BUNGE LA KATIBA LIMEVUGWA, MWENYEKITI ALAZIMIKA KUVUNJA DAKIKA TANO TU BAADA YA KUANZA.
KIKAO cha Bunge Maalumu la Katiba kimelazimika kuvunjika dakika tano baada ya kuanza, kutokana na vurugu za baadhi ya wajumbe waliokuwa wakimshutumu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuvunja Kanuni za Bunge hilo. Vurugu hizo zilisababishwa na wajumbe wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoka vyama vya siasa vya upinzani isipokuwa TLP.
Wajumbe hao walikuwa wakipinga Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba kabla ya Bunge hilo kufunguliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Hali ilianza kuvurugika mara tu baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kumwita Jaji Warioba atoe hotuba yake.
Mabavu
Wakati anatoa tangazo hilo, wabunge kadhaa walisimama kuomba mwongozo wa Mwenyekiti, akiwemo Andrew Chenge na Profesa Ibrahim Lipumba, lakini Sitta aliwakatalia wabunge hao kuwa hakukuwa na mwongozo wa Mwenyekiti kwa wakati huo.
“Mwenyekiti nakuomba uje utoe hotuba yako,” alisema Sitta lakini wajumbe wengi kutoka vyama mbalimbali vya siasa vya upinzani, walisimama kumpinga Sitta, huku wakigonga meza na kumtupia maneno Sitta ya kumtaka afuate Kanuni.
Kitendo cha Sitta kutowasikiliza, kilisababisha wajumbe wote wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kusimama akiwemo Christopher Mtikila, Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe, Zitto Kabwe na James Mbatia.
Tundu Lissu alisikika akisema: “Fuata Kanuni, si hutaki kufuata Kanuni hatukai.” Alisikika mjumbe huyo ambaye tangu Ijumaa alimpinga Sitta kwa hatua yake ya kutaka Jaji Warioba awasilishe rasimu hiyo kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua Bunge hilo.
Hatua hiyo ya Sitta, ni kinyume na Kanuni ya 7(1)(h) ya Bunge inayotamka kuwa rasimu ya Katiba mpya, itawasilishwa baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano au Rais wa Zanzibar, kulihutubia Bunge hilo.
Warioba aduwaa
Licha ya wajumbe hao kugoma kukaa, Sitta alisisitiza Warioba aende akatoe hotuba na Jaji Warioba alipoenda mbele kwa ajili ya kutoa hotuba yake, alipigiwa kelele na wajumbe hao na kumfanya Jaji Warioba kusimama kwenye kipaza sauti bila kufanya lolote.
Kelele hizo za kanuni, mwongozo wa Mwenyekiti zilipozidi huku Warioba akiwa amesimama kwenye kipaza sauti mbele ya wajumbe hao, baada ya dakika tano kupita Warioba alikusanya nyaraka zake na alirudi kukaa kwenye sehemu yake.
Baada ya Warioba kurudi kwenye sehemu yake na kukaa, Sitta alilazimika kutangaza kuahirisha Bunge hilo hadi hapo watakapotangaziwa vinginevyo baadaye.
“Kwa hali hii waheshimiwa wajumbe, hatuwezi kuendelea mbele nalisitisha Bunge hili hadi hapo baadaye,” alisema Sitta na kunyanyuka kwenye kiti chake za enzi.
Walinzi, Pole
Mara baada ya kusitishwa kwa kikao hicho, Jaji Warioba na Makamu wake Jaji mstaafu Augustine Ramadhani, ambao walikuwa ndani ya ukumbi wa Bunge, waliondolewa ukumbini humo na walinzi wao wakisindikizwa na askari wa Bunge.
Saa 11.10 jioni, Sitta alipita kwenye ukumbi wa waandishi wa habari, akaelekea kwenye chumba cha mikutano kilichoko ndani ya jengo la Bunge na kupewa pole na waandishi wa habari.
“Pole Mwenyekiti...” aliambiwa na waandishi wa habari naye akajibu “ndio demokrasia hiyo,” na baada ya hapo aliingia kwenye chumba cha mikutano na kufuatwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho.
Pia walionekana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Katibu wa Bunge, Yahya Khamis Hamad na Naibu wake, Dk Thomas Kashililah na Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema wakimfuata.
Mashati
Wakati shughuli zikiwa zimesitishwa, ndani ya ukumbi hali haikuwa tulivu, kwani baadhi ya wajumbe walionekana kutaka kushikana mashati na wengine wakizozana hadharani.
Miongoni mwao aliyeonekana kuwaambia wajumbe waliosimama kupinga Warioba kuwasilisha rasimu hawana akili kwa kuonesha ishara, ni Ave-Maria Semakafu, hali iliyosababisha arushiane maneno na wajumbe hao na kuondolewa na Celina Kombani.
Baadaye alikwenda kwenye kikundi kilichomzunguka Lipumba, nako alionekana kubishana kana kwamba anataka kupigana na kumfanya Muhamed Seif Khatib kumuondoa.
Mikusanyiko ya vikundi vya watu vilitawala ndani ya ukumbi huo wakijadli sintofahamu iliyotokea ndani ya ukumbi huo.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuonekana Sitta na Kificho wakiondoka kutoka kwenye chumba cha mkutano, Katibu wa Bunge, Yahya aliwatangazia wajumbe waondoke hadi hapo watakapotangaziwa siku ya kuendelea na Bunge.
Tangazo hilo lilionekana kutoeleweka, ambapo wajumbe walihoji lini na waondoke kwenye ukumbi wa Bunge wasubiri nje au warudi makwao, lakini Katibu huyo akasisitiza “ninachozungumza ni Kiswahili, ondokeni hadi hapo tutakapowatangazia”.
Maoni
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wajumbe wa Bunge Maalumu, Beatrice Shelukindo alishauri Rais Kikwete avunje Bunge hilo kwani kilichofanyika jana ni uhuni wa wanasiasa.
Alisema wajumbe ambao wanashinikiza Rais aje kwanza alihutubie Bunge hilo ndipo Warioba awasilishe rasimu, hawana msingi na wanaofanya hivyo hawana nia njema na nchi hii.
“Kwa nini walazimishe Rais aje hapa kuhutubia wakati hayupo? Mimi nashauri Rais alivunje Bunge hili maana hakuna tunachokifanya hapa cha maana,” alisema Shelukindo.
Alisema wajumbe hao wanatumbua pesa za walipa kodi lakini wameshindwa kuendelea mbele kwa sababu tu ya malumbano ya kisiasa na akaonya kuwa kwa hali ilivyo inaweza isipatikane katiba nzuri.
Moses Machali kwa upande wake alisema kwamba Sitta alivunja Kanuni makusudi bila kushirikisha pande zote zinazounda Bunge hilo na licha ya kumwandikia barua kumwomba akutane nao aliwakwepa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment