BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UZEMBE TENA, SERIKALI YATUPIWA LAWAMA.



GHOROFA LAPOROMOKA NA KUUA WATU WATANO, 15 WAJERUHIWA.
http://www.freemedia.co.tz
UZEMBE wa serikali kutotekeleza mapendekezo ya ripoti iliyobaini upungufu kwenye majengo marefu ya ghorofa umeleta tena maafa kwa watu watano kupoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa.

Tukio hilo limetokea jana asubuhi baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linaendelea kujengwa katika mitaa ya Indira Ghandi na Morogoro kuporomoka na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo ya katikati ya jiji.

Hata hivyo, huenda idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na watu wengine zaidi ya 40 kuhofiwa kufunikwa na kifusi wakiwamo mafundi pamoja na watoto waliokuwa wakicheza jirani na jengo hilo.

Jengo hilo lililoko katika kitalu Na.166 ni mali ya Raza Ndagji na mjenzi wake ni Kampuni ya Lucky Construction Limited.

Baadhi ya watu walidai jengo hilo kujengwa chini ya kiwango kutokana na vifaa vilivyotumika, ingawa mkandarasi huyo hajapatikana kulieleza hilo wakati huu ambapo uokoaji unaendelea kwa kutumia vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama.

Majeruhi hao 15 walipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu huku wawili kati yao hali zao zikiwa mbaya. Pia magari madogo manne yalipondeka baada ya kufukiwa na kifusi.

Tukio hili limetokea wakati serikali ikiwa bado haijachukua hatua za kurekebisha kasoro zilizobainishwa na tume iliyoundwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa baada ya kuporomoka kwa ghorofa la Chang’ome Village Hoteli Inn mwaka 2006 na kuua mtu mmoja.

Tume hiyo ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam yalikuwa yamejengwa kinyume na taratibu za ujenzi. Kati ya maghorofa 505 ambayo waliyakagua, 147 yalikutwa hayana nyaraka za ujenzi.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliliambia Bunge kuwa tume hiyo ya Lowassa ilibaini kuwa katika ukaguzi huo pia maghorofa 81 yalikutwa yamekiuka masharti ya ujenzi huku mengine 22 wenyewe hawakupatikana na yalikuwa yamejengwa bila kuzingatia sheria za ujenzi.

Hali ilivyokuwa 
Tanzania Daima lilifika eneo la tukio majira ya saa 2:49 asubuhi na kukuta hatua za awali za uokoaji zikiendelea na baada ya muda viongozi mbalimbali waliwasili pamoja na vikosi vya uokoaji.

Vikosi mbalimbali vya polisi wakiwa na mbwa pamoja na farasi vilizingira eneo hilo kuimarisha ulinzi na baadaye vikosi vya Jeshi la Wananchi (JWTZ) na lile la Kujenga Taifa (JKT) viliwasili.

Majira ya saa 6:45 mchana, Rais Jakaya Kikwete akiambatana na mkewe Salma Kikwete walifika huku kiongozi huyo akionekana mwenye hasira ingawa hakuzungumza chochote zaidi ya kuangalia na kuondoka.

Baadaye kupitia Kurugenzi yake ya Mawasiliano Ikulu, rais alitoa maagizo akizitaka taasisi za kitaaluma zinazohusika na shughuli za ujenzi, wachoraji majengo, wakadiriaji majengo, wajenzi, makandarasi na wahandisi nazo zichunguze tukio hilo kwa haraka.
Alisema baada ya kubaini yapi yalikuwa ni matatizo, zichukue hatua kwa mujibu wa madaraka na mamlaka yao.

Rais Kikwete pia aliwapa pole wafiwa pamoja na majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu baada ya kubanwa katika kifusi, wakiwamo watoto wadogo ambao walikuwa wanacheza chini ya jengo.

Alitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa Saidi Mecky Sadik pamoja na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova kuhakikisha mjenzi wa jengo hilo, Mhandisi mshauri aliyekuwa anasimamia ujenzi, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam aliyetoa kibali cha ujenzi na pia Mkaguzi wa ujenzi pamoja na mwenye jengo wanapatikana haraka na kuwajibishwa.

Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, mmiliki wa jengo hilo alikuwa tayari amekamatwa na Jeshi la Polisi.

Kamanda Kova alisema hadi sasa kuna baadhi ya viongozi wa Manispaa ya Ilala wanashikiliwa kwa mahojiano ya awali.

Viongozi hao ni Mhandisi Mkuu wa Manispaa hiyo, Ogare Salu, Mkaguzi wa Majengo, Wilbrod Bulyabuso na Mhandisi Goodluck Mbaga.

Kova alisema kuwa Mbaga alikuwa akihusika katika kulikagua jengo hilo mara kwa mara.

“Lakini nataka mtambue kuwa hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa jengo hilo limejengwa chini ya kiwango, hadi wataalamu watakapotoa taarifa baada uchunguzi wao,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadik alisema hali ya uokoaji ilikwenda taratibu kutokana na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni inayojenga jengo hilo kukosekana kutokana na jana kuwa mapumziko.

“Madereva wa mitambo kwa ajili ya uokoaji hawakuweza kupatikana pia kupata taarifa muhimu kuhusu ni wafanyakazi wangapi walikuwemo ndani wakati jengo hilo linaporomoka,” alisema.

Walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa kulikuwa na watu wengi kwani ilikuwa ni siku ya kumwaga zege.

Naye Aliridha Viranj (12) aliyeokolewa akiwa salama alisema kuwa alikuwa na watoto wenzake wapatao 13 wakicheza mpira.

“Wakati naondoka kabla sijafika mbali nikasikia sauti kubwa na mara vumbi likatanda eneo zima, nikarudi tulipokuwa tunacheza na kumkuta kaka yangu akiwa pembeni ameumia na ndipo wakaja watu na kuwasaidia, wenzangu wengine watano na kuwapeleka hospitali,” alisema.

Aliwataja waliosalia ambao bado hawajatoka kuwa ni Yusuf Khaki, Suhail Karim, Zahid Abbas Kanji na Salmin Damji.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: