BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE HAPENDI KUSUTWA.



ASEMA SERIKALI YAKE ITATEKELEZA AHADI ZOTE ILIYOBAKI,
ADAI ANATAKA AKUMBUKWE KWA MAENDELEO, AWAPIGA KIJEMBE WANAOMBEZA MAENDELEO YALIYOFIKIWA.
RAIS KIKWETE.

RAIS Jkaya Kikwete amesema hataki kusutwa kwa kutotekeleza ahadi zake baada ya kuondoka madarakani. Alisema Serikali yake ina dhamira njema ya kuwatumikia Watanzania na atahakikisha anatekeleza ahadi zote zilizoahidiwa na Serikali yake.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati wa maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete aliyasema hayo wakati kuna malalamiko katika jamii, kwamba Serikali yake, imeshindwa kutimiza ahadi nyingi ilizoahidi tangu aliposhika madaraka mwaka 2005.

Alisema wakati akijiandaa kumalizia nafasi hiyo ya urais, ana furaha kuona Serikali yake inawatumikia Watanzania kikamilifu kwa kuwa anataka akumbukwe na Watanzania kupitia mema aliyoyafanya.

Kuhusu baadhi ya wapinzani ambao wanajisifu kwa mambo yaliyofanywa na Serikali, alisema ni wakati mwafaka kwa wana-CCM kuwaeleza wananchi ni nini kilichofanyika kwa kuwa jambo la kushangaza kuona mpinzani anasimama na kujisifu eti barabara ya lami ya Mwandiga hadi Manyovu ameijenga yeye wakati ni kazi ya CCM kupitia Serikali yake.

“Ninataka kumaliza kupindi changu cha uongozi nikiwa na furaha ya kufanya mambo mengi yaliyo mema ili hata rais ajaye, aweze kutekeleza pale nilipoishia,” alisema.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara, alisema atahakikisha barabara zote ambazo zimeahidiwa kwa Mkoa wa Kigoma zinajengwa kwa kutumia fedha za Serikali na fedha za misaada zitakapokuja zitakuta kazi imeshaanza.

Aliwahakikishia wananchi wa Kigoma kwamba anataka kuifanya Kigoma kuwa mkoa wa kiuchumi na katika hilo atahakikisha anatimiza ndoto yake ya kuifanya kuwa ya kisasa zaidi na kitovu cha uchumi.

Alisema kuwa, mtu anayesimama katika haki huwa anafanikiwa na katika hilo la maendeleo ya Kigoma anaamini atafanikiwa.

Wakati huohuo, Rais Kikwete, alionya na kusema chokochoko za kidini zinazoendelea nchini hazina mshindi.

Kutokana na hali hiyo, alisema chokochoko hizo zinatakiwa kukemewa na kila mtu wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwa wanaheshimika katika jamii.

Alisema kuna haja wazee nchini kufanya jitihada za kukutana na viongozi wa dini ili wazungumzie hali ilivyo.

“Nilipofika hapa Kigoma, nilisomewa risala na wazee wa mkoa huu na pamoja na mambo mengine, walionya juu ya suala la udini. Nami ninakiri jambo hili kwani hata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 lilijitokeza hata pale nilipoonya nilibezwa na baadhi ya watu lakini huo ndio ukweli wenyewe.

“Ninapenda kusema kwamba, jambo hili ni lazima kwa kila mmoja wetu atambue kuwa vita ya udini haina mshindi na hapa tuna mfano ulio hai kwa jirani zetu hawa wa Burundi ambao tangu Novemba 27, mwaka 1995 nilishiriki mazungumzo ya kutafuta amani huko kwao na wengi wetu tuliona namna viongozi wa dini na wanasiasa walivyochochea mauaji nchini humo.

“Ni wazi katika hili, sasa wazee wakiwamo wa misikiti na makanisa, zungumzeni na viongozi wengine ili tuepuke hali hii kwani kama tutaruhusu machafuko haya yanayoendele kati ya Waislamu na Wakristo, tunaweza kuliangamiza Taifa letu,” alisema Rais Kikwete.

Aliwaomba viongozi wa dini zote nchini kukaa na waumini wao na kuwaleza kuhusu madhara ya migogoro ya kidini kwa kuwa vita hiyo haina mshindi na hatari kwa nchi.

“Ni vema wanasiasa wenzangu ambao wanafanya kazi ya uchochezi kwa Watanzania, waache tabia hii kwani nchi ikiharibika hakuna anayeweza kukaa. Ninaamini kuwa, jambo lolote humalizwa kwa mazungumzo na si kuchochea vurugu ambazo hazina tija kwa Taifa.

“Ninasikitika sana leo hii kuona mwanasiasa anahubiri kumwaga damu wakati anashindwa hata kuchukua kiwembe ajikate badala yake anatanguliza watoto wa watu na yeye anakwenda kwenye runinga na kujifanya anatetea watu wakati yeye ndiye aliyesababisha uvunjifu wa amani,” alisema.
 CHANZO http://www.mtanzania.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: