Kwa ufupi:
Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza
Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na
Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo
uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa
sehemu ya maadhimisho hayo.
Kada wa Chadema Mkoani Dodoma, Arnold Swai akikimbizwa na wafuasi wa CCM
jana, baada ya kutokea vurugu katika eneo la Mwanga baa, Dodoma.
SHEREHE
za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana ziliingia dosari, baada ya kuibuka
vurugu kubwa kati ya wafuasi wa chama hicho na Chadema mkoani Dodoma
wakati wakigombea eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao.
Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza
Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na
Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo
uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa
sehemu ya maadhimisho hayo.
Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema
kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti
la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo
wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.
“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha
bendera hiyo kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze
kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza
kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika
vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora
Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said
Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).
Baadhi ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe
na kuwapiga wenzao wa Chadema na kusababisha tafrani kubwa katika eneo
hilo la mkutano.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah
Mambo alisema kuwa tukio hilo limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa
bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo la Mwanga Baa kulikofanyika
sherehe za chama chao (CCM).
“Kwanza wamechukua bendera yetu. Halafu
tumeshangazwa na CCM kuruhusiwa kufanya maadhimisho yao wakati kuna
agizo la Mkuu wa Mkoa na polisi kukataza mikusanyiko ya kisiasa wakati
wa Bunge.
“Kwa nini sisi (Chadema) tuzuiwe mikutano yetu
wakati wenzetu wanafanya? Huku si kutenda haki....Tulikuwa na mikutano
ya kuimarisha chama katika kata kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili,
lakini tumezuiwa na tukaheshimu mamlaka,” alisema katibu huyo.
Pia tulikuwa tufanye mkutano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini tukazuiwa na tuliheshimu amri hiyo, alisema.
Mambo alisema katika vurugu hizo wafuasi wawili wa Chadema; Idd Kizota na Anord Swai waliumizwa na kushonwa nyuzi saba usoni.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya alisema hana taarifa za majeruhi hao.
0 comments:
Post a Comment