MATUKIO YA KISIASA. http://www.dw.de
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nicolas Tiangaye ametangaza
baraza jipya la mawaziri baada ya kufanyika mapinduzi, ambalo asilimia
wanatoka kwenye kundi la waasi la Seleka na chama cha zamani cha
upinzani.
Tiangaye, ambaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu na kiongozi wa waasi,
Michel Djotodia aliyeongoza mapinduzi na kujitangaza rais baada ya
kuudhibiti mji mkuu wa Bangui, aliitangaza serikali hiyo mpya jana
Jumapili jioni kupitia redio ya taifa. Mbali na kuwa rais, Djotodia
amejiongezea nafasi ya waziri wa ulinzi.
Baraza hilo lenye mawaziri 34, linajumuisha tisa kutoka kundi la waasi
wa Seleka, wanane wanatoka chama cha zamani cha upinzani na mmoja ni
mshirika wa karibu wa rais aliyeondolewa madarakani, Francois Bozize,
aliyelazimika kuikimbia nchi hiyo, baada ya waasi kuidhibiti Bangui.
Mawaziri wengine 16 bado hawajulikani wanatoka makundi gani ya kiraia.
Nafasi muhimu zashikwa na Seleka.
Nafasi za mawaziri wa petroli, usalama, maji na misitu, na mawasiliano,
zimechukuliwa na waasi wa Seleka, ambapo wizara ya habari na mawasiliano
ikiongozwa na Christophe Gazam Betty.
Serikali hiyo mpya itakuwa
madarakani kwa muda wa miaka mitatu, hadi hapo itakapoitisha uchaguzi
mkuu ambao Bozize amepigwa marufuku kushiriki.
Rais aliyepinduliwa, Francois Bozize.
Ijumaa iliyopita, Djotodia alitangaza kuongoza nchi kwa
kuzingatia mkataba wa amani uliofikiwa mwezi Januari mwaka huu na
ameahidi kuondoka madarakani mwaka 2016 na kwamba hatoshiriki katika
uchaguzi.
Ufaransa na Marekani iliitaka serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati
kuheshimu mkataba wa kugawana madaraka uliosainiwa Gabon.
Hata hivyo,
Marekani imesema Waziri Mkuu, Nicolas Tiangaye, aliyeteuliwa kushika
nafasi hiyo kulingana na mkataba huo, ndiye kiongozi halali wa serikali.
Waasi wa Seleka walianza harakati za kuingia Bangui mwezi Desemba mwaka
uliopita kabla ya kukubali kushiriki kwenye mazungumzo ya amani na
serikali ya Rais Bozize.
Baada ya siku kadhaa za kupora vitu na ghasia,
wanajeshi waasi wameudhibiti mji wa Bangui kwa msaada wa kikosi cha
Afrika katika ukanda huo.
Wanajeshi wengi waliouawa walikuwa watoto
Lakini taarifa za kushtua kuhusu watoto wanajeshi kuuawa katika
mapambano ya kuudhibiti mji wa Bangui zimechapishwa na gazeti la Afrika
Kusini jana Jumapili.
Mpiganaji mdogo wa Seleka.
Gazeti la Sunday Times limewanukuu wanajeshi wakisema kwamba wengi wa wanajeshi waasi waliouawa walikuwa ni watoto.
Afrika Kusini imekataa kulizungumzia suala hilo.
Afrika Kusini ina
wanajeshi wake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikiwa ni kikosi cha
kudhibiti usalama nchini humo kabla ya kuanguka kwa Bozize, jitihada
ambazo zimeshindwa.
Wanajeshi wake 13 waliuawa katika mapigano katika
Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wiki iliyopita, Umoja wa Afrika uliusimamisha uanachama Jamhuri ya
Afrika ya Kati na imewawekea vikwazo waasi wa Seleka, akiwemo Djotodia.
Tangu ijipatie uhuru wake kutoka Ufaransa, mwaka 1960, Jamhuri ya Afrika
ya Kati imeshuhudia mapinduzi ya mara kadhaa.
Wasiwasi wa kidini
umeongezeka katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Wakristo, tangu
Djotodia ambaye ni Muislamu kujitangazia urais.
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment