AMTAKA ASITUMIE MALI ZA SERIKALI KWA KAZI ZA CCM.
ZITTO KABWE.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuacha kutumia mali za serikali kwa ajili ya kufanya shughuli za Chama chake cha Mapinduzi (CCM).
Angalizo hilo la Zitto limekuja wakati Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, akitarajiwa kuwasili mkoani Kigoma wakati wowote kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya miaka 36 ya chama hicho.
Rais pia atatumia nafasi hiyo kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali kuu na halmashauri.
Akihutubia mkutano wa hadhara jana mjini hapa, Zitto alimtaka Rais Kikwete kama anakuja kwenye shughuli za CCM aje kwa gharama za chama chake na si kwa gharama za serikali.
“Rais anakuja kwenye shughuli za CCM, ndege atakayopanda ni ya serikali. Tunasema kama unakuja kwenye shughuli za CCM njoo kwa gharama za CCM,” alisema.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, aliongeza kuwa Rais Kikwete asichanganye kazi za CCM na kazi za serikali na kuongeza kuwa hana kinyongo naye kwa kuwa vitu alivyofanya mkoa wa Kigoma vinaonekana kulinganisha na marais waliotangulia.
“Sisi hatuna kinyongo naye, maanake Nyerere alipita hakuna kitu, Mwinyi amepita hamna kitu, Mkapa alipita hamna, yeye kaja kuna vitu tumeviona, hatuna kinyongo naye lakini asije kwa gharama za serikali kwa mambo ya CCM, asichanganye kwa kuwa si utawala bora.
“Haiwezekani miradi ya maendeleo ya halmashauri kama ile stendi ya mabasi ya daladala ya kituo cha stesheni, ni mradi wa halmashauri, Rais anakuja kuzindua hatukatai lakini kama anakuja kwa shughuli za CCM amalize mambo yao kwanza arudi Dar es Salaam halafu aje kiserikali atufungulie miradi,” alisema.
Aliwataka madiwani wa CHADEMA kutotoa ushirikiano kama Rais anakuja kwa shughuli za CCM kufungua miradi ya maendeleo kwa sababu itakuwa ni propaganda ya CCM.
“Hatuwezi kuruhusu mkuu wa nchi kutumia fedha za nchi kufanya kazi ya CCM na usalama wa taifa mlioko hapa mpeleke taarifa,” aling’aka.
Katika hatua nyingine Zitto pia amemtaka mkuu wa mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali mstaafu Issa Mchibya asiende kukagua miradi ya maendeleo akiwa na katibu wa CCM kwa gari la serikali na kwamba kuanzia leo wataanza kufanya ufuatiliaji.
0 comments:
Post a Comment