BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KESI YA SHEKHE ISSA PONDA BALAA TUPU.

ULINZI MKALI WA FFU, POLISI, MBWA WATANDA KILA KONA KESI YA SHEKHE ISSA PONDA.
 
 Sheikh Ponda Issa Ponda.



ULINZI unaowekwa wakati wa kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, na wenzake 49, umevunja rekodi.

Ponda na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya sh milioni 59, jana walipanda tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu tuhuma zinazowakabili.

Ulinzi uliimarishwa kuanzia majira ya saa 12 asubuhi ambapo askari waliokuwa na silaha, mbwa na vifaa vingine vya kubaini silaha, walitanda kila kona ya mahakama hiyo.

Askari waliohusika kusimamia ulinzi huo ni pamoja na wale wa kikosi cha kutuliza ghasia na wa idara ya usalama. 

Pia kulikuwa na askari waliovaa nguo za kiraia na wengine wenye sare, wakiwa na silaha nzito yakiwemo mabomu ya machozi, mbwa maalumu 12 wa polisi, wakiwa wamezingira ndani na nje ya mahakama hiyo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.

Kuimarishwa kwa ulinzi huo kulielezwa kutokana na taarifa za kiintelijensia za kipolisi kwamba baadhi ya wafuasi wa Sheikh Ponda, walipanga kufanya fujo mahakamani hapo.

Ponda ambaye aliingia katika eneo hilo akitokea katika gereza la Segerea, alisindikizwa na msafara wa magari ya maji ya kuwasha na magari mengine ya magereza na kuingizwa moja kwa moja hadi katika chumba cha mahabusu ya mahakama hiyo.

Baada ya kuingia katika mahabusu hiyo, askari waliokuwa wamesimama getini, walianza kuwazuia ndugu na wafuasi wa Ponda ambao baadhi yao walitaka kutumia nguvu kuingia kushuhudia kesi hiyo inayogusa hisia za wengi, inavyoendeshwa.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya wafuasi wakitumia nguvu kusukumana na polisi kutaka kuingia ndani, huku mbwa maalumu wakitumika kuwatisha wafuasi hao.

Siku za nyuma polisi waliruhusu watu wachache kuingia mahakamani, lakini jana walizuiliwa kabisa kuingia.

Baadhi ya maofisa usalama waliliambia gazeti hili kuwa utaratibu wa kuwazuia wafuasi wa Ponda, ulianza kutumika jana na utaendelea kila kesi hiyo itakapokuja mahakamani hapo.

“Utaratibu wa kuwazuia wafuasi wa Ponda utakuwa endelevu na hatutasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayekaidi amri hiyo na leo (jana), tumewakamata watu watatu ambao walikuwa wakilamizisha kuingia ndani ya eneo hilo la mahakama bila sababu,” alisema mmoja wa maaskari waliokuwa wakilinda mahakamani hapo.

Wakati kesi hiyo inasomwa na kuahirishwa, ndani ya ukumbi huo kulikuwa na washtakiwa, wana usalama, waandishi wa habari, mawakili na hakimu tu tofauti na awali ambapo ukumbi huo hufurika.

Katika kesi hiyo jana, shahaidi wa nne, D/c-Sajenti Mkombozi Mhando, alidai kuwa katika ungamo aliloungama Ponda, alikiri kushiriki kikamilifu yeye na wenzake kuingia kwa jinai kwenye kiwanja cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya Bakwata.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, shahidi huyo alidai kuwa Ponda alikiri kushiriki kujenga msikiti wa muda katika eneo hilo na walikuwa wakisali katika eneo hilo kuanzia Oktoba 12 -17 mwaka jana, siku ambayo washtakiwa wengine waliokuwa wakilala hapo, walipokamatwa na polisi.

Hata hivyo wakili wa washtakiwa Mansoor Nassor alipinga maelezo hayo yasipokelewe kwa sababu kifungu cha 50(1)(a) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 , kinataka mtuhumiwa achukuliwe maelezo ndani ya saa nne tangu alipokamatwa na hapa maelezo ya onyo yanaonyesha Mhando alimchukua Novemba mosi mwaka jana.

Wakati huo tayari mshtakiwa huyo alishakuwa amekamatwa siku tano nyuma akiwa mahabusu na kwamba kifungu cha 50((1)b cha sheria hiyo ya makosa ya jinai kinampa haki ofisa wa polisi kuongeza masaa ya kuchukua maelezo ya mshtakiwa.

Kwa upande wake wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka, alidai kuwa kutokana na hali hiyo, sheria ipo wazi na inataka mahakama iendeshe uchunguzi na upande wa serikali uko tayari kuleta mashahidi wa tatu kuthibitisha kuwa maelezo ya onyo la Mkadamu yalichukuliwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria.

Aidha mahakama iliambiwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ametoa kibali cha kuzuia dhamana kwa mshtakiwa wa kwanza, pili na wa tatu chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, na kwamba kwa kuwa washtakiwa wanakabiliwa na makosa ya kuvuruga amani, upande wa serikali unaiomba mahakama ifunge dhamana za washtakiwa wengine 51 wa kesi hiyo hadi hali ya usalama itakapotengemaa. Kesi hiyo inaendelea tena leo.

Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: