BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAPINDUZI YA ELIMU NCHINI.

JAMBOLEO.
Kawambwa
Waziri wa elimu na ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeleta rasimu mpya ya sera ya elimu nchini kwa wabunge.

Sera hiyo inamtaka mtoto mwenye umri wa miaka mitatu kuanza elimu ya awali na mwenye umri wa miaka minne hadi mitano kuanza darasa la kwanza.

Akitoa mada kwenye semina iliyoandaliwa kwa wabunge kuhusu sera hiyo, Katibu Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Sifuni Mchome, alisema mtoto huyo atasoma hadi darasa la 12 huku akisema lengo ni kubores
ha elimu na kwamba mfumo huo unatarajia kuanza mwaka 2018.

Wakichangia kwenye semina hiyo, baadhi ya wabunge wamepinga mpango huo kwa kusema itakuwa vigumu mtoto mwenye umri wa miaka mitatu  kushika mambo anayofundishwa kwani ni mdogo.  

Mbunge wa Viti Maalumu, Hilda Ngoye ( CCM), alisema mtoto wa miaka mitatu bado ni mdogo kuweza kumudu mambo anayofundishwa shuleni.

Pia alitaka sera hiyo ielezee mafunzo yanayotokewa katika shule binafsi lakini pia alitaka watoto wa shule za msingi wawe na maktaba ambayo wataandaa kuitumia wakiwa wadogo hali itakayowafanya kujijengea utaratibu wa kujisomea tangu wakiwa wadogo.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alisema umri mzuri kwa mtoto kuanza darasa la kwanza ni kuanzia miaka mitano na kusema katika umri huo mtoto anaanza kutamka maneno vizuri.
Pia alitaka kujua sera hiyo inasema nini kuhusiana na shule binafsi nchini na kutaka kurudishwa utaratibu wa kuumba herufi mtoto anapofundishwa kuandika.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu alisema ni vyema sera hiyo ikaweka utaratibu wa namna itakavyotatua changamoto za watoto wa kike ikiwemo kununua taulo za kike za kuwasaidia wanapokuwa katika siku zao.

Alisema kila mwaka watoto 8,000 wanakatisha masomo kila mwaka kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba, lakini pia katika maeneo mbalimbali ikiwemo Njombe Vijijini baadhi ya wasichana wanashindwa kwenda shule kwa muda wa siku saba kutokana na kukosa taulo za kike pindi wanapokuwa kwenye siku zao.

Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM), alitaka kurudishwa kwa ufundishaji wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) huku akisema kuondolewa kwa utaratibu huo kunakosababisha baadhi ya watoto wanaomaliza darasa la saba kutojui kusoma, kuandika wala kuhesabu.

Mbunge wa Igunga, Dk. Dalali Kafumu alizungumzia kuhusu Lugha ya Kiingereza ambapo alisema lugha hiyo ni tatizo hata kwa wanafunzi wengi wa vyuo vikuu nchini.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna changamoto kwa wizara ya kutengeneza utaratibu wa kuhakikisha watu wanajifunza Kiingereza na kutaka lugha hiyo iwe ya kufundishia ili Tanzania iweze kuingia katika ushindani wa soko la ajira hususan katika Jumuia ya Afrika Mashariki.

Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo ( UDP ), alitaka kujua sera hiyo inasema nini kuhusiana na vyuo vya ufundi huku akisema hilo ni eneo muhimu ambalo linafundisha watoto kuweza kujitegemea.

Mbunge wa Karagwe, Dogratius Nyukamazina ( CCM ), alitaka sera hiyo iangalie ubora wa walimu katika shule binafsi huku akisema baadhi ya shule zina walimu kutoka Kenya ambao kimsingi hawana taaluma ya ualimu isipokuwa wanafundisha kwa sababu wanajua Kiingereza.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: