Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dkt Ali
Muhammed Shein amesema kuwa ataendelea kukiimarisha na kukienzi Chama Cha
Mapinduzi pamoja na kuulinda Muungano wa Serikali mbili uliopo.
Kauli hiyo ameitoa leo huko katika ukumbi wa CCM Mkoa Amani
wakati akizindua ziara yake ya Mikoa mitano ya Zanzibar.
Dkt Shein ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar amesema kuwa kuna kila sababu ya kukiimarisha chama hicho kutokana na
umuhimu wake na kwamba Muungano uliopo wa Serikali mbili ndio njia bora ya
kuendeleza mashirikiano ya kidugu yaliyodumu kwa muda mrefu.
Amesema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kupata taarifa za
matukio mbali mbali pamoja na changamoto zilizopo katika mikoa hiyo zinazohusu
CCM.
Aidha amewataka viongozi wa CCM kuwa na mashirikano mazuri
katika kukiimarisha Chama na kuhakikisha kwamba kinapata ushindi katika kila
uchaguzi unaokuja.
Dkt. shein amesema kuwa ana imani na Chama chake kuibuka mshindi
katika chaguzi kutokana Chama hicho kuchagua uongozi makini ambao utahimili
vishindo vya uchaguzi ujao.
Katika hatua nyingine Dkt Shein aliwataka Wananchi kuendelea
kujishughulisha na harakati zao za kujiletea maendeleo na kuepuka kuvunja
sheria za nchi.
“Serikali inataka amani na utulivu kwa Wananchi wake sambamba na
kuimarisha maendeleo kama Malengo ya Mapinduzi yalivyoelekeza na kwa njia hiyo
hatuna budi kuyaenzi Mapinduzi” alieleza Makamo Mwenyekiti wa CCM.
Katika ziara hiyo Makamo Mwenyekiti amezindua Tawi jipya la CCM
la Vikokotoni, Kikwajuni SACCOS BANK pamoja na kutoa kadi 270 kwa wanachama
wapya wa Chama cha Mapinduzi.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
0 comments:
Post a Comment