BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DK KIKWETE AWAPA POLISI MENO KUDHIBITI MAANDAMANO

Kwa ufupi:
“Wajibu wenu umetajwa kisheria, mamlaka yenu mlikabidhiwa na Bunge na wanapopiga kelele kuwa mmetumia nguvu kubwa, waambie sheria mmezitunga ninyi kwa hiyo nendeni mkazibadilishe,”
 
RAIS Jakaya Kikwete amewapa meno polisi kudhibiti maandamano, ambayo yamekuwa yakitokea na kusababisha uvunjifu wa amani sehemu mbalimbali nchini.
Alitoa kauli hiyo kutokana na siku za karibuni taifa kughubikwa na maandamano sehemu mbalimbali, huku  mengine yakisababisha uharibifu wa mali hata baadhi ya watu kupoteza maisha.

Mathalan, maandamano ya gesi ya Mtwara yaliyotokea hivi karibuni. Pia, mwaka jana wafuasi wa dini ya Kiislamu Dar es Salaam na Zanzibar waliandamana.

Pia, maandamano yaliyoandaliwa na Chadema yalisababisha watu kupoteza maisha baada ya kuuawa na polisi Mikoa ya Morogoro na Iringa.  
Akifungua mkutano wa maofisa waandamizi wa polisi Dodoma juzi jioni, Rais Kikwete alisema  maandamano na mikutano ya hadhara ni haki ya kila mtu, lakini  baadhi ya watu wamekuwa wakiwatia majaribuni polisi kwa kukaidi amri halali. 

“Hivi karibuni suala la maandamano limechukua sura mpya na kuonekana kama la kawaida, wakati yanasababisha uvunjifu wa amani na kuwafanya Watanzania waendelee kuzoea hali ya machafuko,” alisema.
Aliwaagiza polisi kutimiza wajibu wao kuhakikisha wanadhibiti vurugu zote bila ya kusikiliza maneno ya wanasiasa na watu wengine, ambao wanalaumu bila  kujua kazi nzuri inayofanywa na askari.
“Wajibu wenu umetajwa kisheria, mamlaka yenu mlikabidhiwa na Bunge na wanapopiga kelele kuwa mmetumia nguvu kubwa, waambie sheria mmezitunga ninyi kwa hiyo nendeni mkazibadilishe,” alisema Rais Kikwete.

Pia, Rais Kikwete alishangazwa na  kauli za watu kuwa, polisi wanatumia nguvu kubwa kupita kiasi, lakini hajajua tafsiri hiyo inacholenga.

Aliwaagiza polisi kufanya kazi kwa uweledi na kujituma zaidi kulingana na mafunzo waliyoyapata kutoka vyuoni, ikiwamo  kutafuta jinsi bora ya kuzuia machafuko hata kabla ya kutokea.

Akitaja baadhi ya vyanzo vya vurugu hizo, alisema ni kutokana na baadhi ya wanasiasa kushindwa kutii maagizo ya polisi hata pale wanapozuiwa kufanya mikutano.

Awali, Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema alisema wanaendelea  kuratibu na kusimamia mikakati  kuhakikisha wanakuwa wa kisasa zaidi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: