Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa, ametoa kauli hiyo
siku moja tu baada ya gazeti hili kuripoti kuwa Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Kiteto, Mainge Lemalali, amemshitaki kwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kuwa anachochea mgogoro wa wakulima na wafugaji, Kiteto.
“Ni aibu kubwa, kama mimi ningekuwa mbunge wa huko,
ningeshajiuzulu,” alisema Ndugai na kuongeza kuwa mauaji yanayotokea
Kiteto yanazidi yaliyotokea katika Operesheni Tokomeza Ujangili
iliyosababisha mawaziri wanne kujiuzulu nyadhifa zao.
Alisema kati ya watu 15 waliofariki katika mapigano wilayani humo,
sita wamepokelewa na kuzikwa katika jimbo lake Kongwa na kusisitiza kuwa
wamechoshwa kupokea maiti na suala hilo hawezi kulinyamazia kwa sababu
linamhusu.
Akiongea kwa njia ya simu, Ndugai alisema mgogoro wa Kiteto
umedumu zaidi ya miaka 10 sasa na madhara yake wanayoyapata ni majirani
likiwamo jimbo lake.
“Nisingeweza kueleweka nikiwa kama kiongozi ninapoona madhara
yanatokea halafu ninyamaze…wanaposema mimi naingilia kati nawashangaa
sana,” alisema.
Alisema unapochaguliwa kuwa mbunge maana yake wewe ni mbunge wa kitaifa unawakilisha wananchi wote.
Ndugai, alisema baada ya kuingilia kati mgogoro huo ndipo Mashirika
yasiyo ya kiserikali, Taasisi za Kijamii, Haki za binadamu, NGOs na
Serikali, yaliamua kujitokeza na kwenda kujionea. “Kama nisingesema mimi
hali ile ingeendelea.”
Aliwashutumu viongozi wa Kiteto akiwamo Mwenyekiti na Mkuu wa
Wilaya ya Kiteto ambao alidai kuwa ni wenyeji wa huko, kukusanya fedha
nyingi kutoka kwa wafugaji kwa ajili ya kuwafukuza watu aliowaita
waswahili kwa lengo la kutenga eneo moja la wafugaji.
“Fedha hizo ziko wapi?..Zimelipwa nani?...Wao ni wachochezi wakubwa
wa kikabila,” alisema na kufananisha mauaji hayo ni sawa na yale
yaliyotokea Rwanda.
Alisisitiza kuwa tatizo la Kiteto linasababishwa na wakubwa ambao ndio wanaopanga matumizi ya ardhi.
Ndugai alisema anamshukuru Waziri Mkuu kwa kwenda huko kwa
helikopta ambapo ameshuhudia eneo hilo ni mashamba wala sio hifadhi kama
inavyodaiwa.
Alisema Waziri Mkuu baada ya kujionea hali halisi aliagiza
waathirika wapewe msaada wa chakula, mahema na matibabu, “wao kama
viongozi walitakiwa kuchukua hatua za haraka badala ya kumsubiri waziri
mkuu aje na kutoa agizo,” alisema.
“Wanachotakiwa hawa viongozi ni kujiuzulu…kwa nini mauaji
yanatokea Kiteto? Kwa nini wasiwajibishwe, wanamlaumu Ndugai?”Alihoji na
kusisitiza kuwa mauaji ya Kiteto ni ya kikabila. CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment