RAIS MTAAFU AWAMU YA TATU ALHAJ ALLY HASSAN MWINYI.
MTUHUMIWA
anayedaiwa kumuibia rais mstaafu Ally Hassan Mwinyi sh.milioni 37, Abdallah
Nassor Mzombe (40) zikiwa ni kodi ya pango katika nyumba mbili zinazomilikiwa
na rais huyo, ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa
anajua siri nyingi za Mwinyi ambazo kamwe hawezi kuzisema mahakamani hapo.
Mbele
ya Hakimu Mkazi, Jenevitus Dudu, katika utetezi wake, mbali ya kukataa kutenda
kosa hilo, Mzombe alidai amefanya kazi nyingi na kushirikishwa na mzee Mwinyi
mambo mengi ya wazi na ya siri ambayo hata watoto wake wa kuzaa hawayajui na
kwamba anashangazwa kuona sasa anashtakiwa kwa makosa ya kumuibia fedha hizo.
Mzombe
ambaye wakati akitoa utetezi wake alikuwa akiangua kilio na kulitaja jina la
Mungu, alidai ameanza kufanya kazi za Mwinyi tangu mwaka 1996 na kwamba Mwinyi
amekuwa akimuamini.
Alidai
kuwa hakukuwa analipwa mshahara maalumu na Mwinyi kwani alimchukulia kama
mwanae.
“Mzee
Mwinyi aliniamini sana na hata mambo mengine ambayo amekuwa akituma nifanye
siwezi kuyasema hapa mahakamani, kwani hata watoto wake hakuwahi
kuwashirikisha…
hizo nyumba mbili mnazodai mimi nimemuibia fedha si kweli, kwani
Mzee Mwinyi amekuwa akinipa zaidi ya shilingi milioni 300 bila kuandikishiana
sehemu niende nikamnunulie nyumba, mashamba, nikamjengee majumba na nimekuwa
nikifanya hivyo na kuandika jina lake.
“Mwendesha
Mashtaka naomba nikuulize, unaujua uhusiano wetu na Mwinyi? usitake niseme
mengi hapa..hivi unafahamu kuwa nilishakaa na Mwinyi tukajifungia na kuongea na
kukubaliana kwamba ninavyomfanyia shughuli zake hizo kwa uaminifu tena bila
hata watoto wake hawajui ipo siku ataninunulia nyumba? lakini hadi leo nyumba
hajaninunulia,” alidai.
“Mheshimiwa
hakimu, mimi sina crown, sina fedha na hao wapangaji waliokuja kutoa ushahidi
kuwa walinipa kodi mimi sikumpelekea Mwinyi ni waongo na sijawahi kugombana nao
isipokuwa mpangaji mmoja ambaye tangu mwanzo nilimuona kama ni mkorofi.
“Kwa
kuwa Mwinyi ni kiongozi mkubwa ni wazi mashahidi hao wanaweza wakawa
walishinikizwa kuja kutoa ushahidi wa kunikandamiza, ila nasema sina madaraka,
fedha na mashahidi ambao nilikuwa nategemea waje kunitolea ushahidi wananipiga
chenga kwa sababu wapo karibu na Mzee Mwinyi….kikubwa hapa naomba mahakama
initendee haki,” alidai Mzombe huku akiangua kilio.
Kuhusu
wizi wa fedha za kodi nyumba hizo za Mikocheni na Msasani, Mzombe alidai
kushangazwa na tuhuma hizo, kwani ni rais Mwinyi ndiye aliyempa fedha za kwenda
kumnunulia nyumba hizo na alikuwa akizisimamia wakati wa kufanyiwa ukarabati.
Bada
ya kumaliza utetezi huo, Hakimu Dudu alisema hukumu ya kesi hiyo ataitoa
Februari 12 mwaka huu.
Oktoba
9 mwaka jana, rais All Hassan Mwinyi alifika mbele ya Hakimu Dudu na kutoa
ushahidi wake, lakini hata hivyo wana usalama ambao walikuwa wakimlinda
waliwazuia waandishi wa habari kuingia mahakamani kusikiliza ushahidi huo.
Katika
kesi hiyo, Mzombe anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai mwaka
2012 huko Mikocheni, akiwa Wakala wa rais huyo alimwibia sh milioni 17 ambazo
ni pato la kodi ya nyumba yake iliyopo eneo la Mikocheni.
Aidha,
alidai kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 10, mwaka huu huko
Msasani Village, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alimwibia rais huyo sh. milioni
19.8 ambayo ilikuwa ni kodi ya nyumba namba 55 iliyopo kwenye Kitalu C.
CHANZO http://www.freemedia.co.tz
0 comments:
Post a Comment