NI MAUAJI YA MCHUNGAJI GEITA. WAZIRI STEPHEN WASSIRA.
IGP SAIDI MWEMA.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema, wametimuliwa mkoani Geita, huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, akisulubiwa kwa masharti magumu.
Vigogo hao wa serikali walikumbwa na patashika hiyo, juzi mkoani humo walikoenda kusaka suluhu ya vurugu za kidini zilizosababisha mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachila (45) wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God.
Habari za uhakika kutoka mkoani Geita zimesema kuwa mamia ya wananchi wa Geita walitishia kufanya lolote, ikiwa Wassira na Mwema wangeonekana wakati wa mazishi ya mchungaji huyo au sehemu yoyote mkoani humo.
Taarifa za uhakika zimesema kuwa viongozi wa wilaya na mkoa huo, baada ya kubaini kuwepo na hali ya hatari kwa viongozi hao, walilazimika kubadili eneo ambalo helkopta iliyowabeba mawaziri na IGP ingetua.
Uchunguzi umebaini kuwa, chopa hiyo, awali ilitua katika eneo la Kalangalala, lakini baada ya kubainika kuwepo na hali ya hatari, ililazimika kuruka na kwenda kutua katika eneo la Magereza mjini Geita.
Mawaziri hao waliandamana na Mwema, toka Dodoma kulikokuwa kunafanyika kikao cha makamishna wa polisi, makamanda wa mikoa na Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa wakazi wengi wa mjini Geita, hususan Wakristo, walipata taarifa ya ujio wa mawaziri hao, ndipo walipoamua kuchukua hatua hizo, na kwamba wasingekuwa tayari kuonana na Wassira kwa madai kuwa alitoa tamko lililochochea zaidi chuki baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu, huku wakimshutumu IGP Mwema kwa kuzembea kuchukua hatua kulinda usalama wa watu.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Waziri Nchimbi kutumia juhudi kubwa kuwashawishi wananchi wakubali kumsikiliza kwa nia ya kupata ufumbuzi wa vurugu hizo.
Imedaiwa kwamba Nchimbi alikubaliwa kuonana na wananchi ambao walimpa masharti mazito matano aliyolazimishwa kuyakubali, kama njia ya kupata ufumbuzi.
Sharti la kwanza alilopewa, walimtaka akubali na kutamka hadharani kuwa serikali haina dini, na hivyo sio lazima kwa Waislamu tu ndio wachinje na Wakristo wasichinje.
Sharti la pili ambalo Nchimbi alipewa na kulitekeleza hapo hapo ni kuwaachia wachungaji waliokuwa wamekamatwa kwa madai ya kuchinja, wakati sharti la tatu lilimtaka athibitishe kuwa wachungaji na Wakristo wengine wataacha kunyanyaswa na Waislamu.
Sharti la nne lilimtaka Nchimbi atamke kuwa serikali itagharamia matunzo ya familia ya mchungaji aliyeuawa na mazishi yake kwa sababu kifo chake kimetokana na uzembe wa serikali kutochukua hatua dhidi ya jambo hilo pamoja na kulalamikiwa na kupewa taarifa na wachungaji kwa barua.
Hata hivyo, Nchimbi aliomba jambo hilo hususan matunzo ya familia aliwasilishe kwa wakubwa wake wa kazi, hususan Waziri Mkuu ili waweze kupata ufumbuzi wa pamoja.
Pamoja na juhudi hizo za Nchimbi, Mkuu wa Mkoa Saidi Magalula, na Mkuu wa Wilaya Ludorick Mpogolo, walikataliwa kabisa na wananchi, kiasi cha kushindwa kuhudhuria mazishi ya mchungaji huyo.
Mashuhuda waliokuwepo kwenye msiba huo, wanasema Mpogolo aliyekuja kwa niaba ya serikali alizomewa hali iliyomsababisha atoe rambirambi haraka na kuondoka eneo la tukio.
Taarifa zaidi zilizopatikana zinasema Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa kufika Geita leo ili kutafuta suluhu ya madhehebu hayo.
Wakazi wa kata za Buseresere na Katoro katika wilaya za Chato na Geita walilalamikia serikali kushindwa kutoa msimamo juu ya mgogoro huo na kuufanya wa kisiasa zaidi jambo lililosababisha vurugu na mauaji ya mchungaji na baadhi ya raia kujeruhiwa vibaya.
Katika vurugu hizo, mali za wananchi zimeharibiwa vibaya huku baadhi ya maduka na bidhaa zikiteketezwa kwa moto.
Miongozi mwa wananchi walioharibiwa mali zao ni pamoja na Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Chato na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Buseresere, Yusuf Idd Banana ambaye ametaja mali zilizoharibiwa kuwa na thamani ya sh milioni 10.
Waziri Nchimbi hakupatikana kwa simu
kuzungumzia hali hiyo kwa kuwa simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa.
CHANZO http://www.freemedia.co.tz
0 comments:
Post a Comment