Kwa ufupi
NI DK SALIM,NCHIMBI,MWINYI,MIGIRO NA WASSIRA.
UCHAGUZI wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanywa na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho Jumatatu wiki hii mjini Dodoma, ni kama unabadili mwelekeo wa siasa za ndani za chama hicho kikongwe nchini.
Tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani miaka
saba iliyopita na kupewa kofia ya uenyekiti wa CCM, chama hicho kimekuwa
kwenye minyukano ya siasa za visasi kiasi kwamba hakijawahi kuwa na
utulivu wa kisiasa kama ilivyo sasa, miezi michache baada ya kufanyika
mabadiliko kadhaa ya kiuongozi.
Uteuzi na baadaye uchaguzi wa wajumbe wa Kamati
Kuu umeweka kando baadhi ya vigogo wa kisiasa hasa waliokuwa wakitajwa
katika harakati za kuusaka urais katika uchaguzi wa 2015 na kuziingiza
sura mpya ambazo huenda baadhi yao wanaweza kuingia katika
kinyang’anyiro hicho.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni vigogo ambao wamekuwa
wakitajwa kupiga mbio hizo, lakini waliwekwa kando katika Kamati Kuu
ya sasa.
Pia majina ya mawaziri na wizara zao kwenye mabano
Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Dk John Magufuli
(Ujenzi), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) pamoja na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Katibu Mkuu wa
UVCCM, Martin Shigela, pia hayakuwa sehemu ya waliopendekezwa kuingia
katika CC ambacho ni chombo cha kufanya uamuzi mkubwa ndani ya CCM.
Profesa Mwandosya licha ya kuwa na matatizo ya
kiafya, amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa watu muhimu katika mustakabali wa
siasa za sasa za Tanzania wakati Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wamekuwa
wakipigiwa chapuo na umma kwamba huenda wangefaa kuwania urais kutokana
na kasi katika utendaji kwenye wizara wanazoziongoza.
Badala yake Kamati Kuu inawajumuisha makada ambao
siyo wapya, lakini ambao wanaweza kutumika kubadili sura na mwelekeo wa
siasa ndani ya CCM hasa tunapoelekea 2015, akiwamo Waziri Mkuu wa
zamani, Dk Salim Ahmed Salim.
Hatua hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kujaribu
kujipanga kwa CCM katika kuzipa sura mpya siasa za ndani ya chama hicho.
Dk Salim kama ilivyo kwa Profesa Mwandosya, alikuwa mpinzani wa Kikwete
katika kinyang’anyiro cha urais wa 2005, ambaye bado anatizamwa kuwa
mtu mwenye uwezo licha ya kwamba umri wake ni mkubwa.
Wengine ambao kuingia kwao katika Kamati Kuu ya
CCM kunaweza kuwa na maana ya kubadili siasa za urais ni pamoja na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na mwenzake kutoka Tanzania Visiwani
ambaye alipata kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.
Dk Nchimbi anarejea Kamati Kuu ambako aliingia kwa
mara ya kwanza akiwa na umri mdogo pale alipochaguliwa kuongoza Umoja
wa Vijana wa CCM (UVCCM) na kuongoza jumuiya hiyo kwa miaka kumi
mfululizo.
Kwa mujibu wa kanuni za CCM, wenyeviti wa jumuiya za chama huwa ni wajumbe wa CC kwa mujibu wa nyadhifa zao. Nchimbi amekuwa mjumbe wa CC kwa miaka 10.
Kwa mujibu wa kanuni za CCM, wenyeviti wa jumuiya za chama huwa ni wajumbe wa CC kwa mujibu wa nyadhifa zao. Nchimbi amekuwa mjumbe wa CC kwa miaka 10.
Hali kadhalika, Dk Mwinyi ni mmoja wa makada wa
CCM ambaye amekuwa ndani ya CC kwa muda mrefu, wakati Nahodha alikuwa
akiingia ndani ya kamati hiyo alipokuwa Waziri Kiongozi wa SMZ (kwa
wadhifa wake).
Nahodha, Dk Mwinyi na Dk Nchimbi kwa nyakati
tofauti wote wamepita katika wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa. Dk Mwinyi wakati alipokuwa waziri, naibu wake alikuwa Dk Nchimbi
ambaye baadaye alihamishiwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo na sasa Mambo ya Ndani.
0 comments:
Post a Comment