Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Tamko hilo, ambalo ni azimio la nne kati ya 20 yaliyopitishwa na
Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa, lilisomwa na Mwenyekiti wa chama
hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alipozungumza na waandishi wa habari,
jijini Dar es Salaam juzi.
Alisema Baraza Kuu limefikia azimio hilo kwa madai kwamba Pinda ndiye chanzo kikuu cha udhalilishaji na mauaji hayo.
“Kauli yake ya ‘piga tu, tumechoka’ aliyoitoa ndani ya Bunge
imehamasisha unyanyasaji wa wananchi unaofanywa na vyombo vya dola. Kwa
hivyo, Waziri Mkuu anapaswa kujiuzulu kwa matukio haya. La sivyo, Rais
amfukuze kazi,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema Baraza Kuu linapongeza Bunge kwa kukubaliana na
mapendekezo yaliyotolewa na kamati ndogo ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge
wa Kahama (CCM), James Lembeli na kusababisha mawaziri watatu kuvuliwa
nyadhifa zao na mmoja kujiuzulu mwenyewe.
Hao ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Dk. David
Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa-JKT) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na
Utalii).
“Kamati hii imetoa mapendekezo mazuri juu ya uhalifu na unyanyasaji waliofanyiwa wananchi,” alisema Profesa Lipumba.
WAHUSIKA WAFIKISHWE MAHAKAMANI
Alisema Baraza Kuu linaitaka pia serikali kuwachukuliwa hatua za
kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wale wote
waliohusika na uvunjwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi
wakati wa operesheni hiyo.
WAATHIRIKA WALIPWE FIDIA
Alisema pia linaitaka serikali kutazama utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi wote walioathirika na vitendo hivyo.
DK. SHEIN AMUIGE JK
Pia linamtaka Rais wa Zanzibar, Dk. Shein kuiga mfano wa Rais
Kikwete katika kushughulikia kero zinazoibuliwa na vikao vya Baraza la
Wawakilishi kwa kuwawajibisha mawaziri wanaohusika.
Alisema hiyo ni kama ambavyo Rais Kikwete amekuwa akifanya katika kuunga mkono hoja zinazoibuliwa na bungeni.
SERIKALI ISITUMIE JWTZ
Alisema Baraza Kuu pia linaitaka serikali kutolitumia Jeshi la
Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kushughulikia masuala ya
uvunjifu wa sheria katika maeneo mbalimbali ya nchi, badala yake kazi
hiyo ifanywe na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuongezewa uwezo wa kutimiza majukumu yake huku likiheshimu haki za kisheria za watuhumiwa.
“Jeshi la Wananchi liachiwe majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi
yetu. CUF inaona kwamba si vyema kulitumia Jeshi letu la kulinda mipaka
ya nchi katika operesheni zinazohusu uvunjaji wa sheria unaofanywa na
wananchi,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza: “Askari wa JWTZ hawana mafunzo ya kukamata mwananchi mwenye tuhuma za uhalifu bila kuvunja haki zake za kisheria.”
MUUNDO WA MUUNGANO, MCHAKATO WA KATIBA
Alisema Baraza Kuu linaitaka serikali kusimamia kikamilifu mchakato
wa katiba mpya ili ipatikane kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,
kwani wananchi hawatakubali kuingia kwenye uchaguzi huo kwa kutumia
katiba ya sasa, ambayo imekataliwa na Watanzania wengi waliotoa maoni
kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA
Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu linamshauri Rais Kikwete kuunda
serikali ya umoja wa kitaifa ili kusaidia kupatikana kwa katiba mpya
katika kipindi hiki cha mpito.
Alisema uwapo wa serikali hiyo utarahisisha mjadala wa Bunge
Maalumu la Katiba na kulifanya kuchukua sura ya kitaifa zaidi na hivyo
kurahisisha upatikanaji wa katiba taifa kwa misingi ya utashi wa
wananchi.
Profesa Lipumba alisema serikali ya umoja wa kitaifa itampa fursa
rais kuteua Baraza la Mawaziri lililo imara na kuondokana na mawaziri
wanaoonekana ni mizigo ili ashughulikie matatizo mazito yanayolikabili
taifa, ikiwamo ongezeko la gharama za maisha, ukosefu wa ajira,
kuporomoka kwa elimu, huduma hafifu za afya na maji safi na salama na
ukosefu wa umeme wa uhakika.
DAFTARI LA WAPIGAKURA
Alisema Baraza Kuu limesikitishwa na Daftari la Kudumu la Wapigakura kutoboreshwa tangu kumalizika uchaguzi wa 2010.
DAFTARI LA ZANZIBAR
Alisema pia kuwa Baraza Kuu linaitaka serikali ya Zanzibar kutoa
vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi (Zan ID) na kuandikisha wananchi
waliofikisha umri wa miaka 18 katika daftari la wapigakura.
Pia alivitaka vyama vyenye wabunge kuacha kupigania maslahi ya vyama vyao wakati wa mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment