BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

"HOJA YA WATU WA MTWARA KUHUSU GESI NI UPUUZI"


Nyumba ikiteketea kwa moto baada ya wananchi kuchoma moto wakati wa vurugu zilizohusu kupinga gesi asilia ya Msimbati kwenda jijini Dar es Salaam hivi karibuni mkoani Mtwara.
 
BARAZA la Habari la Kiislamu Tanzania (BAHAKITA), limesema hoja ya watu wa Mtwara kutaka gesi iwanufaishe wao kwanza ni upuuzi, kwa kuwa hoja hiyo itajenga ukanda katika Tanzania isiyoamini mgawanyiko wa kikabila.


Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa BAHAKITA, Shekhe Said Mwaipopo.

Alisema kitendo cha watu wa Mtwara na wengine kutoka nje ya Mtwara, kusema gesi hiyo ni yao ni kitendo cha kukosa busara.

“Tukianza kugawana mafungu si kitu kizuri. Leo hii watu wa Mwanza wanasema maji yao yasiende Shinyanga hadi wao wayatumie, Wazaramo nao waseme watu wote ambao si wa Dar es Salaam watoke, si hoja ni upuuzi na kauli za kichochezi,” alisema Mwaipopo.

Aidha, aliwaonywa baadhi ya wanasiasa na viongozi wa dini wanaotoa kauli za kichochezi na kusema watu hao wamefilisika kisiasa.

“Hawa viongozi wa kisiasa hususani wa Chadema wamefilisika kisiasa, ni wanasiasa uchwara na mbaya zaidi wenyewe wamekiri kupitia Katibu wao Mkuu Dk. Wilbroad Slaa kuwa vitendo vinavyofanywa na watu wa Mtwara ni matokeo ya M4C.

“Lakini cha kushangaza ndani ya CCM pia wapo viongozi wakubwa akiwamo Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnein Murji ambaye alitoa kauli hadharani za kuchochea vurugu za watu wa Mtwara kwa kuwaunga mkono kuwa gesi ni ya kwao.

“Kuchoma moto nyumba si busara, mali zimeharibiwa, kwa mambo haya tunaliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wale wote ambao wamehusika katika zile vurugu na uharibifu wa mali, ile gesi ya Watanzania wote,” alisema Mwaipopo.

Kwa upande wake, Katibu wa BAHAKITA, Chifu Hussein Msopa, alisema vyama vya siasa viache kutumia gesi ya Mtwara kama chanzo cha uvunjifu wa amani.

“Tunaomba ndugu zetu wa Mtwara wawe na subira katika kipindi hiki ambacho Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amekwenda kuzungumza nao.

“Tunalaani vurugu zote ikiwamo uchomaji nyumba na uharibifu wa mali, tunaomba Jeshi la Polisi liwachukulie hatua wote waliohusika.

“Tunawaomba wanasiasa, viongozi wenzetu wa dini na asasi zisizo za kiserikali, kuacha kufanya jambo hili mtaji, iwe viongozi wa Kikristo na wale wa Kiislamu, waache kuchochea jambo hili, tuache kupandikiza chuki kwa kuwa suala hili likiachiwa litaibua hoja ya ukanda,” alisema Shekhe Msopa.
CHANZO http://www.mtanzania.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: