DAKTARI AELEZA NAMNA ALIVYOUGUA HOMA YA DENGUE, MPAPAI NAO UMO KATIKA TIBA YA DENGUE.
Dar es Salaam.
Daktari wa Hospitali ya Mwananyamala, Saleh Kijangwa amejitokeza na kueleza jinsi alivyougua homa ya dengue ambayo imeukumba Mkoa wa Dar es Salaam.
“Niliumwa sana, nikadhani ni malaria na nikahisi imekuwa kali kiasi hicho kwa sababu sikuwahi kuugua malaria maishani mwangu. Nilipima magonjwa mengi lakini hakuna kilichoonekana,” alisema
Dalili alizoona
Dk Kijangwa alisema alianza kuhisi maumivu makali ya kichwa usiku wa Ijumaa Kuu yaliyoambatana na maumivu ya misuli na viungo vya mwili na joto la mwili kuwa kali isivyo kawaida.
“Niliumwa sana kichwa, misuli, mgongo, kiuno na shingo. Maumivu yalikuwa makali kiasi nilishindwa kupata usingizi, wakati huo joto lilikuwa kali sana.”
Daktari huyo alisema kosa alilofanya ni kuamua kujitibu kwa kunywa dawa ya maumivu aina ya diclofenac ambayo kwa kawaida haipatani na maradhi hayo.
“Diclofenac ina tabia ya kuingiliana na utendaji kazi wa chembe hai hizo, hivyo mtu mwenye dengue akizinywa huathirika zaidi. Kujitibu ni kosa tunalolifanya mara nyingi. Ndiyo maana tunatakiwa tupime kwanza kabla ya kumeza dawa ya aina yoyote,” alisema.
Dk Kijangwa alisema alibainika kuwa na homa hiyo siku tano baada ya kuanza kuona dalili na kwa kuwa dengue haina tiba, alitibiwa kwa paracetamol na kutakiwa kunywa maji kwa wingi.
Kilichosababisha maambukizi
Dk Kijangwa alisema anahisi kilichosababisha yeye pamoja na wakazi wengi wa Wilaya ya Kinondoni kupatwa na ugonjwa huo ni uwepo wa bwawa la maji maeneo ya Kambangwa ambalo huenda ndicho chanzo cha mazalia ya mbu anayeambukiza maradhi hayo, Aedes Egyptiae.
Mpapai wadaiwa kutibu dengue.
Baadhi ya ripoti zimeonyesha kuwa majani ya mpapai yana uwezo wa kutibu homa ya dengue. Ingawa haijathibitishwa lakini historia inaonyesha kuwa majani ya mpapai yanatibu ugonjwa huo baada ya kulipuka mara kwa mara nchini India.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment