BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWENYEKITI CHADEMA FREEMAN MBOWE: SPIKA NI DIKTETA

NI BAADA YA KUHALALISHA UAMUZI WA NDUGAI.
http://www.freemedia.co.tzSpika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda (katikati).

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda analiendesha Bunge kidikteta.

Alisema vurugu na ghasia zinazotokea bungeni wakati wa mijadala mbalimbali zinatokana na spika na naibu wake Job Ndugai kutaka kuliendesha Bunge kidikteta kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alitoa kauli hiyo jana kupinga uamuzi wa spika wa kuridhia adhabu iliyotolewa na Ndugai dhidi ya wabunge sita wa CHADEMA.

Wabunge hao ambao walitolewa bungeni na kuzuiliwa kuhudhuria Bunge kwa siku tano ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiel Wenje (Nyamagana) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).


Awali akisoma uamuzi wake jana bungeni kufuatia mwongozo alioombwa na Mbowe, Spika Makinda alisema uamuzi uliofanywa na naibu wake, Ndugai ni sahihi.

Ndugai aliamuru Lissu atolewe nje kwa kukiuka kanuni ya 60 (12) wakati aking’ang’ania kutoa mwongozo wakati naibu spika akimzuia.

Makinda alisema adhabu hiyo ilitokana na kukaidi agizo la kiti la kumtaka kukaa wakati alipompatia nafasi Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga (CHADEMA).

Alisema wabunge wengine watano walipewa adhabu hiyo kwa kosa la kuwazuia wapambe wa Bunge kutekeleza agizo la naibu spika la kutaka kumtoa nje Lissu na kusababisha fujo.

“Waheshimiwa wabunge, kanuni zetu na hasa ya 2 (2) na kanuni ya 5(1) ya kanuni za Bunge imempa mamlaka spika kufanya uamuzi pale ambapo hakuna utaratibu wa kanuni.

“Aidha uamuzi unaofanywa na spika ambao unaruhusu uendeshaji bora wa shughuli za Bunge wa kuleta amani na utulivu bungeni, unaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji wa Bunge.

“Kwa kitendo kilichotokea Aprili 17 bungeni, hakiwezi kupuuzwa kwa kuwa ni kitendo dhahiri cha kudhalilisha mamlaka ya spika na kilikuwa kitendo cha utovu wa nidhamu wa hali ya juu. 

Watanzania wote waliushuhudia na wanalaani kilichokuwa kinaendelea ukumbini,” alisema Makinda.
Alifafanua kuwa mbunge yeyote aliyekuwa anaongoza Bunge wakati huo, angeweza kutoa uamuzi huo.

“Ninatumia kanuni ya 5(1) na kanuni ya 2 (2) ya Bunge inayompa mamlaka spika kufanya maamuzi ambapo jambo ama shughuli yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi.

“Uamuzi uliofanywa na mheshimiwa Job Ndugai, naibu spika wa kuwatoa nje Mheshimiwa Tundu Lissu…na kubaki nje kwa kutohudhuria vikao vya Bunge siku tano ni halali,” alisema na kuongeza:

“Na sasa utaingizwa katika kitabu cha maamuzi ya spika, na mbunge yeyote atakayefanya vitendo hivi apewe adhabu hii.”

Kauli ya Mbowe
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa mara baada ya uamuzi wa Spika Makinda, Mbowe alisema kama kiti cha spika hakitakuwa tayari kusimamia haki, wabunge wa CHADEMA hawataacha kusimama kuomba utaratibu wa kuzungumza kupinga hoja za upotoshaji za mawaziri na wabunge wa CCM na uendeshaji mbovu wa Bunge.

Alisema kanuni ya 2(2) na kanuni ya 5(1) ya kanuni za Bunge kweli inampa mamlaka spika kufanya uamuzi pale ambapo hakuna utaratibu wa kanuni.

“Kosa la wabunge wetu adhabu yake iko kwenye kanuni. Kanuni aliyotumia inahusu kwa mfano, wewe mwandishi wa habari umetoka sehemu yako, ukaingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kuanza kupigana.

“Hapo hakuna kanuni ya kukuadhibu na ndiyo spika anaweza kutumia hiyo kanuni na kisha kuingiza kwenye kumbukumbu ili iweze kutumika baadaye, lakini sio katika kosa la wabunge wetu,” alisema Mbowe.

Alisema uamuzi wa spika ni wa kitoto kwani amezidi kukoroga kanuni kwa ajili ya kumlinda naibu wake.

“Hatutangazi vita na Bunge, lakini kama Bunge halitakubali kufuata haki, wategemee hali hii kuendelea kujitokeza kwani hatutaogopa kufukuzwa kwa kupigania haki,” alisema.

Alisema Lissu alipata adhabu ya kutolewa nje na kufungiwa vikao vitano kwa sababu alisimama mara nyingi kuomba mwongozo na kutoa ufafanuzi wa hoja za kupotosha.

“Lissu au mbunge mwingine yeyote atasimama hata zaidi ya mara 100 kuomba kuzungumza, na tunafanya hivyo kutokana na wingi wa hoja za hovyo za serikali na wabunge wa CCM, na hakuna kanuni inayozuia kuzungumza mara nyingi, na katika hilo tuko tayari kufukuzwa wote,” alisema.

Mbowe alirejea kauli aliyoitoa juzi wakati akiomba mwongozo kuwa kilichotokea bungeni ni sintofahamu kati ya wabunge na kiti cha spika ambapo katika mambo ya msingi, CHADEMA ilitegemea kifungu cha nne cha kanuni za Bunge, kifungu kidogo cha kwanza kingetumika.

“Kifungu hicho kinasema hivi: ‘Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge, ikiwa;
Kwa maneno au vitendo, mbunge huyo anaonesha dharau kwa spika au mbunge huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo’.

“Kosa la wabunge wetu linaangukia kwenye kanuni hii kwamba wameonyesha dharau pale walipokaidi kutoka nje. 

Kanuni iko wazi kwamba spika atapeleka majina ya wabunge hao kwenye Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge ambako watapewa nafasi ya kusikilizwa na kutoa ushahidi kabla ya kuhukumiwa,” alisema.

Mbowe alieleza kushangazwa na hukumu hiyo kwani hakuna mbunge wala kiongozi yeyote wa CHADEMA aliyeitwa kusikilizwa, na hata uamuzi wa spika nao haukuzingatia kuwahoji wahusika.

Aliitaka jamii kujiuliza kwanini wabunge hao wanapokutana nje ya Bunge ni marafiki wa karibu, lakini wakiingia ndani ya Bunge vurugu za kurushiana maneno hujitokeza.

“Huwezi kukuta wabunge nje wanagombana kwa sababu wanaheshimiana. 

Ndani ya Bunge chanzo cha hao wanaopatana nje kurushiana maneno ni kiti cha spika kushindwa kusimamia haki na kanuni,” alisema.

Hatua za kuchukua
Pamoja na Spika Makinda kuridhia adhabu ya Ndugai dhidi ya wabunge wa CHADEMA, Mbowe alisema wanatarajia kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni kupinga uamuzi wa spika.

Alisema anajua CHADEMA itashindwa katika kesi hiyo, lakini wanataka kuweka rekodi na kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Alisema Spika Makinda kama ilivyokuwa kwa Ndugai, amekosea kuridhia adhabu hiyo.

Katika hatua nyingine, Mbowe alisema kuwa Bunge limenajisiwa kwa kuruhusu watu wasiotakiwa kikanuni kuingia bungeni kiholela kwa nia ya kutaka kumtoa Lissu.

Akifafanua, alisema kisheria wanaoruhusiwa kuingia bungeni ni wabunge, uongozi wa Bunge na watumishi wao, na kama kuna mtu mwingine anataka kuingia lazima kanuni itenguliwe.

“Ukiacha rais ambaye ni sehemu ya mbunge, mtu yeyote haruhusiwi kuingia bila kutengua kanuni. 

Juzi Ndugai alivunja kanuni kwa kuruhusu askari kuingia bungeni wakati siwa iko mbele na hadi sasa hakuna taarifa iliyotolewa,” alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: