KWA UFUPI
RAIA WA KIGENI ATAKA KUMSHTAKI KWA TUHUMA ALIZOZITOA BUNGENI, YEYE AKIMBILIA KWA KATIBU WA BUNGE.
MBUNGE KIGOMA ZITTO KABWE
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe ameingia matatani, baada ya kutakiwa kukanusha tuhuma alizozitoa bungeni
katika Mkutano wa Tisa wa Bunge, kwamba mfanyabiashara wa kigeni, Moto Mabanga,
alipewa vitalu vya mafuta kinyume na taratibu.
Mfanyabiashara huyo amesema kuwa
iwapo Zitto atashindwa kukanusha tuhuma hizo, atafikishwa mahakamani.
Barua iliyoandikwa kwenda kwa mbunge
huyo iliyosainiwa na Mwanasheria wa Mabanga, Lawley Shein wa Kampuni ya Uwakili
ya Lawley Shein Attorneys, ambayo Mwananchi Jumapili limeiona, inaeleza kuwa
hoja binafsi aliyoitoa Zitto, haikuwa na ukweli wowote.
Barua hiyo ya tarehe 28 Novemba,
2012 ilisema kuwa hoja hiyo ya Zitto ni ya uongo, imemkashifu mteja wao na
kumshushia hadhi yake binafsi na biashara zake.
“Katika kuthibitisha kuwa tuhuma
zako siyo za kweli katika hoja uliyotoa, umemtaja mteja wetu kama raia wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mteja wetu ni raia wa Afrika Kusini, lakini,
umeamua kumtaja kama raia wa Kongo bila kuangalia ukweli,” alisema Shein.
Katika barua hiyo, Shein pia amesema
kuwa Zitto amemtuhumu mteja wake Mabanga kuwa aliwahonga baadhi ya vigogo
serikalini na kuwapa rushwa wanasiasa katika mchakato wa kufanikisha
upatikanaji wa vitalu hivyo.
“Tuhuma hizo siyo za kweli, mteja
wetu alifuata taratibu zote kwa uwazi na mamlaka husika nchini na hakuwahi
kutoa rushwa kwa mtu yeyote,” alisema mwanasheria huyo.
“Tuhuma hizi ni za uongo,
zimemharibia jina mteja wetu na kumsababishia madhara. Kama hutazifuta kauli
hizo, uongo huo utamsababishia mteja wetu madhara makubwa zaidi na tutalazimika
kudai fidia,” Shein alionya kupitia barua hiyo.
Shein aliongeza kuwa pamoja na Zitto
kuongea hoja hiyo akiwa bungeni hivyo kuwa na kinga ya kibunge, lakini kwa
mazingira aliyotolea hoja hiyo alitumia vibaya kinga ya kibunge, anayopata
mbunge yeyote anapotoa hoja akiwa bungeni.
Kupitia barua hiyo, Shein alimtaka
Zitto kufuta kauli yake dhidi ya mteja wao na kwamba mteja wao ana haki zote za
kushtaki dhidi ya hoja hiyo.
Zitto azungumza.
Alipotakiwa kuzungumzia hoja hiyo na hatua atakazochukua, Zitto alisema kuwa amemwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, kumjulisha hatua hiyo ya kutaka kushtakiwa.
Alipotakiwa kuzungumzia hoja hiyo na hatua atakazochukua, Zitto alisema kuwa amemwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, kumjulisha hatua hiyo ya kutaka kushtakiwa.
“Nimemwandikia Katibu wa Bunge kumjulisha kwamba nimeletewa kusudio la kushtakiwa, maana hili ni suala la Kinga ya Bunge,” alisema Zitto na kuongeza:
“Mbunge ana kinga kwa masuala
aliyozungumza ndani ya Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba. Kwa hiyo
Katibu (Dk Kashililah), atawajibu hao wanasheria.”
0 comments:
Post a Comment