RASILIMALI ZA NCHI ZIKIWEMO GESI, MAFUTA NA PEMBE ZA NDOVU ZAANZA KUONYESHA DALILI ZA KUIGAWA TANZANIA.
WATANZANIA wametakiwa kuwa makini na mali na rasilimali za nchi, ikiwemo gesi, mafuta, pembe za ndovu na dhahabu kwani zimeanza kuonesha dalili za kugawa Taifa.
Akizungumza katika Ibada ya Siku Kuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Jimbo la Geita, na kutangazwa moja kwa moja kwenye televisheni, Askofu Damian Dallu alitaka Watanzania ili kuondokana na tatizo hilo, wawe makini kumwomba Mungu.
Alisema siku zote palipo na mali pamekosa furaha ya kweli, kwa wananchi na kutolea mfano nchi kadhaa zenye utajiri wa mafuta duniani ambazo pamoja na utajiri huo, bado mataifa hayo yamekuwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
“Palipo na mali hapana furaha, hata hapa Geita pana dhahabu je, kuna furaha? Pamoja na kuwapo dhahabu kila siku kuna malalamiko, palipo na utajiri hapatoshi. “Hata kama kutakuwa na taarifa zisizo za kweli, kuwa sehemu fulani ina mafuta basi inakuwa shida, na hata hapa kwenye kanisa hili wakisema kuna dhahabu kila mtu na baadhi yenu mliomo humu kila mmoja atataka kujaribu kuchimba. Mali haitoshi kuleta furaha, itawatenga na kuvunja Muungano,” alisema.
Dallu alisema kutokana na mali na watu walio madarakani kutetea mali zaidi, wamekuwa chanzo cha kuchafua hali ya hewa ya furaha.
Alisema hata hewa ambayo ni furaha ambayo Mungu amewapa Watanzania, imekuwa ikichafuliwa na wanaotafuta mali na hata mazingira ikiwamo misitu inayokatwa, imekuwa ikiharibiwa na wanaotafuta mali.
Alisema mali na rasilimali zilizopo zinaonekana kuanza kugawa Watanzania kati ya matajiri na masikini, walio madarakani na watawaliwa.
Zanzibar
“Kuna wakati ilisemekana yamegundulika mafuta, upande mmoja wa Muungano ukasema mafuta si ya Muungano, gesi imepatikana Mtwara watu wanasema haitoki, haitoki ni yetu,” alisema.
Alikumbusha kuwa kabla ya kugundulika kwa mali hizo, Watanzania walikuwa wenye furaha licha ya kuwa masikini, lakini leo ile furaha waliyokuwa nayo haionekani.
Askofu Dallu pia alikemea tabia ya watu kuvuna maliasili za nchi kiholela, ikiwa ni pamoja na kuua tembo kwa lengo la kutaka kupata utajiri.
“Mtu anaua tembo na kukata pembe eti anataka kujikomboa na kupata utajiri, hiyo ni furaha ya kifo ambayo kamwe haitadumu kwa muda mrefu. “Hata hawa wanaoitwa majambazi, wanavamia kwa tajiri na cha kwanza wanamwua ndipo wanaiba, hawa ni wapumbavu. Walipaswa kuchukua mali na kumwacha tajiri akiwa hai, kwa kuwa huyu ana akili ya kuzalisha mali nyingine, ili waweze kurudi tena siku nyingine,” alisema.
Pia Dallu aliomba Watanzania kuliombea Taifa ili liepukane na changamoto na kuleta furaha ya kweli na si kutumia njia ya mkato kutafuta furaha ya muda mfupi ambayo inajenga chuki.
Operesheni Tokomeza
Katika ibada ya mkesha iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Dar es Salaam juzi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Titus Mdoe alikemea ukatili uliojitokeza wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Alisema yaliyofanywa wakati wa operesheni hiyo hayakuwa sahihi kwa kufanyia ukatili binadamu na kuwa hayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.
“Inasikitisha matendo ambayo yanaendelea sasa, tumekuwa tunasikia kwenye redio, malalamiko bungeni ya watu kutendea binadamu unyama. “Wewe ni mlinzi na umeapa, lakini unashiriki kutesa binadamu mwenzako, unamkata masikio, vidole kwa lengo la kutafuta ukweli unaoutaka na unamdhalilisha mbele ya watoto. Haya hayafai ni lazima tusali.”
Mdoe alisema pamoja na muda mrefu kuwapo vitendo vya ukatili vinavyoendelea nchini, lakini hakuna hatua inayochukuliwa na kutaka walioshiriki kutubu kwa Mungu.
“Watu wamekuwa wakisikia kutokea matendo mabaya kwenye redio na kwenye magazeti … wanaishia kufunika tu, mwisho wake nini kitatokea? Amani itapatikana wapi tukiingia katika mambo haya?” Alihoji na kutaka Watanzania kukataa ubaya na kuishi wakiwa wema.
Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis akisherehekea Krismasi ya kwanza tangu achaguliwe kuongoza Kanisa hilo lenye wafuasi bilioni 1.2, ametaka watu kuachana na ujivuni na uchoyo na kujitolea nyoyo zao kwa Mungu na binadamu.
Francis, ambaye Machi alikuwa Papa wa kwanza asiyetoka Ulaya baada ya miaka 1300, aliendesha Misa ya Mkesha kwa watu 10,000 katika viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro huku mamia wengine wakifuatilia kwenye skrini kubwa nje ya viwanja hivyo.
Kengele kubwa za kanisa hilo, ambazo zilipigwa siku alipotangazwa kuchaguliwa Machi 13, zililia wakati kwaya ya kanisa dogo la Sistine ilipoimba Gloria, maombi ambayo huanza na maneno ya Biblia, yasemayo malaika waliimba usiku ambao Yesu alizaliwa Bethlehem.
Francis alitoa mahubiri mafupi ambayo yalikuwa rahisi kama vazi lake jeupe akisema mtu anaweza kuchagua kati ya giza na mwanga.
“Kwa upande wa watu kuna wakati wa mwanga na giza, uaminifu na uhalifu, utii na uasi; wakati wa kuwa mahujaji na wakati wa kuwa watu wa ovyo ovyo tu,” alisema akizungumza Kitaliano.
“Katika historia yetu pia, kuna nyakati za nuru na giza, mwanga na kivuli. Kama tunampenda Mungu na kaka na dada zetu, tunatembea katika nuru; lakini kama nyoyo zetu zimefungwa, kama tunatawaliwa na ujivuni, ulaghai, uchoyo, basi giza litatushukia na kutuzingira,” alisema.
Francis ambaye aliendesha misa hiyo pamoja na zaidi ya makadinali, maaskofu na wachungaji 300, alitaka watu kuacha kuogopa kumfikia Mungu.
“Msiogope! Baba yetu ni mvumilivu, anatupenda, ametupa Yesu kutulinda katika njia ambayo inatuongoza kufika kwenye nchi ya ahadi. Yesu ni mwanga ambao unamulika giza. Ndiye amani yetu,” alisema.
Mahujaji walitoka sehemu zote duniani kuhudhuria misa hiyo na baadhi wakasema ni kutokana na kwamba Francis amewaletea pumzi safi kwenye Kanisa. HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment