WADAU WATANGAZA KUISHITAKI SUMATRA MAHAKAMANI, WAMILIKI WA MABASI WASEMA NCHI INAKOSA USAFIRI.
http://www.mtanzania.co.tz
Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA), Hassan
Mchanjama, akizungumza na waandishi wa habari jijini jana kuhusu kupinga
kupandishwa kwa nauli kulikofanywa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti
wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
SAKATA la ongezeko la nauli mpya za daladala na mabasi yaendayo mikoani, sasa ni wazi kuwa limegeuka kuwa kaa la moto.
Hali hiyo inajitokeza baada ya Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA), kutangaza kusudio la kuishitaki Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kwa hatua yake hiyo.
Uamuzi huo ulitangazwa na Mshauri wa Idara Kuu ya Huduma ya Maoni ya chama hicho, Wilson Mashaka wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Mashaka alisema chama chake kinakusudia kuishitaki SUMATRA, kutokana na kupandisha nauli kiholela bila kushirikisha wadau wa usafiri, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.
Mashaka alisema sababu na vigezo vilivyotumika kuishawishi SUMATRA kufanya mabadiliko hayo ya nauli, hazina msingi wala mashiko mbele ya jamii.
“Hizi nauli zimepandishwa kwa hila na nia ya kuweka rehani maisha ya wananchi masikini ambao hawana uwezo wa kumiliki usafiri kama watu wengine.
“Suala la usafiri ni haki ya kikatiba ya kila mwananchi kwenda mahali popote anakotaka, kwa kulipa nauli inayofaa na linganifu katika vyombo vya usafiri,” alisema.
“Madai ya kupata hasara kutoka kwa wamiliki yasiyokuwa na ukweli siku zote yanaaminika kwa SUMATRA tu, kwani taarifa ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha ya wamiliki wa mabasi haijatolewa.
“Maamuzi ya kupandisha nauli hizo hayakuzingatia ukweli kuwa wamiliki wa mabasi wana mfumo mbaya wa kuwagawia pesa wapiga debe na askari traffic barabarani.
“Sasa fedha hizo ambazo hutolewa kiholela, wamiliki wanataka zilipwe na wananchi, huo ndiyo msingi wa wamiliki wa mabasi kutaka abiria wapandishiwe nauli ili kufidia,” alisema.
0 comments:
Post a Comment