MWANARIADHA nyota wa Afrika kusini katika michezo ya Olimpiki na
Olimpiki ya walemavu Oscar Pistorius, ametiwa nguvuni
baada ya mpenzi wake wa kike kupigwa risasi nyumbani kwake mjini
Pretoria.
Polisi ya Afrika kusini ilijizuwia kumtaja Pistorius mwenye umri wa miaka 26 kuwa ni mtuhumiwa wa mauaji hayo, lakini imethibitisha kuwa mwanamke mmoja amekutwa amefariki katika eneo la Silver Wood mashariki ya mji huo mkuu.
Oscar Pistorius.
Luteni kanali Katlego Mogale ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa polisi ilipokea simu mapema leo asubuhi (14.02.2013) kuwa kulikuwa na mashambulio ya risasi katika nyumba anayoishi mwanariadha huyo ambaye miguu yake yote imekatwa.
Maafisa wa polisi walikuta bastola katika eneo la tukio na kumchukua mwanariadha huyo na kumuweka korokoroni.
Afisa huyo wa polisi amesema kuwa wakati polisi walipowasili walimkuta mwanariadha huyo akijaribu kumpa msichana huyo huduma ya kwanza kwa nia ya kumrejeshea uhai.
Mogale amesema Pistorius alikuwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani baadaye leo mchana.
Vyombo vya habari
Vyombo vingi vya habari nchini Afrika kusini vinaripoti kuwa mwanamke huyo aliyeuwawa alikuwa mpenzi wake Pistorius na kwamba huenda alidhania kuwa ni mwizi na kumpiga risasi, lakini polisi hawajafafanua uhusiano wa mwanamke huyo na Pistorius.
Pistorius katika michezo ya walemavu.
Kutokana na kukatwa miguu yake kuanzia magotini wakati akiwa na umri chini ya mwaka mmoja, alifanya kampeni kwa miaka kadhaa kuruhusiwa kushindana dhidi ya wanariadha ambao hawana ulemavu na hatimaye aliruhusiwa na mahakama ya juu ya michezo kushindana katika michezo mbali mbali.
Oscar Pistorius kushoto.
Alishiriki katika mbio za mita 400 na pia katika kikosi cha Afrika kusini kinachokimbia mbio za mita 400 kupokezana vijiti katika mashindano ya Olimpiki mjini London na pia alishinda tena katika mbio za mita 400 za walemavu katika michezo ya Olimpiki mjini London.
Hata hivyo alishindwa kurejesha taji lake la mbio za mita 200 kwa walemavu kwa kushindwa kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka tisa.
0 comments:
Post a Comment