RAIS Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amemfukuza kazi Waziri
wa Ulinzi nchini humo pamoja na Mkuu wa majeshi kutokana na kushindwa
kuwadhibiti waasi wa Seleka.
Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Waziri wa ulinzi aliyefukuzwa kazi ni mtoto wa kiume wa rais Bozize
anayeitwa Jean Francis Bozize. Hatua hiyo inachukuliwa wakati waasi wa kundi la Seleka wakiwa wametangaza kusitisha harakati zao za kuelekea Bangui.
Kutokana na kuendelea kwa mzozo nchini humo Umoja wa Mataifa umetoa mwito kwa pande zote mbili kukaa katika meza ya majadiliano na kutafuta suluhu ya matatizo yao ukisema kuwa uko tayari kuyaratibu mazungumzo hayo.
Msemaji wa umoja huo, Martin Nesirky, ameliambia shirikia la habari la AFP kuwa wanaendelea kufuatilia hali ya mambo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa umakini mkubwa.
Juhudi za Umoja wa Mataifa
Naye Balozi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Margaret Vogt, yuko karibu na pande zote mbili katika taifa hilo pamoja na washirika kutoka nchi za eneo zima la Afrika ya Kati ili kuhakikisha kwamba yanafanyika majadiliano ya amani.
Rais Denis Sassou-Nguesso wa Jamhuri ya Kongo
Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, mazungumzo ya amani yamepangwa
kufanyika tarehe 8 Januari kwenye mji mkuu wa Gabon, Libreville, na
yataratibiwa na Rais wa Jamhuri ya Kongo Brazaville, Denis Sassou
Nguesso. Sassou Nguesso ndiye aliyeteuliwa kuwa kiongozi wa majadiliano ya amani katika nchi za eneo la Afrika ya Kati.
Wawakilishi wa serikali na upande wa waasi wote wamesema kuwa wamekubali kushiriki mazungumzo hayo ingawa hawajathibitisha kukubali tarehe hiyo iliyopangwa.
Waasi wakubali mazungumzo
Rais Francois Bozize na wanajeshi wake
Katika kipindi cha wiki tatu waasi wa muungano wa Seleka wameweza
kuiteka miji muhimu nchini humo na sasa wako karibu na mji mkuu wa
Bangui wakitishia kuutwaa wakati wowote. Waasi hao wanamtuhumu Bozize kwa kushindwa kutimiza makubaliano ya amani ya mwaka 2007.
Hapo jana waasi hao walitangaza kusitisha mashambulio yao kuelekea mji mkuu Bangui na kutuma ujumbe katika mazungumzo yanayosimamiwa na jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Afrika kati, mjini Libreville nchini Gabon.
Msemaji wa waasi, Eric Massi, alisema kwa njia ya simu kutoka Paris, Ufaransa amewataka wanajeshi wao wasisonge mbele kutoka mahala waliko hivi sasa kwa sababu wanataka kushiriki katika mazungumzo ya Libreville ili kusaka ufumbuzi wa kisiasa.
0 comments:
Post a Comment