CHAMA kikuu cha upinzani nchini Ujerumani SPD, kimezindua kampeni yake
siku ya Jumapili, kikiahidi ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwezi
Septemba mwaka huu.
Lakini kura za maoni zinamuweka mgombea wa chama hicho cha mrengo wa kati-kuelekea kushoto Peer Steinbrück, nyuma ya mhafidhina Angela Merkel kwa tofauti kubwa, na umaarufu wa Kansela huyo umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60, wakati ni chini ya theluthi moja ya Wajerumani wanaompendelea Steinbrück kama Kansela.
Steinbrück, mwenye umri wa miaka 66, alisema serikali ya Kansela Merkel haina jipya la kuwafanyia Wajerumani, na kubainisha vipaumbele vyake vinavyosisitiza malipo ya haki ya mashahara, pensheni, na viwango nafuu vya pango, na msisitizo mkubwa juu ya uundwaji wa nafasi zaidi za ajira, kuliko mfumo wa Merkel wa kubana matumizi. Juu ya hayo, Steinbrück anataka kuweka viwango vikali kudhibiti masoko ya fedha.
Achochea hamasa ya wanachama
Wajumbe wengi walishawishika na hotuba yake. Klaus Wowereit, meya maarufu wa jiji la Berlin kwa tiketi ya SPD, alisema chama hicho sasa kiko katika hali ya kampeni, na kuongeza kuwa Steinbrück aliweza kuwashawishi hata wale ambao siyo mashabiki wake ndani ya chama.
"SPD hivi sasa iko katika hali kamili ya kampeni.
Huo ndio ulikuwa ujumbe hapa leo," alisema Wowereit na kuongeza kuwa chama hicho bado kina hamasa.
Mgombea Peer Steinbrück akisalimiana na wajumbe wa chama cha SPD
wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho mjini Augsburg siku ya Jumapili.
Lakini wakati ambapo mshirika wa sasa wa Kansela Merkel, chama cha kiliberali cha FDP, kikiwa na matumaini madogo sana ya kuvuka asilimia 5 inayohitajika ili kupata uwakilishi bungeni, na huku SPD na washirika wao, chama cha kijani wakiondoa uwezekano wa kushirikiana na chama chenye msimamo mkali wa kushoto, uwezekano wa muungano mpya unaonekana kutoepukika.
"Nadhani bado kuna uwezekano wa nyekundu-kijani (SPD na chama cha Kijani), lakini mtu anapaswa kufikiria kuhusu njia mbabadala," alisema mwanachama mwandamizi, ambaye hakutaka jina lake litajwe, na alikuwa akitafakkari juu ya nini SPD itataka wakati itakapolaazimu kufanya mazungumzo ya ushirikiano na Merkel.
Uchaguzi mkuu Septemba 22
Raia wa Ujerumani watapiga kura katika uchaguzi mkuu Septemeba 22, ambapo Steinbrück na chama chake cha SPD ndio wapinzani wakuu wa Kansela Angela Merkel na chama chake cha Christian Social Union CDU.
Kura ya maoni iliyoendeshwa hivi karibuni na kituo cha televisheni cha umma, ARD, ilionyesha kuwa umaarufu wa Kansela Merkel umeongezeka kwa gharama ya upinzani, ingawa kura hiyo iliendelea kuonyesha uwanja wa kisiasa ambapo hakuna kati ya miungano yote - ulio na uungwaji mkono wa kutosha kupata wingi wa kuunda serikali kivyake.
Mwenyekiti wa chama cha Kijani, ambacho kinashirikiana na SPD katika uongozi Claudia Roth akihutubia mkutano wa SPD.
Nafasi nzuri aliokuwa nayo Steinbrück hapo awali iliharibiwa na makosa ya mfululizo aliyoyafanya na kuandikwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari, ikiwemo mapato makubwa aliyoyapata kutokana na kutoa hotuba katika shughuli za umma, matumizi yake ya pombe za rahisi, matamshi kwamba jinsia ya Kansela Merkel inamsaidia kisiasa, na mapendekezo ya kuongezwa kwa mashahara wa kansela, ambao kwa sasa unafikia kiasi cha euro lakini tatu kwa mwaka.
0 comments:
Post a Comment