Mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Leodegar Tenga.
MBUNGE wa Viti Maalum, Philipa Mturano (Chadema), amelaani vikali utaratibu wa unaoendelea sasa katika ukusanyaji wa mapato kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi.
Huku akiwa ameshikilia nakala ya gazeti la NIPASHE la toleo la juzi
iliyoonyesha hatari inayoifanya serikali kwa kuchukua fedha zake kwa
malipo taslim na tena bila ulinzi kutoka kwenye ofisi za Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) , mbunge huyo alisema ni vyema sasa kukafanyika
ukaguzi ili kuhakikisha kuwa taratibu zinafuatwa.
Mbunge huyo aliongeza kuwa Manispaa ya Temeke ambayo uwanja huo upo, haijawahi kufaidika na tangu uwanja huo uanzishwe.
“Niliwahi kuwauliza wakurugenzi waliopita na waliopo wakanijibu
kuwa hawapati kitu chochote kutoka kwenye uwanja huo.
Inasikitisha
sana... ninachoomba serikali itueleze na CAG afanye ukaguzi kwa kuwa
hapa pana ufisadi,” alisema.
Alikumbushia tukio la uporaji wa fedha zilizopatikana katika mechi
ya kirafiki kati ya Black Leopards ya Afrika Kusini na Simba
iliyofanyika Desemba 29, 2012 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, na kusema kuwa lazima serikali iongeze umakini katika eneo hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo, Naibu Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, alisema fedha zote
zinazopitia wizarani kwao hupelekwa kwenye mfuko mkuu wa serikali.
"Kwa hiyo fedha hizi zote hupeleka katika mfuko mkuu wa serikali...
kwa hiyo Temeke wanapata kupitia kwenye mfuko mkuu wa serikali,”
alisema.
Makalla aliongeza kuwa kwa takwimu walizonazo, upo uwazi wa mapato
yanayotokana na Uwanja wa Taifa na kwamba, asilimia 15 ambayo serikali
inapata uwanjani na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni
miongoni mwa mapato yanayokwenda katika mfuko mkuu serikalini.
“Mimi sitaki kufanyia kazi habari za magazeti... lakini nataka niseme kwamba kama jambo hilo lipo, sisi serikali tutandelea kulifuatilia,” alisema Makalla,
akiongeza kuwa serikali imejipanga kudhibiti zaidi mapato kwa kubariki
matumizi ya tiketi za elektroniki viwanjani.
Awali katika swali la msingi la mbunge huyo, alitaka kujua serikali
inatoa kauli gani kuhusiana na kutonufaika na mapato kwa halmashauri ya
Temeke?.
Aidha, alitaka kujua tangu uwanja huo uanze kutumika, serikali
imepata kiasi gani na kati ya hayo, Manispaa ya Temeke imepata kiasi
gani?.
Makala alisema Manispaa ya Temeke hunufaika kutokana na mapato
yatokanayo na matumizi ya uwanja huo ambayo huingia kwenye mfuko mkuu wa
Serikali.
"Mapato hayo yote hutumiwa na serikali katika kutoa huduma
mbalimbali kwa wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja na wa Manispaa ya
Temeke,” alisema.
Tangu uwanja wa huo uanze kutumika Agosti, 2007 hadi Februari,
2013, makusanyo ya mapato yanayopitia wizarani ni asilimia 15 ya mapato
baada ya kutoa VAT ambayo ni Sh. bilioni 1.533.
WABUNGE WAPONDA
Wakati huohuo, baadhi ya wabunge wamelalamikia mfumo wa ubebaji wa
fedha za mapato yanayotokana na mechi zinazofanyika kwenye uwanja wa
Taifa mjini Dar es Salaam kwa kuonya kuwa jambo hilo linahatarisha
usalama wa wabebaji na pia fedha hizo.
Akizungumza na NIPASHE jana mjini hapa, Mbunge wa Kinondoni, Idd
Azzan alisema kitendo cha kubeba fedha 'kienyeji' kinahatarisha maisha
ya mbebaji na fedha za umma.
“Hiki si kitendo kizuri kabisa…na ili kuepukana na suala la ubebaji
wa fedha kiholela mimi naona tiketi ziwe zinauzwa wiki moja kabla ya
mechi ili fedha ziwekwe benki,” alisema.
Alisema utaratibu wa sasa wa kugawana mapato baada ya mechi kumalizika muda wa usiku si mzuri na tena ni wa hatari na hivyo, ni bora fedha hizo ziwe zinatunzwa na zigawanywe siku inayofuatwa.
Aliishauri serikali kujenga chumba maalum kwenye uwanja huo kwa
ajili ya kutunza fedha hizo kuliko kuzigawa kwa wahusika baada ya mechi
kumalizika.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema utaratibu wa kubeba fedha kienyeji ni wa hatari na unapaswa kuachwa.
“Kama ni kweli wanabeba mamilioni ya fedha kwenye mifuko, basi
wanahatarisha maisha yao na usalama wa fedha wanazobeba,” alisema
Lusinde.
Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa kuna mianya fulani ya kujenga njia ya kuziiba hizo fedha.
“Inatakiwa kuweka njia za kisasa za kubeba fedha kiusalama zaidi
lakini kubeba fedha kwenye mfuko wa rambo si utaratibu mzuri… maana hata
kama ni za kwao, sidhani kama wanaweza kuzibeba hivyo,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment