KATUNI ZA MCHORAJI, MASOUD KINYA ZINAZOPATIKANA KATIKA GAZETI LA MWANANCHI.
SAKATA
la maandamano yaliyofanywa na wananchi wa mikoa ya kusini kupinga mradi wa
gesi, limekivuruga vibaya Chama cha Mapinduzi.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya serikali na chama hicho,
zimesema kuwa umezuka msuguano mkali miongoni mwa viongozi wa serikali,
kuhusiana na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa hivi karibuni kupinga maoni ya
wananchi wa mikoa hiyo kuhusiana na sakata hilo.
Wakati Rais Kikwete, Waziri wa Nishati na Madini Profesa
Sospeter Muhongo na viongozi wengi wa CCM wakiwashutumu vikali wananchi
walioandamana wakipinga kusafirishwa kwa gesi hiyo kwenda Dar es Salaam,
taarifa zimebainisha kuwa mawaziri wengine wakisaidiwa na wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya chama hicho, wamemgeuka mwenyekiti wao wakitaka maoni ya
wana Mtwara yasikilizwe.
Chanzo chetu cha habari cha kuaminika ndani ya CCM, kimeiambia
Tanzania Daima kwamba juzi mawaziri watatu (majina yanahifadhiwa),
walikubaliana kwa dhati kulifikisha jambo hilo mbele ya vikao halali kufuta
kauli ya Rais Kikwete na Profesa Muhongo, badala yake waangalie namna ya
kutekeleza maoni ya wananchi hao.
“Kuna mvutano mkubwa mno. Hawa mawaziri wamekataa kabisa
kukubaliana na hoja za Rais na waziri wake wa nishati na wanataka jambo hili
litazamwe kwa uangalifu kwa sababu lina madhara makubwa kwa uhai wa serikali,”
kimesema chanzo hicho.
Aidha chanzo hicho kimedai, mbali na mawaziri hao, wabunge wengi
wa CCM tayari wametofautiana na kauli ya Kikwete na viongozi wengine wa CCM,
wakisema kuwa hawakubaliana na mtindo wa serikali wa kupuuza mawazo ya
wananchi, na kibaya zaidi wakisukuma lawama kwa viongozi wa vyama vya upinzani
kwa madai yasiyokuwa na msingi.
“Unajua kama hatutaacha kusukuma lawama kwa wapinzani kwa kila
jambo, bila kutambua kuwa hata wao ni Watanzania na wanayo haki ya kukataa
jambo lolote wanaloona halina manufaa kwao, tutakuwa tunajichimbia kaburi na
kupoteza heshima bure,” kilisisitiza chanzo hicho.
Hata hivyo, kuna habari kwamba tayari Rais Kikwete amefikishiwa
ujumbe akiombwa kufuta kauli yake, na kukubali kukaa meza moja na wazee wa
mikoa ya Mtwara na Lindi kujadiliana namna njema ya kutekeleza mradi huo kwa
manufaa ya Watanzania wote.
“Mzee wamempelekea taarifa mbaya na zisizo na ukweli. Hawa
Watanzania wenzetu, hawajakataa mradi huu, bali wanachosema wao, mtambo ujengwe
Mtwara kwenyewe, na umeme usambazwe kutoka hapo, ili nao wanufaike na mradi huo
wa umeme badala ya gesi hiyo kusafirishwa hadi Dar es Salaam,” kilifafanua
zaidi chanzo hicho.
Wakati msuguano huo ukiendelea, wiki hii Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Mtwara Mohamed Sinan amesema wanapongeza msimamo wa Kikwete alioutoa wakati
wa kutoa hotuba ya mwisho wa mwaka, wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia
toka Mtwara hadi Dar es Salaam.”
Msimamo huo wa Rais Kikwete, ulirudiwa kwa namna isiyovutia na
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, alipokutana na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam.
Waziri Muhongo, aliwakejeli wakazi wa mikoa hiyo akisema
hawakuwa na sababu ya kuandamana kutaka gesi asilia iwanufaishe kwa kuwa mikoa
hiyo haina uchumi utakaoweza kutumia gesi hiyo.
Prof. Muhongo pia aliwakejeli wanasiasa waliounga mkono
maandamano ya wakazi hao, akiwemo mbunge wao wa Mtwara Mjini, akisema kuwa
wanapaswa wajue kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara haina gesi inayomiliki.
“Hiyo gesi inayowafanya wanasiasa wawashawishi wakazi wa Mtwara
kuandamana haiko Mtwara wala Lindi, bali iko katika mipaka ya Tanzania ndani ya
kina kirefu cha bahari na kwa hilo kila Mtanzania ana haki ya kutumia,” alisema
na kuwashambulia wabunge wa maeneo hayo, akisema kuwa walikuwa wamepelekwa
semina nje ya nchi kwa ajili ya masuala ya gesi na wamelipwa posho hivyo
aliwashangaa kwa msimamo huo.
Wananchi wa Mtwara waliandamana Desemba 27, 2012, kupinga
kusafirishwa kwa gesi asilia kupelekwa Dar es Salaam, msimamo ambao pia
uliungwa mkono na Mbunge wa Mtwara Mjini kupitia chama hicho Husnain Murji.
Akijibu kuhusu msimamo wa Prof. Muhongo alisema: “Kwanza
namshukuru waziri kwa kunipeleka kujifunza Trinidad na Tobago, nilichojifunza
ni kwamba wenzetu wa huko wana uzoefu wa miaka 100, na wanawajali watu wa eneo
husika ambako rasilimali inatoka tofauti na sisi tunavyotaka kuwafanyia wakazi
wa Mtwara,” alisema.
Aliongeza kuwa wananchi wa Mtwara ni lazima wajue watanufaika
vipi na rasilimali ya gesi kwa kile alichoeleza kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, alipofika mkoani humo katika ziara ya
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwaambia hawana chao katika mrahaba
mzima wa gesi.
Murji aliongeza kuwa kazi ya mbunge ni kusikiliza mawazo ya
wananchi na alichoeleza ndio msimamo wa wananchi, huku akisisitiza kuwa Waziri
Muhongo amedanganya kwani wakazi wa Mtwara hawajawahi kunufaika na umeme wa kutoka
nje ya Mtwara.
Alihoji ulazima wa serikali kujenga mtambo wa gesi Kinyerezi
jijini Dar es Salaam na kuacha kuzalisha umeme huo mjini Mtwara na kisha
uunganishwe katika gridi ya taifa.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu mstaafu na mwanasiasa mkongwe nchini,
John Malecela, aliishauri serikali ifanye kila iwezalo ili wakazi wa Mtwara
wananufaika kwanza na rasilimali hiyo.
“Ukiwa karibu na waridi unatakiwa kunukia waridi.
Wakazi wa
Mtwara nao wanatakiwa wanukie waridi,” alisema Malecela na kuongeza kuwa ukweli
wakazi wa eneo inakopatikana rasiliamali hiyo wanapaswa kunufaika nayo,
haukwepeki.
“Hatutakiwi kuwaacha hivi hivi wana Mtwara eti kwa sababu hii ni
rasilimali ya Watanzania wote. Serikali iyaangalie kwa umakini maeneo yanayotoa
utajiri na rasilimali, ni lazima wapewe upendeleo ili wafurahie matunda ya mali
asili yao.
Msimamo huo ulifanana pia na wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Willibrod Slaa ambaye alililalamikia serikali kuwa inasisitiza kujenga mitambo
Kinyerezi kwa kuwa wanataka kuleta gesi hiyo Dar es Salaam ili kunufaika wao
kwanza, jambo ambalo ni la kiubaguzi.
“Wananchi wa Mtwara ni maskini, mkoa wao umetelekezwa muda
mrefu, wamekopwa korosho yao, sasa wamepata gesi na wanayo haki ya kudai
wanufaike nayo ili nao wapate viwanda, shule na hospitali nzuri.
Dk. Slaa alisema mikoa hiyo haijawahi kuwa na hospitali ya
rufaa, hivyo wanaionya serikali isiendeshe shughuli za uchumi kwa maslahi ya
watu wachache.
Alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kutokuwekeza mitambo ya gesi
Mtwara na Lindi ili isaidie ukuaji wa maeneo hayo kiuchumi na kwamba jambo hilo
wala halina siasa.
CHANZO http://www.freemedia.co.tz
0 comments:
Post a Comment