WABUNGE SABA WALIOTIKISA BUNGE LA JAMHURI WA TANZANIA.
Dodoma.
Wabunge saba wamelitikisa Bunge tangu mkutano wa Bunge la Bajeti ulipoanza kutokana na michango yao binafsi.
Mwandishi wetu ambaye amekuwa bungeni tangu Mkutano wa Bajeti ulipoanza ametoa tathmini yake kuhusu michango ya wabunge iliyosisimua katika mjadala na kuibuka na orodha ya wabunge hao saba.
Hata hivyo, katika tathmini hiyo, majina ya wabunge ambao walichangia kwa niaba ya kamati au kutokana na nafasi zao za uwaziri au uwaziri kivuli hajayaingizwa katika orodha hiyo.
Tathmini hiyo imefanyika huku leo mjadala wa Bajeti ya Serikali ya 2014/15 ukihitimishwa tayari kwa kupigiwa kura na wabunge kesho, baada ya kukamilisha mfululizo wa mijadala ya bajeti za wizara zote za Serikali tangu Bunge hilo lilipoanza Mei 6, mwaka huu.
Hoja zilizoibuliwa na wabunge hao kwa nyakati tofauti ziliitikisa Serikali na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kiti cha Spika au aliyekuwa akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) kusimama kutoa ufafanuzi.
Waliotikisa.
Wabunge waliotikisa Serikali katika michango yao ni Ally Keissy (Nkasi Kaskazini - CCM), David Kafulila (Kigoma Kusini - NCCR-Mageuzi), Kangi Lugola (Mwibara - CCM), Dk Faustine Ndugulile (Kigamboni - CCM), Tundu Lissu (Singida Mashariki - Chadema), Abbas Mtemvu (Temeke –CCM) na Cecilia Paresso (Mbunge wa Viti Maalumu-Chadema) .
Kafulila.
Siku mbili baada ya Bunge kuanza Mei 8 mwaka huu, wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kafulila aliibuka na sakata la kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 milioni (Sh200 bilioni) akidai ni ufisadi uliofanywa na vigogo sita wa Serikali.
Aliwataja kwa majina vigogo hao na kusisitiza kuwa wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa kibiashara kati ya IPTL na Tanesco na Tanesco ilipeleka shauri hilo mahakamani kulalamikia gharama kubwa za uwekezaji wanazotozwa na IPTL, hivyo kuamuliwa fedha hizo ziwekwe humo hadi shauri litakapoamuliwa, lakini baadaye zilichotwa katika mazingira ya kutatanisha.
Lugola.
Lugola aliibuka Mei 10, mwaka huu katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na kusema kuwa Serikali ya CCM ambayo yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii huku akishangaa waziri mwenye dhamana ya kilimo, Christopher Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blaablaa.
Pia alimgeukia Naibu Waziri, Godfrey Zambi na kumwambia amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma bungeni akipaza sauti, baada ya kupata madaraka amewageuka wenzake na kushirikiana na waziri.
Akizungumza kwa sauti ya ukali ambayo mara nyingi haitarajiwi kwa wabunge wa CCM, Lugola alihoji inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki kama waziri.?MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment