hiyo Dar es Salaam ili kunufaika wao kwanza, jambo ambalo ni la
kiubaguzi,” alisema.
Kwa mujibu wa katibu huyo, serikali ingekuwa wazi kwa kuwaambia wananchi
inalinda Katiba ipi; maana iliyopo inawapa wananchi haki ya kulinda rasilimali
zao na kunufaika nazo.
Alifafanua kuwa mkazo unaopaswa kuwepo kwa maendeleo ya taifa,
unazungumzia kuondoa maadui watatu yaani ujinga, maradhi na umaskini.
“Wananchi wa Mtwara ni maskini, mkoa wao umetelekezwa muda mrefu,
wamekopwa korosho yao, sasa wamepata gesi na wanayo haki ya kudai wanufaike
nayo ili nao wapate viwanda, shule na hospitali nzuri,” alisema.
Dk. Slaa alisema mikoa hiyo haijawahi kuwa na hospitali ya rufaa, hivyo
wanaionya serikali isiendeshe shughuli za uchumi kwa maslahi ya watu wachache.
Alisisitiza kuwa hakuna sababu za kutokuwekeza mitambo ya gesi Mtwara na
Lindi ili isaidie ukuaji wa maeneo hayo kiuchumi na kwamba jambo hilo wala
halina siasa.
Alisema ni jukumu la kila mwananchi kulinda utajiri wa taifa lake kwani
wao ndio wamiliki, hivyo hawapaswi kutegemea hisani ya serikali na badala yake
serikali inapaswa kuwajibuka kwao.
Kauli hiyo ya Dk. Slaa inakuja siku chache baada ya Waziri wa Nishati na
Madini kuwabeza wananchi wa Mtwara walioandamana wakiongozana na baadhi ya
wanasiasa kupinga usafirishwaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Desemba 27, wananchi wa Mtwara waliandamana kupinga hatua ya serikali
kutaka wasafirishe gesi hadi Dar es Salam na kuwaacha wao wakiwa hawana kitu.
Januari 2, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo,
akizungumza na waandishi wa habari alipinga hatua hiyo ya wananchi na kusema
jambo hilo limevamiwa na wanasiasa.
“Hiyo gesi inayowafanya wanasiasa wawashawishi wakazi wa Mtwara
kuandamana haiko Mtwara wala Lindi, bali iko katika mipaka ya Tanzania ndani ya
kina kirefu cha bahari na kwa hilo kila Mtanzania ana haki ya kutumia,”
alisema.
Waziri Muhongo alisema ni jambo la kusikitisha kuona wakazi wa Mtwara
wakiandamana kwa ajili ya gesi wakati walipa kodi wa Tanzania hawajaandamana
kwa ajili ya rasilimali zinazotoka maeneo mengine kwenda kutumika Mtwara.
Alikwenda
mbali na kulaumu kile alichokiita wanasiasa kujiingiza katika sakata hilo na
kuwahimiza wananchi waandamane.
CHANZO http://www.freemedia.co.tz
0 comments:
Post a Comment