DODOMA/IRINGA.
Ofisi ya Bunge Maalumu la Katiba imesema kuwa Mbunge Mteule wa Kalenga, Godfrey Mgimwa ataweza kushiriki katika vikao hivyo ikiwa Rais Jakaya Kikwete atawapa barua ya uteuzi wake.
Ofisi ya Bunge Maalumu la Katiba imesema kuwa Mbunge Mteule wa Kalenga, Godfrey Mgimwa ataweza kushiriki katika vikao hivyo ikiwa Rais Jakaya Kikwete atawapa barua ya uteuzi wake.
Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Maandalizi ya Bunge
Maalumu la Katiba, John Joel alisema hayo jana wakati akizungumza na
gazeti hili kuhusu uwezekano wa Mgimwa kuhudhuria vikao kama Mjumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba.
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ni sehemu ya Wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea na vikao vyake vya kupitia
Rasimu ya Pili ya Katiba mjini Dodoma.
“Mimi simpokei hapa isipokuwa kwa barua ya uteuzi kutoka kwa Rais,” alisema Joel.
Kwa mujibu wa Joel, baada ya Mgimwa kuchaguliwa
hatalazimika kuapa kwanza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ili aingie kwenye Bunge la Katiba, bali atatakiwa kuteuliwa tu
na Rais Kikwete.
“Uteuzi wake huo utatangazwa kwenye Gazeti la
Serikali na yeye ataruhusiwa kuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba baada ya
sisi kupata barua ya uteuzi huo kutoka kwa Rais,” alisema.
Alisema hata wabunge na wawakilishi waliingia katika Bunge hilo baada ya kuteuliwa na Rais kuwa wajumbe.
Katika hatua nyingine, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo
la Kalenga Pudenciana Kisaka juzi alimtangaza Mgimwa kuwa mshindi wa
kiti cha ubunge wa jimbo hilo.
Mgimwa ametangazwa mshindi katika uchaguzi huo
uliolenga kuziba pengo lililoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo
hilo, marehemu William Mgimwa baada ya kuwashinda Grace Tendega wa
Chadema na Richard Minja wa Chausta.
Mgombea ubunge kupitia Chadema, Grace Tendega
amekubaliana na matokea hayo akidai watu wa Kalenga wamemchagua mbunge
waliomtaka na kuongeza kuwa kazi ya kuwaletea ukombozi watu hao bado
inaendelea.
Pudenciana alimtaja Mgimwa wa CCM kuwa mshindi
baada ya kupata kura 22,962 sawa na asilimia 79.32, huku mshindani wake
wa karibu, Grace wa Chadema akipata kura 5,853 sawa na asilimia 20.22 na
Richard Minja wa chausta akipata kura 150 sawa na asimilia 0.52.
Katika uchaguzi huo, jumla ya wapigakura
waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura la mwaka 2010 ni
71,965 idadi ya waliojitokeza kupiga kura ikiwa ni 29,541.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment