ALIYEKUWA Waziri
Mkuu, Edward Lowassa, ameenguliwa katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la
Wadhamini la Mali za Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Baada ya kuenguliwa huko,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, ameteuliwa kuwa
Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo.
Akitangaza uteuzi
huo jana, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema uteuzi huo umezingatia
mabadiliko yanayotokeandani ya chama na wameamua kuingiza nguvu nyingi ya
vijana.
Lowassa pamoja na
wajumbe wengine wa Baraza hilo wamekuwa katika nafasi hizo kwa kipindi cha
miaka 10 mfululizo.
Wajumbe wengine
walioachwa ni pamoja na Nadhir Karamagi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Uwekezaji na Uwezeshaji Dk Mary Nagu, Yusuph Ahmad Yusuph na Said Aboud.
Hata hivyo, mtu
aliye karibu na Lowassa ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema Waziri
Mkuu huyo wa zamani amemaliza muda wake wa uongozi katika Baraza hilo na si
kwamba ameenguliwa. Alisema alishika uongozi huo kwa vipindi vitatu mfululizo.
Wajumbe wapya
Shigela alitaja wajumbe wapya kuwa ni Machano Othman Saidi ambaye ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.
Wengine ni William
Lukuvi (ambaye alikuwamo katika Baraza lililopita), Profesa Anna Tibaijuka,
Janeth Mbene, Hamad Masauni na Mohamed Aboud.
Wajumbe wa Kamati
Kuu ya Utekelezaji wa Baraza hilo kutoka Tanzania Bara ni Daud Njali, Ruben
Sixtus, Seki Kasuga, Amini Mkalipa na Mariam Chaurembo. Kutoka Zanzibar ni
Shaka Shaka, Bakari Vuai, Nadra Mohamed, Viwe Hamisi na Ally Nassoro.
Akizungumzia taarifa, kwamba UVCCM ina mpasuko na kuwapo taarifa za kufukuzana,
Shigela alisema umoja huo hauna mpasuko na hakuna mjumbe aliyefukuzwa.
Alisema vikao viliendeshwa
kwa utaratibu mzuri na kama kuna watu waliamua kutangaza kuwapo mpasuko ndani
ya umoja huo, zilikuwa ni hisia binafsi.
Kuhusu madai kwamba wajumbe walijadili
hotuba ya Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamisi na kwamba hawakufurahishwa
nayo, Shigela alisema mwanzoni hakukuwa na ajenda za kujadili hotuba ya
Mwenyekiti.
“Hotuba ya
Mwenyekiti haikujadiliwa, wajumbe wa Baraza tulikuwa na ajenda zetu na hotuba
ya Mwenyekiti ilikuwa kwa ajili ya ufunguzi wa Baraza.
Kama kuna wajumbe
wanaona hotuba ya Mwenyekiti imewadhalilisha, huwezi kuzuia watu kutathimini,
waliamua kutoa hisia zao,” alisema.
Alisema huwezi
kubishana na hisia za mtu mmoja mmoja na kwa maana hiyo huwezi kuzuia watu
kuzungumza na kusisitiza kutokuwapo mtafaruku na wananchi waelewe UVCCM ni
imara na haina mgogoro wowote.
Shigela alisema
hakukuwa na mtu aliyefukuzwa kwenye mkutano huo na hata wajumbe wawili
walioteuliwa kuingia kwenye Baraza hilo, Rashid Msarika na Paul Makonda
hawakufukuzwa, bali hawakuthibitishwa.
Alifafanua, kwamba
kwa utaratibu wa UVCCM, baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza, majina yao
hupelekwa barazani kuthibitishwa, lakini walionekana kuwa hawakuwa tayari kwa
ajili hiyo.
Alisema kutokana
na hali hiyo, yatapendekezwa majina mengine mawili kwani wameonesha hawako tayari
kufanya kazi na UVCCM.
“Wajumbe hao
wawili walikuwa hawajathibitishwa, kwa hiyo huwezi kusema wameenguliwa au
wamefukuzwa,” alisema Shigela.
Shigela alisema Baraza Kuu ndilo
linalothibitisha uteuzi wa wajumbe wa Baraza, lakini wajumbe hao walisema kuwa
hawako tayari kwa hilo.
Maazimio Akitoa
maazimio ya UVCCM, Shigela alisema Baraza Kuu lilitoa maazimio kadhaa likiwamo
la mikoa na wilaya zote Tanzania Bara, kuwa na maeneo ya kilimo ili kuunga
mkono Sera ya Kilimo Kwanza.
Alisema umoja huo
una jukumu la kutathimini hali ya kisiasa na kupendekeza njia za kukabiliana na
hali hiyo na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha hali ya kisiasa inakuwa ya
amani na utulivu, ili kuwezesha utekelezaji wenye mafanikio ya Ilani ya CCM.
Maazimio mengine
ni kuongezwa kwa mitaala, likiwamo somo la ujarisiamali katika vyuo vikuu, ili
wanafunzi wanapomaliza shule, wawe na elimu itakayowawezesha kujiajiri.
Pia viongozi wa
UVCCM mikoa na wilaya, wameagizwa kusimamia mikopo ya vijana na wanawake katika
halmashauri zao, ili wapate kama inavyoelekezwa na Serikali.
Shigela alisema
Baraza hilo limeelekeza mikoa ianze jitihada za kujitegemea kwa kuanzisha
miradi mipya na pia Serikali iweke utaratibu mzuri kwa wajasiriamali wadogo
kama vile boda boda na wamachinga, kuendesha shughuli zao bila kubughudhiwa na
vyombo vya Dola.
Alisema Baraza
hilo limeelekeza jitihada za kujitegemea kiuchumi zipewe msukumo zaidi na
kamati ya utekelezaji iendelee kusimamia miradi ya zamani na mipya.
Katika
miradi hiyo, alisema Baraza Kuu limedhamiria uendelezaji wa kiwanja kilichopo
jengo la Makao Makuu, Makontena ya Darajani Zanzibar na Kiwanja cha Igoma na
Nyamagana, Mwanza.
0 comments:
Post a Comment