BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIONGOZI VIDUDU MTU.

MTAZAMO WANGU.http://www.freemedia.co.tzhttps://si0.twimg.com/profile_images/1131272789/bbb.JPG
Na Bryceson Mathias. 
JE, mtu anapokuwa kinara wa kutoa habari za uongo, uchochezi, propaganda, zinazohusu vyama pinzania, ndani ya chama tawala hiyo ni tiketi ya kufaa kuwa kiongozi ?.

Kama ndivyo, tuna watu wengi wabovu ndani yake, hivyo mtu anaweza kuvaa nguo za kijani, kofia, tisheti, kanga na vitambaa mabegani na shingoni, akatunukiwa kwa uongo wake, akapata uongozi !.

Biblia katika Mathayo 7:21 inasema: “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”

Kwa msingi huo, si kila mwana CCM, mtu au mwanasiasa akisema kuwa anayo video inayowaonesha viongozi wakipanga mikakati fulaji atakuwa mkweli, kutakiwa achaguliwe kuwa kiongozi wa ngazi ya juu! Na hao wapo wengi na ni waongo.

Kwa mtazamo wangu, si kila mbunge mjengoni anafaa kuwa mwakilishi mzuri wa wananchi. 

Wengine tunawajua kwa matendo yao, ni usingizi hadi watoke, hao ni mizigo isiyobebeka, kiasi hata wapiga kura wanaomba uchaguzi wa mwaka 2015 ufike haraka wawatose.

Maana kwa sasa wanateseka na kujuta, wakijilaumu kwa nini walifanya makosa ya kuwachagua ?.

Siku moja nilimuonya mtu, akienda mikoa fulani awe na hekima, asije akamtukana mbwa, kwa Watanzania wengine ni nyama. 

Asipige teke vigunzi vya mahindi, vifuu vya nazi na kuongea ovyo na watu warefu wenye nguo nyeupe na kukubali kubeba mizigo isiyo na mapatano; akanipuuza.

Ghafla alipopita kona moja, alikikuta ‘kidudu mtu’ kikamuita kwa huruma na kujifanya chema huku kina bakuli ya kuombea msaada. 

Kilipozungumza naye kwa sauti ya upole na unafiki, alikisikiliza na akakipa msaada, kikamuomba akibebe akisogeze kwenye eneo la watu.

Alipiga magoti akakibeba mgongoni hadi mbele ya watu kilipotaka. Alipopiga magoti kishuke, kilikatalia mgongoni kikidai hakiwezi kushuka labda akipeleke kilabuni kinywe pombe.

Kilifungua kucha zake, kikaanza kumparura mgongoni kikidai kinyweshwe pombe.

Kwa kupuuza ushauri na kupokea udanganyifu ili asiumizwe zaidi akakipeleka kwenye pombe, kikadai kunywa kikiwa mgongoni na kikimaliza kitashuka.

Kilipomaliza, hakikushuka, kikadai kinunuliwe sigara, kikamparura hadi alipokinunulia kikavutia mgongoni, hata hivyo hakikushuka!.

Kikiwa mgongoni kikasema, ni kichawi kinaua na kula nyama za watu, hivyo kinamtaka wakaroge, waue na kula pamoja nyama za watu na wakikamilisha kitashuka na kumuacha aende zake!

Aliposema amechoka, maana alikibeba mchana kutwa na usiku, kikamparura kwa makucha, ikabidi aende nacho wakaroge, wakaua na kula nyama hizo.

Muda wote kikiwa mgongoni, kidudu mtu kilikuwa kinanyonya damu kidogo kidogo, ilipokwisha mtu yule alianguka akafa.

Yawezekane nchini tunao baadhi ya viongozi ni vidudu mtu, wameng’angania migongoni mwa taifa hili wakinyonya haki za wananchi kwa hila mbalimbali hadi damu na uchumi wetu uishe, tufe. 

Hao lazima tuwakatae! Tunawakataa si eti si Watanzania la hasha, hawalitakii mema taifa hili, wanataka tuwabebe hadi Mabwepande wakatunyonye damu ?.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715933308
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: