NAIBU Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo amesema atawafikisha
mahakamani watu wanaodai kuwa ameghushi vyeti vya elimu ya sekondari.
Mulugo alisema amechoshwa na kashfa hizo zinazosambazwa na baadhi ya
watu atawafikisha mahakamani endapo wataendelea kumdhalilisha.
“Wanasema eti nimeghushi vyeti, mara
ooh sijui natumia jina la mtu. Nimechoshwa na maneno haya… ni kweli
nimerudia darasa kama walivyorudia watu wengine, kwa nini iwe tatizo
kwangu. Hata hapa tulipo wapo wengi tu waliorudia darasa.
“Kama kweli ningekuwa nimeghushi
vyeti hivi leo ningekuwa naibu waziri wa elimu? Sasa nimechoshwa,
nitawachukulia hatua watu hawa, siwezi kusema ni lini nitafanya hivyo
ila nitakapoamua nitaanza,”alisema.
Kwa miezi kadhaa sasa Mulugo amekuwa
akidaiwa kughushi vyeti na kutumia jina la mtu ili kufikia kiwango cha
elimu alichonacho madai ambayo alisema yanamchafulia jina katika jamii.
Kuhusu suala la matokeo mabaya ya
kidato cha nne mwaka jana, Mulugo alisema matokeo hayo mabaya
yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa
wanafunzi.
Naye Ruth Mnkeni kutoka Dar es
Salaam anaripoti kuwa Mlugo amezindua tovuti ya elimu kwa wanafunzi wa
shule ya sekondari ijulikanayo kama Shule Direct.
Muluigo alisema kuzinduliwa kwa
tovuti hiyo kutawafanya wanafunzi kupata maarifa mengi ya vitabu
mbalimbali na kuinua kiwango cha elimu nchini
0 comments:
Post a Comment