BENDERA YA NCHI YA KENYA.
BALOZI WA KENYA NCHINI TANZANIA,MUTINDA MUTISO.
Dk Steven Ulimboka akiwa chumba cha wagonjwa mahututi MOI.
UBALOZI
wa Kenya nchini, umesema unajiandaa kutoa taarifa rasmi ya kiofisi kuhusu raia
wake, Joshua Mlundi, anayekabiliwa na kesi ya kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Madaktari Dk. Stephen Ulimboka.
Ubalozi huo umetoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana juu ya
sakata linalomkabili raia huyo wa Kenya, ambaye mapema wiki hii, aligoma na
kupanda juu ya paa la gereza kupinga kunyanyaswa na kutotendewa haki katika
mashtaka yake.
Kitendo hicho kilisababisha raia huyo kupata kipigo kikali na
kulazimika kuhamishwa na kuwekwa sehemu ya siri kwa sababu ambazo hazijawekwa
wazi na Idara ya Magereza nchini.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa masharti ya kutotajwa jina,
katika ofisi za ubalozi huo jana, ofisa mmoja katika ubalozi huo alisema tuhuma
za raia wao ni nzito na zitajadiliwa kwa kina na kisha kuzitolea ufafanuzi.
Ofisa huyo, alisema balozi wa Kenya nchini, na msemaji wake jana
walikuwa katika kikao, hivyo ilikuwa vigumu kupatikana, lakini akakiri kuwa
wanafuatilia kwa makini mkasa mzima wa tuhuma za Mlundi na yale yanayoendelea
akiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Raia huyo wa Kenya anayeshikiliwa kwa tuhuma za kumteka, kumtesa
na kutaka kumuua Ulimboka na ambaye yuko mahabusu, aliliambia gazeti hili kuwa
anataka upelelezi wa kesi yake ukamilike haraka, ili atendewe haki, lakini
kubwa kuliko yote anaitaka serikali imlete Dk. Ulimboka mahakamani ili aweze
kumtambua.
Mwanzoni mwa wiki hii akizungumza kwa kificho kwa njia ya simu
kutoka ndani ya gereza la Keko alikohifadhiwa, raia huyo wa Kenya alisema ameamua
kutoa kauli hiyo baada ya kusoma taarifa ya gazeti hili zilizoonyesha polisi
wakirushiana mpira na kutoa kauli zinazopingana kuhusu tukio la Dk. Ulimboka.
Alisema hadi sasa haoni maendeleo ya kesi hiyo kwani kila
ikifika mahakamani, upande wa mashtaka hutoa hoja ya kutaka iahirishwe kwa
madai kuwa upelelezi haujakamilika.
“Kila ninapoenda mahakamani naiomba mahakama imlete Dk. Ulimboka
anitambue, nahoji kwa nini upelelezi haujakamilika.
Kwa bahati mbaya sana siku
hizi kesi hii inapokuja mahakamani, hata vyombo vya habari havijulishwi.
Nashukuru Mungu nimepata namba zenu za simu kutoka kwenye gazeti lenu ili nitoe
ya moyoni...
“Naomba Dk. Ulimboka aletwe mahakamani ili anitambue, kama
atasema mimi ndiye niliyemteka na kumtesa, basi kesi iendelee na sheria ichukue
mkondo wake, kama atasema sikuhusika, basi kesi iishe maana sioni sababu ya
mimi kuteseka hapa gerezani kwa kusubiri upelelezi ambao haujulikani utaisha
mwaka gani.
Wiki hii gazeti hili liliandika kuwa kijana huyo Mkenya aligoma
akishinikiza madai yake kusikilizwa.
Askari mmoja wa gerezani humo
alilithibitishia gazeti hili na alinukuliwa akisema,
“Ni kweli huyo Joshua
Mlundi amegoma, uongozi wa gereza umefanya juhudi za kuzungumza naye na kilio
chake anasema anataka upelelezi wa kesi yake ukamilike haraka ili atendewe
haki, lakini kubwa kuliko yote, ameitaka serikali imlete Dk. Ulimboka
mahakamani ili aweze kumtambua,” alisema askari huyo.
Kova kuanika mbichi, mbivu leo
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar
esSalaam, leo linatarajia kufumbua kitendawili cha muda mrefu juu ya hatima ya
tume iliyoundwa na jeshi hilo kuchunguza kutekwa, kuteswa, kupigwa, kuumizwa na
kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwe Pande kwa Ulimboka, tukio lililotokea
Juni 26 mwaka jana.
Mbali na kutegua kitendawili hicho pia jeshi hilo litatoa ripoti
ya jopo la wapelelezi wa jeshi hilo waliopewa jukumu la kuchunguza madai ya
kuwepo kwa askari waliokimbia na mfuko wa fedha kiasi cha sh mil. 150 katika
tukio la ujambazi lililotokea mwishoni mwa mwaka jana katika eneo la Kariakoo
ambapo watu wawili walifariki.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa njia
ya simu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema leo ni
siku ya Watanzania kukata kiu yao, juu ya matukio hayo yaliyoteka hisia za watu
wengi baada ya kutokea huku kukiwa na ukimya mrefu wa jeshi hilo juu ya kile
kinachoendelea.
“Mimi ninakualika katika mkutano wangu na waandishi wa habari
utakaofanyika kesho (leo) hapo nitazungumza kila kitu likiwemo suala la Dk.
Ulimboka na hata sakata la askari kudaiwa kukimbia na milioni 150,” alisema
Kamanda Kona.
Dk. Ulimboka alitekwa Juni 26 mwaka jana na kisha kuteswa
kunyofolewa kucha na meno na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwe Pande
jijini Dar es Salaam, tukio lililokuwa likihusishwa na serikali.
Hata hivyo, kutokana na utata wa tukio hilo, Jeshi la Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam chini ya kamanda wake, Suleiman Kova, liliunda
tume ya wataalam kutoka ndani ya jeshi iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi ili
kuchunguza sakata hilo.
Hatua hiyo ilikuja kutokana na Dk. Ulimboka kuwataja baadhi ya
watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini mpaka sasa licha
ya mtu mmoja raia wa Kenya, Joshua Mulundi, kufikishwa mahakamani akituhumiwa
kuhusika na tukio hilo, watuhumiwa wengine hawajawahi kuhojiwa.
Tume hiyo hata hivyo, haikuwahi kutoa ripoti yake kama Kova
alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka hajawahi
kuhojiwa huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana na sakata hilo.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza hivi karibuni, jeshi hilo
kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso, lilikanusha kuwepo kwa tume hiyo na
kusema kuwa walioteuliwa ni polisi ambao wanafanya kazi za kiuchunguzi kwa
taratibu za jeshi hilo.
Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, aliyoitoa Juni 27
mwaka jana juu ya kuwepo kwa tume ya kufuatilia sakata hilo ambapo alimteua
Kamishna Msaidizi wa Polisi Ahmed Msangi kuongoza tume hiyo.
Msemaji wa magereza ashambuliwa
Katika hatua nyingine, msemaji wa jeshi la magereza nchini, Omari
Mtiga, ameshambuliwa vikali kwa kauli yake ya vitisho dhidi ya mwandishi wa
habari wa gazeti hili aliyekuwa akifuatilia suala la mtuhumiwa Joshua Mulundi.
Mwandishi mkongwe nchini, Salim Saidi Salim,
Akizungumza na
Tanzania Daima jana, alisema kuwa kauli ya Mtiga ni ishara ya ulevi wa madaraka
walionao baadhi ya watendaji wa serikali, na akataka achukuliwe hatua za
kinidhamu na jeshi hilo.
Juzi akihojiwa na Tanzania Daima, msemaji huyo aling’aka na
kumtishia mwandishi kumkamata na kumweka ndani kwa madai kuwa suala la magereza
ni nyeti na halipaswi kujadiliwa nje ya utaratibu.
“Huyu ofisa anapaswa kuelewa kuwa jeshi la magereza siyo familia
yake na Watanzania wanapaswa kuelewa mambo yanayoendelea kupitia kwa waandishi
wa habari.
“Hivi kwangu ni vitisho na ninyi waandishi mnapaswa muandike
barua Baraza la Habari Tanzania (MCT) ili waweze kumkemea huyu aliyeshindwa
kutambua wajibu wake na kuishia kutishia wenye kuwajibika,” aliongeza Salim
Salim.
Salim, amewahadharisha waandishi wa habari nchini kuchukua
tahadhari ya hali ya juu katika kazi zao kwa madai kuwa kile alichoeleza kuwa
maisha ya waandishi kwa sasa yapo hatarini kutokana na watenda maovu kutotaka
kuumbuliwa kwa maovu yao.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Freemedia
inayochapisha gazeti hili pamoja na Sayari, Salim Salim alisema kwa sasa
watenda maovu ndani ya nchi wamekuwa wakijihami kwa kila namna ikiwwemo hata
kuwaua wale wanaowaona ni vikwazo katika kutekeleza uovu wao.
Alisema kuwa waandishi wanaoandika habari zenye kuwagusa watu
hao wahakikishe majina yao hayajitokezi katika vyombo vya habari
wanavyovitumikia juu ya habari za hatari walizoandika kwa ajili ya kujiweka
salama na kujitenga na wahalifu hao.
Akizungumzia kifo cha mwandishi wa habari wa Redio Kwizera
kilichotokea hivi karibuni mkoani Kigoma Salim Salim, alisema kuna haja ya
waliohusika kuchukuliwa hatua kali zaidi.
“Mnaandika habari za watu ambao hawapendi mambo yao yajulikane,
fikirieni mnapowaandika wakwepa kodi na waingiza madawa ya kulevya hawa tayari
wameshaamua kuua wananchi kwa njia hiyo na wakiona wewe ndiye kikwazo kwao
sidhani kama watakuacha ukiwa hai,” alisema Salim Salim.
CHANZOhttp://www.freemedia.co.tztp://www.freemedia.co.tzp://www.freemedia.co.tz
cha
CHAcc
0 comments:
Post a Comment