BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WABUNGE WAISAKAMA SERIKALI KWA KUITAKA KUBUNI VYANZO VYA MAPATO.

 
WABUNGE wameendelea kuitaka Serikali kubuni vyanzo vipya vya mapato, huku baadhi yao wakionesha wasiwasi kama Serikali itafanikiwa kukusanya Sh trilioni 19, kutokana na kukosa mbinu za upanuzi wa wigo wa kodi.
Pia, wabunge walio wengi walishauri Serikali ipunguze zaidi Kodi kwa Wafanyakazi (PAYE), wakitaka ifikie kwenye dijiti moja, kwa maelezo kuwa wafanyakazi ndio kada pekee, inayokamuliwa kila mwaka wakati baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wakiendelea kukwepa kodi.

Katika mjadala wa bajeti kuu, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, baadhi ya wabunge waliochangia, wametaka kiwango cha chini cha kukata kodi kiwe Sh 330,000 na kodi iwe asilimia tisa.

Aidha , suala la misamaha ya kodi limeendelea kupigiwa kelele na wabunge, huku baadhi wakitaka katika Sheria ya Fedha ya 2014/15, kiwekwe kipengele kuzuia misamaha hiyo kuzidi asilimia moja ya Pato la Taifa. PAYE Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF) alisema wafanyakazi wanatozwa kodi kubwa.

Alisema asilimia moja iliyopunguzwa ; kutoka asilimia 13 hadi 12, ni kidogo hivyo inafanya wafanyakazi watafute namna nyingine ya kuishi. Esta Matiko ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alishauri PAYE ipunguzwe hadi tarakimu moja kwa wale ambao wanapata mishahara midogo inayofikia Sh 700,000.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), katika mchango wake kwa maandishi, alisema nafuu ya kodi kwa wafanyakazi wa kima cha chini iliyotangazwa kutoka kiwango cha 13 mpaka 12, ni kidogo.

“Hakimsaidii mfanyakazi kubakia na fedha kwa ajili ya matumizi yake na pia kwa ajili ya kujiwekea akiba,” alisema Zitto.

Mbunge huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema ni dhahiri kuwa PAYE ni chanzo kikubwa cha mapato ya ndani ya Serikali.

Alitoa mfano, mwaka 2013/14 Serikali ilitarajiwa kukusanya Sh trilioni 1.5 kama PAYE , Sh trilioni moja kutoka idara ya walipa kodi wakubwa na Sh bilioni 500 bilioni kutoka idara ya kodi za ndani.

“Hata hivyo, utaona kuwa mapato haya ni sawa sawa na kodi inayosamehewa kupitia misamaha ya kodi hivyo iwapo misamaha ya kodi ikipunguzwa mpaka kiasi cha asilimia moja ya Pato la Taifa, Serikali itakusanya kodi ya kutosha kuziba pengo la punguzo la kodi kwa wafanyakazi,” alisema Zitto.

Zitto aliendelea kushauri, “Napendekeza kuwa kiwango cha chini cha kipato (mshahara) kukatwa kodi kiwe Shilingi 330,000 na kiwango cha chini cha kodi kiwe asilimia tisa.”

Alisisitiza kwamba kiwango hicho kinawezekana iwapo Serikali itachukua hatua dhidi ya matumizi mabaya ya fedha. Katika michango ya mbunge huyo na wengine, imeelezwa nchi haiwezi kuendelea kuendeshwa na fedha za wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wahisani.

Kampuni kubwa za uwekezaji nchini zimetakiwa zishiriki kuendesha Serikali kwa kulipa kodi stahili na kuondoa misamaha ambayo haina uhusiano na ukuaji wa ajira.

Vile vile baadhi ya wabunge, akiwemo Zitto walisema ni muhimu kuongeza juhudi za kukuza ajira ili kuwa na wafanyakazi wengi ambao watasaidia kuongeza mapato ya Serikali badala ya kukamua kundi dogo lililopo hivi sasa.

Huduma bure Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM) alisema Watanzania hakuna wanachopewa bure kwani wanachangia kila huduma wanayopatiwa.

"Watanzania ni kipi serikali inawapa bure, angalieni kitu kimoja cha kuwapa bure..kama ni elimu au ni afya au ni maji ijulikane, Hata kimoja tu tuseme hiki tunawapa bure Watanzania," alisema Chilolo.

Assumpta Mshama (Nkenge-CCM) alitaka Serikali ipunguze gharama za maisha ya wananchi ili wafaidike na uchumi unaodaiwa kuwa unapanda.

Mbunge huyo pia alisema ana wasiwasi, kama Serikali itafanikiwa kukusanya kodi mwaka huu, wakati mwaka unaoisha Serikali haikukusanya fedha za kutosha.

Alitoa mfano kuwa Serikali ilishindwa kukusanya mapato ya ndani na akahoji, “ kwa nini viwango havikufikiwa na kwa nini mwaka huu Waziri unadhani utafikia viwango hivyo hadi uongeze matumizi?”

Aidha alihoji sababu ya Serikali kukopa Sh bilioni bila kulihusisha Bunge. Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema) alisisitiza Serikali kuwekeza kwenye kilimo ili kutengeneza ajira kwa vijana.

Pia alishauri suala la viwanda lipewe kipaumbele kutengeneza bidhaa zitakazouzwa nje ya nchi na kupata fedha za kigeni.

Aden Rage ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM) alionesha wasiwasi kwa kuhoji, “ kama mwaka jana malengo yaliyowekwa hayakufikiwa, itakuwaje safari hii zitapatikana hizo Sh trilioni 19?” Deogratius Ntukamazima (Ngara-CCM) alitaka wizara kuondoa kasumba ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuliko kiasi kinachokusanywa.

Alipendekeza kuwe na kamati itakayosimamia ugawanyaji wa rasilimali za taifa ili mikoa ya pembezoni nayo ifaidike na rasilimali hasa fedha za maendeleo.

Alisema kuna haja ya kufuatilia matumizi ya Serikali na sio kumwachia CAG ambaye anafuatilia fedha ambazo tayari zimeshaibwa.

Wigo wa kodi Pia alisema uchumi hauwezi kuwa endelevu kama nchi itaendelea kutegemea wahisani.

Alishauri upanuzi wa wigo wa ukusanyaji kodi. Pia alishauri kilimo cha umwagiliaji kianzishwe mikoani ili kudhibiti vijana kwenda mijini.

Dalali Kafumu (Igunga-CCM) alishauri kuimarisha ukusanyaji wa kodi na hasa kodi ya majengo ili Serikali ipate fedha za kutosha za kuhimili bajeti.

Alitaka uwekezaji wa nje uvutiwe na waachwe kuitwa wezi. Alisisitiza kuwa wawekezaji wa ndani, washirikiane na wa kigeni kuimarisha uchumi.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: