RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DK JAKAYA KIKWETE.
SERIKALI mkoani Mbeya imesema ziara ya Rais Jakaya Kikwete haiwezi kuzuiwa na kauli za wanasiasa majukwaani.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alipotoa ufafanuzi wa sababu ya Rais Kikwete kusitisha ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Mbeya.
Awali, ziara ya Rais Kikwete ilipangwa kufanyika ndani ya mkoa kwa siku nne na kuwasili Jum
apili ya Aprili 28, 2013 na badala yake kuahirishwa kutokana na majukumu ya kitaifa ambapo anahudhuria mkutano wa kimataifa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaoendelea Arusha.
Kutokana na shughuli hiyo, Rais Kikwete alilazimika kupunguza siku katika ziara yake aliyoipanga kuifanya na atawasili Mbeya leo kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi.
“Kutokana na ziara hii kupunguzwa siku, basi kumekuwapo na uvumi ya kwamba eti rais anaogopa kauli za wanasiasa, jambo ambalo si la kweli,’’ alisema Kandoro.
Alisema Rais Kikwete ni kiongozi wa kitaifa, hivyo hakuna kitu wala kauli zitakazomfanya kiongozi huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kitaifa ambayo kwa namna moja ndiyo yanayoweza kuleta maendeleo ya mkoa.
“Rais anapowasili anatembelea miradi mbalimbali ambayo imekamilika na kwa ile ambayo haijakamilika ndio mahala uongozi unapoombea fedha, hivyo wakati umefika kwa wana Mbeya kubadilika kimtazamo na kifikra.
“Mkoa wa Mbeya tumekuwa tukiuharibu sisi wenyewe, hivyo ifike mahala tubadilike kwa kuwa maendeleo yataletwa na wana Mbeya wenyewe,’’ alisema Kandoro.
Alisema Mbeya itajengwa na wahusika wenyewe kwa kutambua na kuheshimu utawala wa sheria kwa Serikali na wananchi kuzifuata bila ya kushurutishwa na kwamba maendeleo yataletwa kwa kuunganisha nguvu.
Aidha, aliwataka wakazi wa Mbeya kuepuka kujiingiza katika mazingira ya chuki, vurugu, fitina na majungu, kwa kuwa mara kwa mara yamekuwa yakikwamisha shughuli za maendeleo kufanyika kwa muda muafaka.
Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi Mr II a.k.a Sugu, akituhutubia wananchi moja ya mikutano ya chama chake hivi karibuni.
“HIVI kama wana Mbeya hawamtaki Rais Kikwete kuja Mbeya, mbona mwaka jana aliwasili na kuzindua mradi wa maji wa shilingi bilioni 79 na kupokelewa na maelfu ya wakazi wa mkoa wa Mbeya,” alisema Kandoro.
Hivi karibuni, Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi, aliwataka wakazi wa Mbeya kutokubali ujio wa Rais Kikwete, huku akitoa masharti kwamba endapo atakuja Mbeya basi aje kikazi na si kisiasa.
“Nimesikia Rais Kikwete anakuja Mbeya, kwa ziara ya siku nne, ninamtahadharisha kama anakuja aje kikazi na si kisiasa, la sivyo patachimbika na ninawaombeni wananchi msikubaliane naye,” alisema Mbilinyi. Chanzo http://www.mtanzania.co.tz
0 comments:
Post a Comment