Katika Sehemu ya pili hii ndiyo sehemu ya mwisho ya makala haya tukiachia wananchi wa Mbangayao wakieleza namna walivyoishi kihalali tuendelee.........
Kwa mujibu wa miktasali mbalimbali kijiji hicho cha Mbangayao wananchi wao
wanaishi kihalali kwani eneo hilo kutokana na kijiji kutambulika na serikali
kwa kusajiliwa toka mwaka 1954 baada ya gavana aliyetambulika kwa jina la
Robert De Stapeldon kugundua eneo hilo kuwa ni msitu wa hifadhi na kuchukua
ekari 1904 za msitu wa hifadhi na kuacha vitongoji vya Lupanga na Mbangayao.
Vuguvugu za wananchi kuwataka kuondoka katika hifadhi hiyo zilianza
mwaka 1991 ambapo serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii wakala wa
huduma za misitu nchini walipeleka pendekezo kwa waziri husika kuwa kijiji
chote cha Mbangayao ni hifadhi ambacho kinahusu vitongoji vyote viwili vya
Lupanga na Mbangayao.
Serikali ilitangaza katika gazeti la serikali namba 154 la Mei 17 1991
na kuchukua hekta zote 2245 hata hivyo zoezi hilo halikufanyika hadi mwezi Mei
mwaka jana lilipoanza tena baada ya mkuu wa wilaya ya Ulanga kwenda kwenye
kijiji cha Mbangayao na wataalamu wa misitu na kusema kuwa kijiji hicho kipo
katika eneo la hifadhi.
Katika barua yake ya Oktoba 5 mwaka 2013 yenye
kumb.Na.DFM/UL/MZ/FR/VOL.2/18 kwa wananchi wa vitongoji vya Lupanga na Mbangayao,
Mkuu wa wilaya ya Ulanga Francis Miti aliwataka wananchi hao kuondoka ndani ya
msitu wa hifadhi Mzelezi kuanzia Oktoba 5, 2013 hadi Novemba 4, 2013 na kutoa
ilani kuwa wananchi wote wa eneo hilo watoke ndani ya muda waliopewa.
Barua hiyo iliendelea kusema kuwa wale wote watakaokaidi ilani hiyo
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufikishwa
mahakamani huku ikieleza kuwa kuishi ndani ya hifadhi haikubaliki kisheria na
baada ya tarehe hiyo nyumba zote za eneo hilo zitabomolewa chini ya usimamizi
wa vyombo vya usalama.
Kijiji cha Mbangayao katika mikutano mbalimbali kwa serikali kabla ya
zoezi hilo ilipendekeza mapendekezo ya msingi kabla ya kuhamishiwa kitongoji
cha Isaka, kwanza kutengenezewa barabara na viongozi wa serikali wakakagua
maeneo ya kupita, wajengewe zahanati na shule na wapatiwe majisafi na salama ya
bomba na kulipwa walipwa fidia ya uharibifu wa mali zao na kama hayo
yakitekelezwa wananchi watachangia nguvu kazi ili kujenga zahanati na
shule na kulinda msitu wa hifadhi wa Mzelezi.
Serikali ya kijiji cha Mbangayao iliiomba serikali ya wilaya ya Ulanga
isitumie nguvu katika kuwaamisha wananchi wake na kijiji kitambulike hata
wakiama na kwa upande wa muhtasari wa mkutano mkuu wa kijiji wao waliunga mkono
maombi ya serikali ya kijiji kwa serikali ila waliongezea kuwa msitu waliutunza
wenyewe hivyo kuiomba serikali iangalie uwezekano wa kulipa gharama za ulinzi
toka mwaka 1954 hadi walipoama.
“Kuitwa jina la wavamizi kwa wanakijiji wale sio zuri na linapaswa
kupingwa kwani wao ni wananchi halali wa kijiji hicho na operesheni
iliyowahamisha katika kijiji hicho ni ya vijiji vya ujamaa na si ya msitu hivyo
kuiomba serikali iwapatie mtaalamu wa kuthamini mali zao kisha walipwe na pia
mtaalamu huyo awapimie maeneo huko Isaka”. Alisema barua.
Aliongeza kwa kusema kuwa ameshangazwa na serikali kupuuza maombi ya
wananchi hao na kuamua kuvunja nyumba zao kisha kuwaamisha kwa nguvu bila
kuwalipa fidia na pia kutowaandalia miundombinu mipya katika makazi yao mapya
huku wananchi hao wakiishi maisha kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Baada ya Diwani wa kata ya Isonga, Henry Prosper
Barua kuelezaa katika baraza la madiwani, halmashauri hiyo iliunda tume ya
kuona hali halisi ya wananchi wa kijiji cha Mbangayao waliohamia kitongoji cha
Isaka ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Severus Kamguna na yenyewe kujione hali ya
maisha ya wananchi katika kitongoji cha Isaka.
Kamguna alidokeza kidogo mambo muhimu na kumweleza mwandishi kuwa ripoti
kamili ya uchunguzi wa tume itatolewa katika kikao cha baraza cha madiwani
kitakachoitishwa lakini hakusikita kuimegea mambo muhimu tume iliyoyabaini.
MWALIMU MKUU WA SHULE YA MSINGI MBANGAYAO, DAVID EPONDA AKIFUNDISHA MASOMO.
“Ni kweli tume ilienda kitongoji cha Isaka januari 31 mwaka huu na kuona
wananchi kutoka kaya mbalimba wakiishi na wakilala katika mapango na watu 19
mpaka sasa bado wanaendelea kuishi katika mapango hayo lakini licha ya kugundua
ukweli huo tume yangu pia ilifanya kazi ya kuchunguza mambo mengine muhimu kama
tulivyoagizwa. Alisema Kamguna.
Lengo kuu la tume ni kutekeleza agizo la baraza la madiwani la kutaka
iundwe tume ndogo kwenda kuthibitisha yaliyosemwa na Diwani wa kata ya Isongo
katika kikao cha baraza la madiwani cha januari 27, mwaka 2014 kuona hali
halisi ya wananchi wa kijiji cha Mbangayao waliohamia kitongoji cha Isaka na
kutoa mapendekezo kwa baraza la madiwani.
Tume hiyo ililenga kuangalia hali halisi ya afya, elimu, makazi, hifadhi
yam situ wa Mzelezi, miundombinu ya barabara na kuhama kwa wananchi wa
Mbangayao na Lupanga kwenda kitongoji cha Isaka kuwa wananchi hao wanalala
katika mapango na kitongoji cha Kitonga.
“Nimekueleza mambo machache kwa sababu umeniuliza na mimi ndiye
Mwenyekiti wa Tume yetu mambo mengine tume yetu itaeleza mbele ya baraza la
madiwani hivi karibu lakini ulichoona wewe kule kitongoji cha Isaka hakina
tofauti sana ndugu mwandishi, wewe subiri utaona kazi ya tume yetu”. Alisema
Kamguna na hakutaka kuendelea kuelezea.
Mkuu wa wilaya ya Ulanga mkoa wa Morogoro, Francis Miti akitolea ufafanuzi
wa suala hilo ofisini kwake na mwandishi wetu alisema kuwa ni kweli kuna kaya
177 zimehamishwa katika kijiji cha Mbangayao kwa sababu wanalikuwa wakiishi
katika hifadhi ya msitu wa asili wa Mzelezi kinyume na sheria.
Miti alisema kuwa kuhamishwa kwa wanakijiji hao wa Mbangayao
kulizingatia matakwa yote ya kisheria na notisi ya kwanza ilitolewa mwaka 1954
lakini katika serikali yake ilichofanya ni kutekelezaji agizo la notisi hiyo na
sio vinginevyo.
Kijiji cha Mbangayao na kitongoji cha Lupanga vipo katikati ya hifadhi
na mchakato wa kuwahamisha wananchi hao ulianza tangu mwaka 1954 ambapo
serikali ilitoa tangazo (GN) la kuwahamisha katika eneo la hifadhi.
Tangazo namba 216 (GN) agizo liliwataka wananchi wote waliokuwa katika
eneo la hifadhi waondoke katika hekta 762 ikiwa ni kitongoji cha Mbangayao na
Lupanga na mwaka 1980 serikali ilituma wataalam kuangalia namna ya hifadhi yam
situ wa Mbangayao na kuupima msitu na kuainisha hekta za msitu kuwa 2245 ambazo
serikali ilitoa tangazo namba 154 mwaka 1991 (GN) na kuianisha mipaka yote ya
hifadhi hekta 2245. Alisema Miti.
Mwaka 1975 katika operesheni hamisha vijiji, serikali ilitoa tangazo kwa
wananchi wote waliokuwa wakiishi ndani ya hifadhi kuondoka na kwenda Mzelezi
vikivikumba vitongoji vya Isongo, Lupanga na Mbangayao lakini baadaye wananchi
hao walianza kujereje katika hifadhi kinyemela (kijiji cha Mbangayao) hilo
ikiwa ni kukiuka seria ya misitu, sheria namba 14 ibara ya 26 ya mwaka 2002
inayozuia shughuli za kibinadamu kufanyika ndani ya eneo la misitu. Alifafanua
mkuu huyo wa wilaya.
Miti aliongeza kwa kusema kuwa kabla ya serikali ya wilaya kuwaondoa
wananchi hao ilikutana na wananchi kwa kufanya mikutano ya hadhara ukiwemo ule
wa machi 23 mwaka 2013 na kukubaliana mambo ya msingi tano.
Aliyataja mambo hayo wananchi waliyoyaomba kwa serikali kuyafanya ni
pamoja na kutotumia nguvu wakati wa kuwahamisha eneo la msitu wa Mzelezi,
kupatiwa mtaalam wa kupimiwa viwanja eneo la Isaka, kuimarisha miundombinu,
kupeana taarifa juu ya kuhama kwao, wananchi walipendekeza kuhamia kitongoji
cha Isaka na serikali iliendelea kufanya vikao mbalimbali juu ya azma hiyo.
Alisema Miti.
Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ulanga ilitoa ilani ya wananchi kuhama eneo
la hifadhi ya Mzelezi Augosti 5 mwaka 2013 na hadi kufikia Novemba 4 mwaka huo
wananchi walipewa muda wa miezi mitatu kuhama eneo la hifadhi huku serikali ya
kijiji ikiwasilisha barua ya kuomba wananchi kusaidiwa kubebewa mizigo yao
kutoka Mbangayao kwenda maeneo mengine ya wilaya ya Ulanga. Alisema Miti.
Miti akielezea changamoto mbalimbali zilizojitokeza alisema kuwa wilaya
ipo katika harakati za kukifanya kitongoji cha Isaka kuwa kijiji cha kisasa
kwani tayari wataalam wake wamepima viwanja 200 na tayari kuna majengo ya muda
ya shule ya msingi Mmbangayao huku ikiwa imejenga jengo lenye vyumba vitatu vya
madarasa vilivyofikia hatua ya kupa bati.
“Kitongoji cha Isaka kitakapo kamilika wenye wataamu waite Mbangayao au
Isaka kitakuwa kijiji cha kisasa na cha mfano wilaya mzima ya Ulanga kwani
kimepangiliwa kwa kutengewa maeneo ya soko, zahanati, shule na nyumba za ibada
na kazi tayari imeanza kufanyika kwa usimamizi uliomakini”. Alisema Miti.
WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI MBANGAYAO WAKIZECHEZA MUDA MFUPI BAADA YA MAPUMZIKO YA MASOMO.
Mkuu huyo wa wilaya ya Ulanga amegawa majukumu hayo ikiwemo ya
usimamizi wa barabara na shule kwa Afisa tarafa ya Vigoi wilaya ya Ulanga,
Maliki Salum Malupu aliyezunguza juu ya maendeleo ya kazi hiyo.
Malupu anasema kuwa kazi aliyopewa na mkuu wa wilaya ya Ulanga ni
usimamizi wa barabara yenye umbali wa kilimometa 7.9 iliyotengewa kiasi cha
sh9,00 milioni kutoka makutano ya barabara ya Mwaya-shule ya wasichana ya Regna
Mund hadi kitongoji cha Isaka pamoja na ujenzi wa shule ya msingi Mbangayao.
“Kuna kaya zaidi ya 150 ambazo zimekumbwa na zoezi la kuhama kijiji cha
Mbangayao na kitongoji cha Lupanga kwenda katika kitongoji cha Isaka hivyo
halmashauri yetu mpaka sasa tayari imepima viwanja zaidi ya idadi kamili ya kaya
177 na ujenzi utakapokamili kijiji hichi kitakuwa cha kisasa kwani kila maeneo
muhimu ya kijamii yametengwa”. Alisema Malupu.
Ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu kwa shule msingi
halmashauri ya Ulanga imetenga kiasi cha sh46 milioni kati ya fedha hizo sh21
milioni ikitengewa kwa ajili ya vyumba vitatu vya madarasa huku kiasi cha sh25
ikitengewa ujenzi wa nyumba ya mwalimu. Alisema Malupu.
Ujenzi wa madarasa matatu tayari yamejengwa na kilichobakia ni hatua ya
kuezeka bati, ujenzi wa choo cha wanafunzi upo katika hatua ya ujenzi wa shimo
huku ujenzi wa nyumba ya mwalimu ukiwa katika hatua ya msingi na vifaa vya
ujenzi vikiwemo mawe, mchanga vikiwa vimesogezwa eneo la ujenzi. Alisema
Malupu.
Malupu alisema kuwa tarafa anayoongoza ya Vigoi ina misitu mitatu mikuu
ambayo mji wa Mahenge inaitegemea kwa kuwa vyanzo vizuri vya mvua.
“Kuna misitu mitatu hii serikali inaiilinda kwa nguvu zake zote na
kuweka mikakati kabambe ili Mahenge isije kugeuzwa kuwa jangwa kama
ilivyofanyika tarafa ya Malinyi ambayo kwa sasa sehemu kubwa imegeuka kuwa
jangwa baada ya wafugaji kuvamia na kukata miti ovyo”. Alisema Malupu.
Alisema mikakati iliyowekwa na serikali kwa misitu iliyopo ni kulinda na
kuzia kwa shughuli zote za kibinadamu kulima, kukata kuni na miti, misitu hiyo
ikitajwa kuwa Mzelezi, Nawenge, na ndororo iliyopo tarafa ya Vigoi na misitu
mingine.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mbangayao David Eponda anasema baada ya
serikali kubomoa shule na kujenga majengo ya muda kitongoji cha Isaka hali ya
utoro imeongezeka mara dufu kutokana na kaya za wazazi wa wanafunzi wake
kujengwa umbali mrefu na eneo lililotengwa shule.
“Mpaka sasa mahudhurio ni mabaya kwa wanafunzi katika madarasa yote,
kwani darasa la saba kuna wanafunzi 13 lakini wanaofika shuleni ni sita huku
darasa la sita wapo nane wanaohudhuria masomo ni watatu wakati la tano wapo 28,
wanaofika nane”. Alisema Eponda.
Madarasa mengine ni kama ifuatavyo darasa la nne wapo 10 wanaofika
shuleni ni sita, la tatu wapo 28 na 12 ndiyo wanaohudhuria, la pili 21 na 16
ndiyo wanaosoma masomo wakati darasa la kwanza wakiwa 28, 24 ndiyo wanafika
shuleni.
Alisema shule hiyo mpaka sasa ina walimu wawili tu kati ya sita
waliokuwa wakifundisha kabla ya kijiji kuhamishwa lakini wengine wameshindwa
kufika kituo cha kazi haifahamiki kama watarejea kituo cha kazi ama laa na hali
hiyo.
“Ni kweli hapa kuna utoro na huu utoro unatokana na wanafunzi kuishi
eneo alilolopa mzazi wake, sasa wazazi wengine wanaishi katika mapango ya
Kipingo, Rock Athman, Mnazi na mengine madogo madogo na yenyewe yapo sehemu
tofauti tofauti na yana umbali mrefu hivyo utoro huo umechangiwa na suala hilo
la kuhamishwa wazazi wao tofauti na kula kijijini”. Alisema Eponda.
Eponda alisema kuwa shule iliyopo ni ile iliyojengwa kwa dharura pamoja
na nyumba za bati tatu, mbili zikitumika kama nyumba za kuishi na moja ofisi
lakini amejikuta akiishi pekee yake eneo hilo na kulazimika kulala mapema pale
ifikapo saa 12 jioni kuingia ndani kutokana ukimpya unaotawala eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment