MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe
amefichua siri kuhusu tukio la mlipuko wa bomu lililotokea jusi katika
viwanja vya Soweto, jijini Arusha.
Katika kauli yake jana, Mbowe
ameibua tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, ambapo alidai kuwa askari
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ndiye aliyerusha bomu hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa,baada ya kutembelea majeruhi katika
Hosp
itali ya Selian, Mbowe alisema chama chake kina ushahidi wa kutosha
juu ya askari huyo kurusha bomu.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa
kambi ya upinzani bungeni,alisema wamefanikiwa kupata ushahidi wa
kutosha juu ya tukio hilo baya linalochafua taswira ya nchi.
Alisema chama chake kipo tayari kuweka ushahidi huo hadharani, iwapo Serikali itaendelea kufanya siasa na kuficha ukweli.
“Tunao
ushahidi wa kutosha, ikiwamo wa picha za video unaoonyesha shambulio la
bomu na risasi lilivyofanyika katika mkutano wangu jusi eneo la Soweto.
“Picha
zinaonesha wazi aina ya silaha zilizotumika kwenye shambulio lile ni
tatu, bomu la gurumeti ambalo lilitupwa na askari wa FFU aliyekuwa
kwenye uniform.
“Kutokana na ushahidi huu tulikuwa tumewaeleza
Polisi kama wataendelea kuficha tutaueleza umma na tutaiambia dunia,
kwani aina ya silaha zilizotumika ni SMG na bastola.
“Makasha ya
risasi kama ushahidi wa jambo hili zilizotumika tuliyaokota eneo la
tukio na tayari tumeyarekodi na kuyakabidhi kwa askari waliokuwa
wakichunguza tukio lile,” alisema Mbowe.
Hata hivyo Mbowe
alipinga tamko la Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uratibu na Bunge), William Lukuvi na kusema kauli yake ni ya kitoto
mbele ya jamii.
“Kauli ya Serikali kupitia kwa Lukuvi kwamba
vurugu zilisababishwa na vikundi, wanasiasa na mashirika yasiyo ya
kiserikali ambavyo havijulikani ni sawa na kuwadhihaki Watanzania,”
alisema.
Kutokana na hali hiyo Mbowe alisema tayari wanasheria wa
chama hicho akiwemo Mabere Marando, Tundu Lissu na Profesa Abdallah
Safari wanashughulikia suala hilo.
Alisema baada ya polisi huyo
kurusha bomu, alikimbilia katika gari ya Toyota Land Cruizer yenye rangi
ya bluu akiongozana na askari mwenzake ambapo gari hilo liliondoka kwa
kasi, huku likisindikizwa kwa kukingwa na gari ya TDI hadi kituo cha
polisi.
SPIKA
Alisema anashangazwa na hatua ya Spika wa Bunge Anne
Makinda, kushindwa kuguswa na jambo hilo ambalo limelitikisa taifa na
kuruhusu Bunge liendelee.
Alisema Spika Makinda, ameendelea
kuongoza Bunge licha ya Hotuba ya Waziri Kivuli wa Fedha kuwekwa kando
kutokana na tukio hilo lililovuta hisisa za watu wengi.
“Kila
linapotokea tukio kubwa la mauaji kama haya shughuli za Bunge husimama
ili kulishughulikia, lakini Spika hakushtuka hata pale alipoona wabunge
wote wa Chadema hawapo bungeni.
“Spika Makinda ameshindwa hata
kunipigia simu hata ya kunipa pole kama mbunge niliyenusurika kuuawa ….
Yaani hawajaona sababu sababu ya kufanya hivyo na huenda watu waliokufa
hawana thamani kwao, wameona ni sawa na kuku.
“Jeshi la Polisi,
wamekuwa na kazi ya kuchunguza mambo yasiyoisha, inakuwaje waue wenyewe
halafu wajichunguze? msione misafara ya magari ya viongozi yanakuja hapa
hospitali ni unafiki mtupu.
“Wanawajua wauaji, tutayaweka haya
yote hadharani sura za wauaji zitaonekana na suala hili tutalipigania
mpaka haki itendeke ikibidi hata mpaka umoja wa mataifa,” alisema Mbowe.
Hata
hivyo, aliishauri serikali kwa kuiambia kuwa kama haitaki ushindani wa
vyama vya upinzani ni vema ikavifuta vyama vya siasa vilivyopo kulikoni
kuendelea kuwaua wananchi wasio na hatia wakiwemo watoto wadogo
wanaposhiriki shughuli za siasa.
SHILINGI MILIONI 100
Katika hatua nyingine, Serikali imeamua
kutenga Sh milioni 100 kama zawadi kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa
zitakazofanikisha kunaswa kwa mhalifu au watu wenye mtandao wa ulipuaji
mabomu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na
Bunge, William Lukuvi, alisema bungeni mjini hapa jana, kuwa kila mtu
mmoja atakayetoa taarifa za siri na za uhakika kufanikisha kukamatwa kwa
mhalifu huyo, atapatiwa Sh milioni 10 “hadi fedha hizo ziishe na
serikali ina uwezo wa kuongeza fedha zaidi hadi mtu huyo apatikane.”
Lukuvi,alikuwa
akitoa kauli ya Serikali kuhusu mlipuko uliotokea katika mkutano wa
hadhara wa kampeni za uchaguzi katika Kata ya Sowote, Arusha, Jumamosi
iliyopita. Mkutano huo, ulikuwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Alisema mtu yeyote atakayetoa taarifa hizo atahakikishiwa usalama wake na polisi.
Alisema
watu wawili walikufa katika tukio hilo, ambao ni Judith William (48) na
Ramadhani Juma (15), huku watu 70 wakijeruhiwa, watatu vibaya na kati
yao wawili hali zao ni mbaya.
Alisema uchunguzi wa awali,
umeonyesha mlipuko huo ulikuwa wa bomu la kurushwa kwa mkono,
lililorushwa kutoka upande wa mashariki kuelekea magharibi, kulikokuwa
na gari aina Fuso lililokuwa likitumika kuhutubia.
“Jaribio la
polisi kutaka kumfuata aliyerusha bomu hilo lilizuiliwa na makundi ya
wananchi, ambao walianza kuwashambulia polisi kwa mawe na kuwazomea na
hivyo polisi kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka mhalifu huo.
“Aina
ya urushaji wa bomu hilo, hautofautiani na mbinu iliyotumika kwenye
shambulio jingine la bomu lililotokea Mei 5, mwaka huu, katika Kanisa
Katoliki la Olasiti katika jiji hilo hilo la Arusha,” alisema.
“Nataka
niwaambie wahalifu hao kuwa njama zao za kutugawa kwa misingi ya dini,
makabila, rangi, rasilimali na itikadi za vyama zitashindwa.
“Tutapambana
nao usiku na mchana kwa silaha zote tulizonazo mpaka tutakapowashinda
na kuwafikisha mbele ya mikono ya sheria,” alisema.
MBATIA
Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD), James Mbatia, ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka
kukabiliana na hali ya uvunjifu wa amani iliyopo nchini.
Mbatia alitoa taarifa hiyo mjini Dodoma jana, wakati akizungumzia tukio la bomu lililotokea mkoani Arusha.
Alisema imekuwa kawaida ya Serikali yanapotokea matukio ya mauaji kama ya Arusha, kutoa majibu mepesi.
"Zamani ilikuwa nadra kutokea kwa matukio ya kuuana wenyewe kwa wenyewe, sasa imekuwa kama utamaduni.
“Hii
inatokana na wenye mamlaka kutoa majibu mepesi ambayo hayana
utekelezaji, tunapaswa kusema na kutenda, vinginevyo nchi inaelekea
kubaya," alisema Mbatia.
“Kuanzia matukio ya Mtwara na matukio ya mabomu Arusha, kauli zinazotolewa na Serikali ni za kubabaisha.
Taarifa hii, imeandaliwa na Bakari Kimwanga (Dar), Revocatus Makaranga na Debora Sanja (Dodoma).
CHANZA MTANZANIA
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment