BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NAMNA YA KUDHIBITI UGONJWA WA MALARIA.

 
HUYU ndiye Mbu anayeambukiza ugonjwa wa malaria na moja ya dalili ya ugonjwa huo nikuuma kichwa na kupatwa na homa kali.Mgonjwa wa akichukuwa damu kwa ajili ya kupima ili kuweza kuona wadudu wanaosababisha Malaria katika chumba cha maabara.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimpa pole mtoto Brenda Boniface (4) wakati akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria hivi karibuni katika Hospitali ya shirika la Elimu Kibaha kulazwa, kulia ni mama wa mtoto huyo Bi.Tiasaeli Palangyo.
JAMII inatakiwa kuelimishwa na kutambua umuhimu wa kuzingatia kinga dhidi ya ugonjwa wa malaria unaoongoza kusababisha vifo vingi nchini na matumizi ya dawa kikamilifu kwa wagonjwa ili kupunguza vifo, hasa kwa akina mama na watoto wenye umri chini ya miaka, Makala hii ya Mwandishi, HELEN MWANGO yafafanua.

“ Sikufikiri kama ningeweza kutaabika hivi, wiki ya tatu sasa, siwezi kula vizuri na huwa najisikia hovyohovyo. 

Nilikwenda hospitali nikaambiwa nina vijidudu vya ugonjwa wa Malaria. 

Sikuamini kabisa, maana kila siku lazima nishushe neti kabla ya kulala. 

Nilichogundua ni tabia yangu ya kulala nikiwa mwili wangu nimegusa chandarua husababisha mbu kuniuma sana,” anasema Juma Bahati, mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Bahati ni mmoja kati ya watu wengi nchini wanaosumbuliwa na ugonjwa wa malaria kwa utaratibu wa kulala wakiwa wameegemea chandarua na kusababisha mbu wawanyonye damu na kuwaachia vidudu vinavyosababisha ugonjwa wa malaria.

Nchini Tanzania, inakadiriwa kuwa kati ya watu milioni 16 hadi 18 huugua malaria kila mwaka na kati yao watu 100,000 hufa.

Asilimia sabini ya vifo hivyo ni watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Malaria inachangia asilimia 30 ya mzigo wa magonjwa kitaifa,asilimia 43 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaohuduhuria kwenye vituo vya huduma ya afya, asilimia 35 ya watoto wa umri chini ya miaka mitano wamnaolazwa vituoni, asilimia 37 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wanakufa vituoni.

Malaria ni chanzo kikubwa cha upungufu mkubwa wa damu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii , Dk. Donan Mmbando, akizungumza hivi karibuni alisema kwamba, mambukizi ya ugonjwa huo husababisha takriban vifo vya watu 100,000 kwa mwaka sawa na kifo cha mtu mmoja kila baada ya dakika tano.

Dk Mbando anasema serikali inafanya jitihada za kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutoka vifo 154 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai (kwa utafiti wa mwaka 2002) hadi 79 mwaka 2010.

Miongoni mwa mikakati ya kufanikisha azma hiyo ni kushirikisha vyombo vya habari kuhamasisha jamii namna ya kujikinga na ugonjwa huo, kwa kutumia vyandarua vyenye dawa ya kinga na kutibu kwa dawa za mseto ili kuutokomeza ugonjwa huo.

Aidha katika harakati za kutokomeza ugonjwa huo, serikali imejiwekea malengo katika Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA), kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaolazwa hospitalini kutokana na ugonjwa huo kutoka asilimia 12 iliyokuwepo mwaka 2005 hadi asilimia nane ifikapo mwaka 2010. 

Katika ngazi ya kimataifa, Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa yameweka msisitizo katika kupunguza kuenea kwa malaria. 

Lengo la sita, shabaha ya nne ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia inasisitiza kutokomeza kuenea kwa malaria na magonjwa mengine kama kifua kikuu. 

“Serikali inafanya kila juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kutosha za kinga na tiba zinawafikia wananchi wote nchini. Njia mbili za kupambana na malaria ni tiba na kinga. 

Kinga ni bora kuliko tiba. 
Matumizi ya dawa ya kuuliwa wadudu ya DDT ili kuteketeza mazalia ya mbu husaidia kupatwa na ugonjwa huo.

Njia madhubuti ya kupambana na malaria ni kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa huo,” alifafanua na kuendelea. 

“ Hadi sasa dunia haijaweza kupata chanjo ya malaria.

Hatuna budi kutumia njia mbadala za kinga. Moja ya njia hizo ni kutumia vyandarua, hasa vyandarua vyenye dawa ya kuua mbu ( vyandarua vyenye viuatilifu),” alisema. 

Njia nyingine ni unyunyizaji wa dawa kwenye maeneo ya mazalia ya mbu, na kuta za nyumba. Ili kusaidia kujilinda na malaria na kusafisha mazingira kama mifereji, kufukia mabaki ya chupa na madimbwi. 

Kwa akina mama wajawazito, alisema Wizara inasisitiza kuwa, wapatiwe dozi za SP ili kujikinga na ugonjwa wa malaria mara mbili kabla hawajajifungua.

Dawa hizo kwa wajawazito zinamlinda mama na mtoto aliyeko tumboni, ili asipate ugonjwa wa malaria kutoka kwa mama yake. Njia hiyo ikitekelezwa kwa usahihi, itapunguza vifo kwa akina mama wajawazito.

Ugonjwa wa malaria ni mzigo mkubwa kwa taifa . Kila mwaka, malaria inatumia dola za kimarekani 121 milioni, ambazo ni sawa na pato la taifa 3.4, hivyo kurudisha nyuma jitihada za kupigana na umaskini nchini. 

Alisema katika hali hiyo, vyombo vya habari ni wadau wakubwa watakaosaidia kuwaelimisha wananchi njia sahihi za kupambana na ugonjwa huu, ili kuwafundisha jinsi ya kutambua dalili za ugonjwa wa malaria, jinsi ya kujikinga na iwapo wataugua, kufahamu umuhimu wa kuwahi matibabu mapema na kutumia dawa kwa usahihi kama wanavyoelekezwa na wataalamu. 

Naye Meneja wa Kinga wa Wizara hiyo, Dk. Alex Mwita alisema kuwa, ugonjwa wa malaria ni mzigo mkubwa kwa Taifa na kwamba kila mwaka, malaria inatumia dola za Kimarekani milioni 121, ambazo ni sawa na pato la taifa 3.4, hivyo kurudisha nyuma jitihada za kupigana na umaskini nchini. 

Aidha, gharama hizo zinazoonekana moja kwa moja zinajumuisha binafsi na zile za kitaifa kwenye masuala ya kinga na tiba kwa ujumla.

Gharama binafsi ni kama vile vyandarua vyenye viatilifu, mahudhurio ya hospitali, dawa, usafiri na matunzo ya mgonjwa , iwapo atalazwa ambapo gharama za kitaifa ni pamoja na matumizi makubwa ya serikali katika ununuzi wa dawa na vifaa vya tiba, matengenezo ya vituo vya kutoa huduma ya afya, miundombinu, udhibiti wa mazalia ya mbu pamoja na utoaji elimu kwa umma na utafiti.

Pia, kuna gharama ambazo hazionekani moja kwa moja zinatokana na kupoteza au kudhoofu kwa nguvukazi kutokana na kuugua na pengine vifo, kutokuhudhuria kazini au shuleni, kuathiri maendeleo na ukuaji kwa watoto.

Hata hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo, wataalamu wa masuala ya sera za afya wakiongozwa na Shirika la Afya Duniani wanafanya juhudi za kuongeza upatikanaji wa dawa mseto kuwa na unafuu zaidi.

Dk. Mwita anasema, serikali inafanya juhudi mbalimbali kupitia vyanzo vya ndani na nje ya nchi ili kuchangia upatikanaji wa dawa mseto zinazotibu malaria kwa sasa.

Katiika jitihada za kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa huo, wananchi wanatakiwa kutumia dawa hizo kikamilifu kwa kuzingatia ushauri wanaopewa na madaktari au katika vituo vya afya nchini. 
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: