BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI KULIPA RIBA LA SH 5 BILIONI IKIWA NI DENI LA MIEZI SITA.


Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15, mjini Dodoma juzi na akiwa ameshikilia gazeti la Mwananchi. Picha na Edwin Mjwahuzi.

Dodoma.
Serikali italazimika kulipa hasara ya zaidi ya Sh5.2 bilioni (Dola za Marekani milioni 3.1) ambazo ni riba ya malimbikizo ya malipo ya miezi sita kwa Kampuni ya Jacobsen Elekron AS inayotekeleza awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa Kinyerezi, Dar es Salaam.
Gazeti hili limebaini kuwa kampuni hiyo ya Norway inaidai Serikali Dola 48.8 milioni (Sh80.52 bilioni), yakiwa ni malimbikizo ya malipo kuanzia Novemba mwaka jana na Mei mwaka huu.


Mbali ya hayo, kampuni hiyo ilitishia kusitisha utekelezaji wa mradi huo na kuondoa vifaa vyake kama isingelipwa walau Dola milioni 25 za Marekani (Sh41.25 bilioni) hadi Juni 15 mwaka huu.


Katika barua yake ya Juni 5, 2014 iliyosainiwa na Meneja wa Mradi wa Kinyerezi wa Jacobsen, Stein Sundbye kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kunakiliwa kwa Katibu Mkuu - Hazina na mwenzake wa Nishati na Madini, kampuni hiyo imelalamikia ucheleweshaji wa malipo hayo kinyume cha mkataba baina ya pande hizo mbili.


“Rejea barua yetu ya 23 Mei, 2014 iliyotoa ilani ya siku 14 kwamba tutasitisha kazi zetu kwa mujibu wa kipengele 41.2 cha mkataba, isipokuwa kama tutapokea malipo tunayodai ya Dola 48.8 milioni kama ankara ya madai iliyoambatanishwa hapa inavyoonyesha,” inasema sehemu ya barua hiyo na kuongeza:


“Kama tulivyoeleza ilani hii inamalizika Juni 6, 2014 wakati usitishaji wa kazi utakapoanza. Licha ya kuomba tulipwe au tuambiwe ni lini malipo hayo yatatolewa, hatujapokea majibu yoyote ya kupewa fedha zetu zote au kwa awamu kama ilivyokuwa imeahidiwa na Wizara ya Fedha katika barua yenye Kumbukumbu namba CDA.327/602/01 ya Aprili 4, 2014.


Laibuka bungeni
Juzi jioni, suala hilo liliibuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema Serikali imekuwa ikipata hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na kupanga utekelezaji wa miradi mikubwa pasipokuwa na uhakika wa fedha.


Akichangia hoja ya Bajeti ya Serikali, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) alisema: “Wakati Serikali ikitafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, tumekuwa tukiingia kwenye madeni ya ajabu ambayo kama tungekuwa makini yangeweza kuepukwa.


“Ninao mfano halisi hapa ambao unaonyesha jinsi Serikali itakavyolazimika kulipa riba ya zaidi ya Sh5 bilioni kutokana na kushindwa kulipa fedha za Kampuni ya Jacobsen inayojenga mradi wa Kinyerezi One, hii ni aibu kubwa maana tumelimbikiza madeni ya miezi sita na wanatudai Dola za Marekani 48 milioni.”


Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema hakuwa amepata taarifa kuhusu tishio la Jacobsen kusitisha mradi, lakini akaahidi kufuatilia ili kutoa taarifa baadaye... “Nafahamu kwamba Jacobsen tunafanya nao kazi tena vizuri sana, sidhani kama wanaweza kufikia hatua ya kusitisha kazi, ila ahsante kwa taarifa nitafuatilia ili kujua ukweli ni upi.”


Baadaye kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi Dk Likwelile alisema: “Naomba nikuhakikishie kwamba jitihada za kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika ni kipaumbele cha kwanza cha Serikali na mkataba baina ya Serikali na Jacobsen ni sehemu ya jitihada hizo. Nitashangaa sana iwapo jambo kama hilo litatokea pasipo sisi (Serikali) kufahamu na kuliridhia.”MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: