MSAKO WA KUSAKA MAJANGILI WAFANIKISHA KUPATIKANA VIPANDE VYA 59 VYA MENO YA TEMBO VYENYE THAMANI YA SH176.7 MANYONI, IKIWA NI SAWA NA TEMBO 29 WALIOPOTEZA MAISHA.
MANYONI.
KIKOSI cha Kupambana na Ujangili Kanda ya Kati (KDU) kimefanikiwa kukamata vipande 59 vya meno ya tembo vikiwa na uzito wa zaidi ya kilo 200 vyenye thamani ya Sh176.7 milioni sawa na tembo 29.
Katika msako huo watu saba walikamatwa baada ya kukutwa na meno hayo, akiwamo ofisa mtendaji wa Kijiji cha Kayui wilayani Manyoni, Philomen Kanyonga aliyedaiwa kuongoza ujangili huo.
Akielezea tukio hilo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu juzi, mhifadhi mwandamizi wa Ngorongoro, Robert Mande alisema meno hayo yalikamatwa Machi 28 na 31.
Alisema kikosi kazi hicho kilianza kufuatilia mtandao wa ujangili katika kijiji cha Kiyombo na walifanikiwa kukamata meno hayo 53 ya tembo 26 katika kijiji hicho pamoja na bunduki aina ya SMG yenye namba 40129 ambayo alikamatwa nayo Eliud Selemani.
Alisema katika tukio hilo waliwakamata watuhumiwa watano ambao aliwataja kuwa ni Idd Waziri (29), Leonard Oscar (32), Ramadhani Said (40) na mtendaji huyo ambao wote walikutwa na meno hayo 53 ya tembo.
Mhifadhi huyo alisema katika kijiji cha Chinangali mkoani Dodoma walifanikiwa kukamata watuhumiwa wawili ambao ni David Makasi na Joseph Malima ambao walikutwa na meno sita yenye uzito wa kilo 31.1 yakiwa na thamani ya sh 27.3 milioni baada ya kuuawa kwa tembo watatu.
Baada ya kupokea maelezo hayo, Waziri Nyalandu alisema anataka kuona watuhumiwa hao wanahojiwa ili kujua watu wanaowatuma kufanya ujangili huo kwa kuwa sasa anataka kukamata majangili wakubwa ambao wamekuwa na mtandao mkubwa wa kuteketeza tembo nchini.
Alisema katika kuhakikisha wanaboresha ufanisi wa idara ya wanyamapori, wako katika mchakato wa kuifanya idara hiyo kuwa mamlaka inayojitegemea, ili kuweza kupambana na majangili hao.
“Hawa majangili wananiumiza kichwa kila siku; wanaua tembo wetu kwa ubinafisi wao,” alisema.
Sasa nataka nikamate majangili wakubwa kabisa wanaoendesha mtandao huu wa kumaliza tembo na pia sasa tuko katika hatua ya mwisho kwa ajili ya kuifanya idara ya wanyapori kuwa mamlaka kamili.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment