Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo.
JESHI la Polisi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam limekumbwa na kashfa baada ya askari wake mmoja kudaiwa kushiriki kumpa kipigo fundi magari mkazi wa Temeke Mikorosheni, Gaspa Mlay, hivyo kusababisha kifo chake na kisha mwili wake kutelekezwa nyuma ya kituo cha polisi.Tukio hilo lilitokea Jumamosi wiki iliyopita baada ya askari mmoja (jina tunalo), wa kituo kidogo cha polisi cha Sandali kwa kushirikiana na mmiliki wa nyumba aliyokuwa amepanga marehemu (Gaspa) kumshambulia kwa kipigo na kusababisha kifo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, hata hivyo, amekana kuwa askari wake ameshiriki katika mauaji hayo.
“Nasita kufanya kazi na nyie kupitia kwenye simu, tukio lenyewe limetokea tangu Jumamosi, na muda huu sipo ofisini, lakini kimsingi siyo kweli kwamba kuna askari ameshiriki katika mauaji hayo, njoo kesho (leo), nitakueleza tukio lilivyo na OCCID (Mkuu wa Upelelezi wa Kituo) atakuwapo,” alisema Kiondo.
Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE jana akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke ambako mwili wa marehemu umehifadhiwa, mjomba wa marehemu, Peter Masoyi, alisema Gaspa ambaye sasa ni marehemu alipewa notisi na mwenye nyumba kutakiwa kuhama katika nyumba aliyopanga eneo la Temeke Mikorosheni.
Alisema bahati mbaya kwa takribani mwezi mmoja marehemu (Gaspa), hakufanikiwa kupata nyumba nyingine ya kupanga na hivyo aliendelea kuishi katika nyumba aliyokuwa amepewa notisi ya kuhama.
Masoyi alisema kitendo cha Gaspa kuendelea kuishi katika nyumba hiyo kilimuudhi mwenye nyumba ambaye aliamua kuchukua umuazi wa kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Sandali kuomba msaada ili aondolewe kwa nguvu kutoka katika nyumba hiyo.
Baadaye polisi mmoja wa kituo hicho, mwenye nyumba na mjumbe wa mtaa walikwenda katika nyumbani aliyokuwa anaishi Gaspa na kumgongea mlango katika chumba alichokuwa amelala, lakini aligoma kufungua mlango.
Alisema baadaye askari huyo na mjumbe waliamua kuvunja kitasa na kufuli la mlango huo na kuingia ndani kwa lengo la kumtoa kwa nguvu Gaspa kutoka katika chumba alichokuwa amelala na kutokea vurugu kubwa zilizosababisha Gaspa kupigwa na kujeruhiwa vibaya na kusababisha ashindwe kutembea.
Baada ya tukio hilo, polisi na mjumbe huyo walikodi pikipiki na kumpeleka Gaspa kituoni na baadaye walimfuata mdogo wake Gaspa aitwaye Elias Mlay anayefanya kazi gereji eneo la Temeke Sterio kumweleza kuwa ndugu yake amesababisha uharibifu kwa kuvunja mlango wa nyumba ya watu.
Aliongeza kuwa askari hao walimweleza Elias kuwa kama anataka ndugu yake aachiwe huru kutoka kituoni hapo atoe Sh. 300,000.
Hata hivyo, Elias kabla ya kukubali kutoa kiasi hicho cha fedha, alimweleza askari huyo kwamba akajionee uharibifu aliofanya ndugu yake na baada ya kufika eneo la tukio, alikuta kilichoharibiwa ni kitasa na kufuli na hivyo kugoma kutoa fedha hizo badala yake akamweleza kuwa yupo tayari kutoa Sh. 20,000.
Askari huyo alikubali kupokea Sh. 20,000 kwa makubaliano kuwa atamuachia Gaspa huru, lakini wakati anakwenda kufanya kazi hiyo, alimweleza Elias kuwa asiambatana naye kwenda kituoni badala yake ikifika mchana ampigie simu kuuliza kama atakuwa ameachiwa.
Masoyi alisema ilipofika saa 7:00 mchana, Elias alipompigia simu askari huyo kufahamu kama amemwachia ndugu yake alijibiwa kuwa ameshafariki dunia na mwili wake upo kituoni hapo.
“Eliasi alivyoelezwa hivyo hakuamini badala yake alikwenda mwenye kituoni na baada ya kufika alikuta kweli ndugu yake ameshafariki (dunia) na mwili wake umewekwa nyuma ya kituo cha polisi huku ukiwa umevimba tumbo,” alisema Masoyi.
Alisema baadaye Elias alikwenda kutoa taarifa kituo kikubwa cha polisi Chang’ombe na polisi wa kituo hicho walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kuupeleka Hospitali ya Wilaya ya Temeke na baadaye walimkamata mwenye nyumba alikokuwa akiishi Gaspa siku ya Jumamosi jioni.
Hata hivyo, ndugu wa marehemu Gaspa walianza kuhoji kwanini askari anayedaiwa kushiriki katika tukio hajakamatwa, lakini walijibiwa na askari waliokuwa wakifuatilia suala hilo kwamba kama wana ushahidi na jambo hilo watoe ushahidi na askari huyo atakamatwa.
Jumanne wiki hii ndugu wa marehemu walipokwenda Hospitali ya Wilaya ya Temeke, walielezwa na askari waliokuwa wakifuatilia suala hilo kuwa mwili wa marehemu unatakiwa kwenda kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini itashindikana kwenda huko sababu gari la polisi halina mafuta.
Majibu hayo hayakuwafurahisha ndugu za marehemu ambao waliamua kwenda kumwona Kamanda Kiondo ambaye baada ya kuwaita askari wa kituo hicho walimweleza kuwa askari anayetuhumiwa amekamatwa na walipoomba waende kumtambua walikuta ndiyo anahojiwa muda huo kituoni.CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment